Sunday 11 March 2018

ABDUL NONDO AREJESHWA DAR CHINI YA ULINZI MKALI WA POLISI

Abdul Nondo Arejeshwa Dar Chini ya Ulinzi Mkali wa Polisi
JESHI la Polisi Mkoa wa Iringa jana lilimsafirisha mwanafunzi wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM) aliyedai kupotea mapema wiki hii, Abdul Nondo (24) kwenda jijini Dar es Salaam kwa ajili ya uchunguzi.

Nondo ambaye ni Mwenyekiti wa Mtandao wa Wanafunzi Tanzania (TSNP), alidaiwa kutoweka kitatanishi usiku wa kuamkia Jumatano kabla ya juzi kupatikana akiwa mkoani Iringa.
Akizungumza na Nipashe jana kwa njia ya simu, Kamanda wa Polisi mkoa wa Iringa, Kamishna Msaidizi wa Polisi Juma Makanya alisema wamemsafirisha kwenda jijini Dar es Salaam kwa mahojiano zaidi.
“Leo (jana) tumemsafirisha kwenda Dar es Salaam kwa ajili ya uchunguzi zaidi kwa sababu huko ndipo alikotokea hadi kufika Iringa,” alisema Kamanda Makanya.
Alisema Jeshi la Polisi linaendelea kumshikilia mwanafunzi huyo kwa ajili ya uchunguzi zaidi wa kufahamu sababu ya tukio hilo.
Juzi Kamanda Makanya aliwaeleza waandishi wa habari kuwa Nondo anayesoma mwaka wa tatu katika Kitivo cha Sayansi ya Siasa na Utawala cha UDSM, aliripoti kwenye Kituo cha Polisi Mafinga wilayani Mufindi akiwa hana jeraha lolote, akidai kutelekezwa na watu wasiojulikana.
Alisema Jeshi hilo linamchunguza ili kufahamu kama Nondo ametoa taarifa za uongo kwa nia uovu ya kutaka kuhamasisha wanafunzi waandamane.
Kabla ya taarifa za kutoweka kwake, Nondo alizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam Jumanne na kumtaka Waziri wa Mambo ya Ndani, Mwigulu Nchemba ajiuzulu nafasi kutokana na kupigwa risasi na kuuwawa kwa aliyekuwa mwanafunzi wa Chuo cha Taifa cha Usafirishaji (NIT), Akwilina Akwilin mwezi uliopita.
Akwilina, aliyekuwa mwanafunzi wa Chuo cha Usafirishaji (NIT), aliuawa kwa kupigwa risasi akiwa ndani ya daladala wakati wa maandamano ya Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) jijini Februari 16.
Kutokana na mauaji hayo TSNP ilitoa tamko la kumtaka Mwigulu ajiuzulu nafasi yake kuonyesha uwajibikaji kutokana na kile ambacho jumuiya hiyo ilidai katika kipindi chake cha uongozi wizarani hapo, nchi imegubikwa na matukio mengi ya mauaji na utekaji wa raia pamoja na Jeshi hilo kutozingatia maadili yake ya kazi.
Baada ya kupotea, TSNP walitoa taarifa Kituo cha Polisi Chuo Kikuu cha Dar es Salaam na kufunguliwa jalada UD/RB/1438/2018.

No comments:

 

ADVERTISE WITH US

AFRICAN FASHION

PLACE YOUR ADS HERE!