Sunday, 18 June 2017

Upepo mkali, mawimbi makubwa kutikisa Pwani


Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA) imewatahadharisha wananchi kuhusu kuwapo upepo mkali na mawimbi makubwa baharini.



Taarifa ya mamlaka hiyo iliyotolewa leo (Jumapili) imesema upepo wa Pwani unatarajiwa kuvuma kwa kasi ya kilomita 40 kwa saa kwa Pwani yote, kutoka Kusini kwa Pwani ya Kaskazini na kutoka Kusini Mashariki kwa Pwani ya Kusini.
Mamlaka hiyo iliyo chini ya Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, imesema pia kutakuwa na mawimbi makubwa baharini.
TMA imesema utabiri huo wa hali ya hewa kwa saa 24 zijazo ni kuanzia saa tatu usiku wa leo.
Katika utabiri huo, TMA imesema hali katika mikoa ya Tanga, Dar es Salaam, Pwani na visiwa vya Unguja na Pemba kutakuwa na mawingu kiasi na mvua nyepesi katika maeneo machache na vipindi vya jua.
Mikoa ya Kagera na Mara, mamlaka imesema kutakuwa na hali ya mawingu kiasi, mvua na ngurumo katika maeneo machache na vipindi vya jua.
Huku kwa mikoa ya Arusha, Kilimanjaro na Manyara; Lindi na Mtwara; Mwanza, Geita, Shinyanga na Simiyu; Tabora, Katavi na Kigoma;
Rukwa, Iringa na Mbeya; Morogoro, Njombe na Ruvuma; na Singida na Dodoma kutakuwa na hali ya mawingu kiasi na vipindi vya jua.

No comments:

 

ADVERTISE WITH US

AFRICAN FASHION

PLACE YOUR ADS HERE!