Tuesday, 16 May 2017

Wanawake 2, kikongwe wauawa kikatili

WANAWAKE wawili wameuawa kikatili kwa kushambuliwa na mashoka na waume zao wa ndoa katika matukio mawili tofauti yaliyotokea mkoa wa Rukwa. Kaimu Kamanda wa Polisi mkoa wa Rukwa, Polycarp Urio amethibitisha kutokea kwa matukio hayo akisema chanzo ni wivu wa kimapenzi wa waume zao.


Wanawake waliouawa ni Theresia Baltazar ambaye wakati wa uhai wake alijulikana kwa jina lingine la Selemani (49) mkazi wa kijii cha Msia kilichopo Bonde la Ziwa Rukwa, Sumbawanga. Theresia aliuawa kikatili kwa kukatwa na shoka kichwani na shingoni na mumewe wa ndoa, Patrick Kipesa(39). Kwa mujibu wa Kamanda Urio, tukio hilo lilitokea Mei 14 mwaka huu saa 1.30 asubuhi kijiji cha Msia kata ya Milepa, tarafa ya Mtowisa, Sumbawanga.
“Baada ya mwanaume huyo kumuua mkewe kikatili naye alijiua kwa kujinyonga kwa kutumia kamba ya katani sebuleni kwake,” alisema. Inadaiwa chanzo cha kufanya mauaji hayo na yeye kujiua ni wivu wa kimapenzi baada ya kuhisi mkewe ana uhusiano wa kimapenzi na mwanaume mwingine ambaye hajafahamika kwa majina. Mwingine aliyeuawa ni Fatma Yusuph (22) mkazi wa Mtaa wa Sengetela Manispaa ya Sumbawanga.
Kwa mujibu wa Kaimu Kamanda, Urio Fatuma ameuawa kwa kukatwa panga shingoni na mzazi mwenzake aliyetoroka baada ya kutenda uhalifu huo na jitihada za kumsaka sheria iweze kuchukua mkondo wake zinaendelea. “Marehemu (Fatuma) alifika kituo cha Polisi kutoa taarifa ya kujeruhiwa akiwa na hali mbaya ambapo alipewa PF3 ili akatibiwe ndipo mauti ilimkuta akitibiwa hospitali ya rufaa ya mkoa wa Rukwa mjini Sumbawanga” alieleza Kamanda Urio.
Naye kikongwe Abel Sikazwe (90) aliyekuwa mgane kwa muda mrefu akiishi peke yake kwenye nyumba yake, aliuawa kwa kupigwa kichwani na kitu chenye ncha kali kisha kuvunjwa mkono na mguu kwa imani za kishirikina. Taarifa za uhakika kutoka kijiji cha Muzi zinaeleza kuwa tangu enzi za uhai wake marehemu Sikazwe alikuwa akihusishwa na ushirikina.
Kaimu Kamanda wa Polisi mkoa wa Rukwa, Polycarp Urio amethibitisha kutokea kwa matukio yote hayo ambapo alisema mtuhumiwa mmoja anashikiliwa na Jeshi la Polisi kwa mahojiano akihusishwa na mauaji ya kikongwe Sikazwe. Alisema marehemu Sikazwe aliuawa juzi akiwa amelala peke yake nyumbani kwake ambapo watu hao baada ya kumuua, waliutelekeza mwili wake mbele ya nyumba yake na kutokomea kusikojulikana.
Kaimu Ofisa Tarafa, Peter Mankambila alithibitisha kuwa kikongwe huyo alikuwa akiishi peke yake baada ya kufiwa na mkewe miaka kadhaa iliyopita. “Mwili wa marehemu huyo uligunduliwa na mjukuu wake wa kike wakati alipofika nyumbani kwake alfajiri kumsalimia. Ndugu wa marehemu waliutaarifu uongozi wa kijiji,” alieleza. Kamanda Urio alisema miili ya marehemu imekabidhiwa kwa ndugu zao kwa ajili ya maziko.

No comments:

 

ADVERTISE WITH US

AFRICAN FASHION

PLACE YOUR ADS HERE!