MFUKO wa Taifa wa Bima ya Afya (NHIF) umesema hakuna Mtanzania atakayekufa kwa sababu ya kukosa pesa za matibabu kutokana na Serikali kuweka mfumo mzuri unaohakikisha wananchi wote wanapata matibabu kwa gharama nafuu.
Umesema hautamvumilia mtu yeyote atakayehujumu huduma zake kwa kuwa umelenga kuwanufaisha wanachama na Watanzania wote. Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi wa NHIF, Anne Makinda alisema hayo mjini hapa wakati wa uzinduzi wa huduma za matibabu kutoka kwa madaktari bingwa itakayotolewa na mfuko huo mkoani Kigoma kwa wiki moja.
Alisema wananchi wote sasa wataweza kujiunga na huduma za matibabu za mfuko huo kupitia makundi mbalimbali yaliyopo kwenye jamii na kwamba, wananchi watapata huduma za matibabu nchi kote bila kubagua hospitali. Alisema NHIF inatambua kuwepo changamoto za uhaba wa dawa, vitendea kazi, uchache wa majengo na vifaa vingine vya kutolea tiba.
Makinda alisema Mfuko huo unatambua na kuzingatia changamoto hizo na kwamba sasa, unatoa mikopo kwa vituo vya afya, zahanati na hospitali ili kuwezesha huduma bora kupatikana wakati wote. Alitoa mwito kwa wananchi wote kuulinda mfuko huo na kujiunga na huduma zake kwa kuwa ni mfumo unaorahisisha upatikanaji wa huduma za matibabu na ndio mfumo unaotumika kote duniani.
Awali wa Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa NHIF, Bernad Konga alisema mfuko unatambua changamoto iliyopo ya uhaba wa madaktari bingwa nchini na kwamba, umeanzisha mpango wa huduma za madaktari bingwa wanaotembea ili kuweza kuwafikia wananchi.
Konga alisema kuwa mpango huo pia unalenga kutoa mafunzo kwa watoa huduma waliopo kwenye vituo vinatekeleza mpango huo ili waendeleze huduma husika baada ya madaktari bingwa hao kuondoka.
Alisema kuwa tangu kuanza kwa mpango huo jumla ya wananchi 13,000 wamefikiwa na kati yao, zaidi ya 600 wamepatiwa huduma za upasuaji wa magonjwa mbalimbali. Mkuu wa Mkoa wa Kigoma, Emmanuel Maganga alisema kumekuwa na uhitaji wa madaktari bingwa mkoani humo hasa ikizingatiwa kuwa, mkoa unao madaktari bingwa wawili pekee jambo linalowafanya wananchi kutumia muda na gharama kubwa kutafuta huduma hizo nje ya mkoa.
No comments:
Post a Comment