SUALA la Mkataba wa Ushirikiano wa Kibiashara (EPA) baina ya nchi wanachama wa Jumuiya ya wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) na Nchi za Umoja wa Ulaya (EU), sasa limechukua sura mpya.
Baada ya Tanzania na Uganda kugoma kusaini mkataba huo wa ushirikiano unaoonekana kuwa sawa na njia nyingine ya ukoloni, viongozi hao wamekubaliana kutuma ujumbe mjini Brussels, Ubelgiji yaliko makao makuu ya EU kwa lengo la kujadili kwa kina juu ya EPA.
Ujumbe huo ambao utaongozwa na Mwenyekiti mpya wa jumuiya hiyo na Rais wa Uganda, Yoweri Museveni (pichani) utakwenda huko ili kujadili nafasi ya kiuchumi ya EAC na pia kutoiadhibu Kenya kutokana na nchi wanachama kutosaini mkataba huo.
Akizungumza katika mkutano wa 18 wa wakuu wa nchi za EAC mara baada ya kukabidhiwa kijiti cha kuiongoza jumuiya hiyo na Rais John Magufuli Ikulu jijini Dar es Salaam jana, Rais Museveni alisema, ataongoza ujumbe huo ndani ya mwezi kuanzia jana na kwamba EU haipaswi kuiadhibu Kenya kwa nchi wanachama kutosaini mkataba wa EPA.
Alisema bado kuna mambo yaliyomo katika mkataba huo yanahitaji ufafanuzi na kuhoji Jumuiya hiyo itawezaje kusaini mkataba huo hali ya kuwa mwanachama wao amewekewa vikwazo na Umoja huo wa Ulaya.
“Tutawezaje kujadili na kusaini mkataba hali ya kuwa mwanachama wetu mmoja amewekewa vikwazo na EU ? bado tunahitaji ufafanuzi juu ya mambo kadhaa yaliyomo kwenye mkataba wa EPA,” alisema Museveni.
Aidha, Rais Museveni alieleza kutofurahishwa na hatua ya Umoja wa Ulaya kuiwekea vikwazo Burundi bila kushauriana na viongozi wa jumuiya hiyo. Alisema Burundi ni tatizo la jumuiya hiyo, hivyo wanaweza kulimaza wenyewe.
Tayari nchi za Kenya na Rwanda zimeshasaini mkataba huo, lakini ziko katika hatari ya kupoteza masoko yake ya nje katika nchi za Ulaya kutokana na kuonekana kama nchi zinazoendelea huku nchi nyingine za jumuiya hiyo zikioneokana kuwa chini.
Kutokana na nchi za Afrika Mashariki kuwa na Himaya Moja ya Forodha (Single Custom Territory) ni lazima nchi nyingine ambazo ni Tanzania, Burundi, Uganda na Sudan Kusini zisaini mkataba huo ili uweze kutekelezeka.
Awali, Mwenyekiti aliyemaliza muda wake, Rais Magufuli alisema, jambo hilo ni changamoto, kwani ameshindwa kulimaliza kwa wakati wake, lakini anaamini chini ya Rais Museveni litaweza kufikiwa mwafaka.
“Wakati tunaambiwa kusaini, Umoja huo huo umeiwekea vikwazo Burundi ambayo ni mwanachama wa jumuiya ya Afrika Mashariki, lakini wao kule wameshagombana wameacha, Uingereza imeshajitoa, kwa hiyo ilikuwa ni vigumu kwa sisi kuamua,” alisema Rais Magufuli.
Alisema ana uhakika chini ya Uenyekiti wa Rais Museveni atapambana na changamoto hiyo na kufikia mwafaka na kwamba yeye ameshindwa kulimaliza na hasa kwa sababu ya masharti yaliyomo kwenye mkataba huo.
Alisema masuala hayo watayazungumza na Umoja wa Ulaya juu ya kuangalia masuala yanayofanya Jumuiya hiyo ishindwe kusaini na kuangalia mwafaka wa Burundi ni mwanachama wa EAC, hivyo wakiondoa vikwazo juu ya nchi hiyo itasaidia kusaini mkataba huo.
Akikabidhi kijiti, alisema anajivunia kubana matumizi na kuokoa dola za Marekani milioni 3.415 (Sh bilioni 7) katika Sekretarieti ya EAC katika kipindi cha mwaka mmoja wa uongozi wake, huku akisifu kuongezeka kwa utawala bora.
Alisema, amebana na kupunguza matumizi hayo kutoka dola za Marekani milioni 12.6 (Sh bilioni 26) kwa mwaka zilizokuwa zikitumika kabla ya uongozi wake hadi kufikia dola milioni tisa (Sh bilioni 19).
“Nipongeze juhudi za Sekretarieti ya chini ya Katibu Mkuu (Liberat Mfumukeko) kwa kubana matumizi na Rais Museveni na wewe naomba uendelee hivyo hivyo,” alisema Rais Magufuli.
Alielezea kufurahishwa na maendeleo ya miradi mbalimbali ikiwemo ya ujenzi wa miundombinu huku mingine ikiendelea kutekelezwa. Mbali na Rais Magufuli na Museveni wengine waliohudhuria mkutano huo ni Naibu Rais wa Kenya, William Ruto aliyemwakilisha Rais Uhuru Kenyatta, Makamu wa Rais wa Kwanza wa Burundi, Gaston Sindimwo.
Wengine ni Mshauri Maalumu wa Masuala ya Uchumi wa Sudan Kusini, Aggrey Sabuni ambaye alimwakilisha Rais wa nchi hiyo, Salva Kiir na Waziri wa Biashara na Uhusiano ya Afrika Mashariki wa Rwanda, Francois Kanimba aliyemwakilisha Rais Paul Kagame. Marais hao pia walijadili masuala ya uchumi endelevu.
Katika mkutano huo pia aliapishwa Naibu Katibu Mkuu wa Jumuiya hiyo kutoka Tanzania, Stephen Mlote na Jaji wa Mahakamu ya Afrika Mashariki kutoka Sudan Kusini, Dk Charle Nyamwelo.
Mapema mwaka huu, Rais Magufuli na Museveni walikutana jijini Dar es Salaam na kukubaliana kuhakikisha wanatumia fursa zilizopo kuongeza biashara kati ya nchi hizo ili kukuza uchumi wa nchi hizo mbili.
Katika mazungumzo yao, Rais Magufuli alibainisha kuwa mazungumzo yao pia yalilenga suala la kusaini mkataba wa EPA ambapo alisisitiza Tanzania haitasaini mkataba huo akibainisha kuwa hiyo ni njia nyingine ya ukoloni.
Alisema: “Tumezungumza kwa kina na Rais Museveni na tumekubaliana kuendelea kulizungumza. Nimemueleza kuwa sisi Tanzania tunaona EPA haina faida na ni ukoloni mwingine, ambao unaletwa kwa sababu ya mambo mengi.
“Hatuwezi kuzungumzia kujenga viwanda wakati huo huo tunashindana na watu wenye viwanda vikubwa…Na yeye Rais Museveni amesema kimsingi anapenda kufanya kitu chenye faida.”
Kwa upande wake, Rais Museveni alisema kutokana na msimamo wa Tanzania katika suala la EPA, ameamua kuja kufanya mazangumzo na Rais Magufuli ili kuwa na msimamo wa pamoja.
No comments:
Post a Comment