Monday 22 May 2017

Hadhari ya Ebola iwe nchi nzima

GAZETI hili toleo la juzi liliandika habari kuhusu hadhari dhidi ya ugonjwa wa ebola katika mikoa ya Mwanza na Mara. Habari hiyo yenye kichwa cha habari ikasema mikoa ya Kanda ya Ziwa ambayo ni miongoni mwa mikoa iliyotajwa na Wizara ya Afya, inatakiwa kuchukua tahadhari zaidi dhidi ya ugonjwa huo ambao umeripotiwa kuwapo nchi jirani ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC).

Lakini jana tukawa na habari kama hiyo kutoka mikoa ya Rukwa na Katavi ikiwa imebeba kichwa cha habari: Katavi wahadharishwa juu ya ebora. Tukumbuke kuwa kuwepo kwa hadhari hizo katika mikoa hiyo inatokana na ukweli kwamba Tanzania inapakana na DRC nchi ambayo Shirika la Afya Duniani (WHO) limethibitisha kuwa na ugonjwa huo.
Habari hizo zilisema mikoa hiyo ya Kanda ya Ziwa, Katavi n Rukwa imeanza kuchukua hatua madhubuti kuelimisha umma umuhimu na namna ya kujihadhari na maambuziki ya virusi vya ugonjwa huo unaoambatana na mgonjwa kutoka damu kwenye matundu yote ya mwili.
Mganga Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, Dk Leonard Subi alinukuliwa akisema hadhari inayochukuliwa ni pamoja na kupima afya za wasafiri wote wanaoingia nchini kupitia mipaka ya mkoa huo ili kubaini kama wana dalili au virusi vya ebola.
Ikumbukwe kuwa, Mkoa wa Mwanza ni kitovu cha biashara katika mikoa ya Kanda ya Ziwa na nchi jirani zote ambazo ni wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki Mkoani Mara, Mkuu wa Mkoa huo Dk Charles Mlingwa ameagiza watendaji wa sekta ya afya kuhakikisha wananchi wanakuwa salama dhidi ya ugonjwa huo kwa kuwa mkoa huo uko mpakani.
Ameripotiwa akisisitiza wananchi kuepuka mikusanyiko isiyo ya lazima na kupata huduma za afya haraka wanapojisikia homa kali ambayo ni moja ya dalili za virusi vya ebola. Huko Katavi Mkuu wa Mkoa huo, Raphael Muhuga jana hili alinukuriwa na gazeti akiwataka wanavijiji vya Ikola na Karema vilivyopo kwenye mwambao wa ziwa Tanganyika, kuchukua hadhari ya kutosha.
Sisi tunaipongeza Wizara kwa kutambua mapema hatari iliyopo ya uwekezakano wa maambukizi toka nchi jirani na kutangaza hatua za tahadhari kuchukuliwa katika mikoa hiyo. Tunasema, licha ya Wizara kuweka msisitizo katika mikoa ya mipakani, haimaanishi kuwa mikoa mingine ilale usingizi, bali itumie msemo kuwa, mwenzio akinyolewa wewe tia maji.
Kwa msingi huo, tunashauri wakuu wa mikoa, wilaya na viongozi wengine katika ngazi za kiutawala wakisaidiana na waganga wakuu na wafawidhi, kuanza kutoa elimu sahihi na ya kutosha katika maeneo yao kwa nchi nzima kuhusu dalili, madhara na namna ya kujikinga au kutibu ugonjwa huo.
Nasi tunashauri wananchi wachukue tahadhari wakizingatia kuwa mlinzi wa kwanza wa mtu, ni mtu mtu mwenyewe hivyo wazingatie kanuni zote za afya, waepuke mikusanyiko isiyo ya lazima zikiwamo sherehe.
Tunasema, waepuke hata tabia ya kushikana mikono au kusalimiana kwa mikono hususani na watu wageni kwa kuwa hakuna ajuae wametoka wapi na wameathirika vipi. Tunaipongeza Serikali kwa kushituka mapema, tunaishauri iweke nguvu kubwa katika upimaji mipakani, utoaji wa elimu na pia ijiandaye kwa wataalamu na watoa huduma wa kutosha, dawa na kambi maalumu kwa wanaobainika kuathitika ili kuepusha maambukizi zaidi.
Sisi tunaamini haya na mengine mengi ya kitaalamu yakizingatiwa, tutashinda mtihani wa kuepuka maambukizi ya virusi vya ebola toka nchi jirani na Tanzania tutakuwa salama endapo kila mmoja atahusika.

HABARI LEO

No comments:

 

ADVERTISE WITH US

AFRICAN FASHION

PLACE YOUR ADS HERE!