Tuesday 24 January 2017

Tanzania na Uturuki kubebana kiuchumi

RAIS wa Uturuki, Recep Tayyip Erdogan ameimwagia neema Tanzania ambapo takribani mikataba tisa inayogusa maeneo ya kilimo, afya, elimu, diplomasia, uchukuzi, habari, ulinzi na viwanda imesainiwa.


Aidha, nchi hiyo ya barani Ulaya pamoja na Tanzania zimekubaliana kuongeza thamani ya biashara baina yake kutoka dola za Marekani milioni 160 mpaka milioni 190 za sasa hadi kufikia dola za Marekani milioni 250.
Pamoja na hayo, Erdogan ameihakikishia Tanzania na Afrika kwa ujumla kuwa sera ya nchi yake kwa Afrika ni usawa na si sera zinazofurahisha upande mmoja na kuukandamiza mwingine. Marais hao wawili akiwemo Rais John Magufuli, walishuhudia mikataba hiyo tisa ikisainiwa na mawaziri wa pande zote mbili Tanzania na Uturuki Ikulu jijini Dar es Salaam.
Mikataba iliyosainiwa ni pamoja na mkataba wa ushirikiano baina ya Kampuni ya Ndege Tanzania (ATCL) na Shirika la Ndege Uturuki (Turkish Airline), ushirikiano baina ya Shirika la Utangazaji Tanzania (TBC) na Shirika la Utangazaji Uturuki na mkataba wa ushirikiano katika maendeleo baina ya nchi hizo mbili.
Mikataba mingine ni pamoja na ushirikiano katika sekta ya elimu na utafiti, ushirikiano baina ya Shirika la Viwanda Vidogo (SIDO) na Shirika la Viwanda vya Kati Uturuki na ushirikiano katika sekta ya utalii kwa nchi zote mbili.
Pia mikataba mingine iliyosainiwa ni ushirikiano katika viwanda na ulinzi, kwenye sekta ya afya na ushirikiano baina ya Chuo cha Diplomasia cha Tanzania na cha Uturuki.
Mawaziri wa Tanzania walishiriki kusaini mikataba hiyo ni Waziri wa Maliasili na Utalii, Profesa Jumanne Maghembe, Waziri wa Fedha na Mipango, Dk Philip Mpango, Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Ummy Mwalimu na Naibu Waziri wa Elimu, Sayansi, Teknolojia na Ufundi, Stella Manyanya.
Wengine ni Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Augustine Mahiga, Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa, Dk Hussein Mwinyi, Waziri wa Viwanda, Biashara na Uwekezaji, Charles Mwijage na Mkurugenzi Mkuu wa TBC, Dk Ayoub Rioba.
Akizungumza katika shughuli hiyo, Dk Magufuli alimshukuru Rais Erdogan kwa kuichagua Tanzania kuwa nchi ya kwanza kuitembelea katika ziara yake Afrika, jambo lililosababisha nchi hiyo kumwagiwa neema ya mikataba tisa yenye lengo la kuboresha na kuimarisha sekta husika kwa nchi zote mbili.
“Katika kabila langu kuna methali inayosema ukiwa wa kwanza kunywa maziwa maana yake utakunywa mengi zaidi. Hili limejidhihirisha kupitia mikataba hii tuliyotiliana saini itakayonufaisha zaidi Tanzania,” alisisitiza Dk Magufuli.
Alisema hivi karibuni Tanzania imeteua Balozi wa Tanzania nchini Uturuki kwa mara ya kwanza, Profesa Elizabeth Kiondo, ikiwa ni ishara na msingi imara kuimarisha ushirikiano baina ya nchi hizo mbili hasa katika kushirikiana kibiashara na kiuwekezaji.
Rais Magufuli alisema anaamini kupitia ushirikiano huo mpya wa kidiplomasia nchi hizo zitaimarisha zaidi uhusiano wake kwa upande wa maendeleo kwani tayari katika mazungumzo aliyoyafanya na Rais Erdogan amemuomba kupitia Benki ya Exim ya Uturuki kuikopesha Tanzania fedha zitakazotumika katika ujenzi wa reli ya kisasa.
“Tanzania tuko kwenye mchakato wa ujenzi wa reli ya kisasa itakayounganisha nchi yetu na nchi nyingi za jirani. Kwa sasa tupo kwenye hatua ya kutafuta mkandarasi na nafahamu moja ya kampuni kutoka Uturuki imeomba kuijenga reli hii. Tuombe Mungu mfanikiwe katika hili,” alisema Dk Magufuli.
Aidha, alifafanua hali ya biashara baina ya Uturuki na Tanzania kuwa inazidi kuimarika kwani kwa sasa biashara imefikia kiasi cha dola za Marekani 190 na kampuni 30 za Uturuki zimewekeza nchini kwa thamani ya dola za Marekani 305.08 zilizotengeneza ajira 2,950.
“Nina uhakika kupitia ushirikiano huu, sasa tutaongeza kiwango cha biashara zetu kutoka dola za Marekani 190 hadi 250 na kuimarisha maeneo mengine ya uwekezaji. Uturuki ni nchi ya saba duniani kwa kuzalisha mazao ya kilimo hivyo kuja kwakwe nchini kwetu ambako kuna takribani asilimia 80 ya Watanzania wakulima, kutatunufaisha,” alifafanua.
Kwa upande wake, Rais wa Uturuki Erdogan alisema mazungumzo yake na Rais Magufuli yameonesha mafanikio makubwa baina ya nchi hizo mbili na yamegusa maeneo nyeti yanayowagusa wananchi ambayo ni elimu, afya, uchukuzi, diplomasia na viwanda.
Alisema katika ziara yake nchini ameambatana na wafanyabiashara takribani 150 ambao aliihakikishia Tanzania kuwa wako tayari kuwekeza katika nyanja mbalimbali, jambo ambalo pamoja na kuchangia katika uchumi lakini pia litaongeza ajira.
Aidha, aliahidi kuongeza fursa zaidi katika maeneo ya elimu na ulinzi ambayo nchi hiyo imekuwa ikitoa udhamini wa mafunzo. Kwa sasa takribani wanafunzi 4,500 hupata ufadhili wa kwenda kusoma Uturuki.
Akizungumzia mchango wa nchi hiyo kwa nchi za Afrika, Rais huyo alibainisha kuwa sera ya nchi yake kwa nchi za Afrika ni usawa hivyo makubaliano yote waliyoyasaini na kukubaliana kushirikiana yamelenga kuwaletea maendeleo wananchi wa Tanzania na Uturuki.
Alisema Tanzania imeingia makubaliano ya mikataba mbalimbali na Uturuki ikiwemo katika eneo la uchukuzi kupitia shirika la ndege la Uturuki ambalo kwa sasa ndio linalounganisha nchi zote za Afrika. “Tunataka kuwapa uzoefu, tumefanya hivi kwa sababu Tanzania ni nchi yenye amani, ukarimu, upendo na utulivu.
” Pamoja na hayo, Rais Erdogan alielezea tukio la kuponea chupuchupu kupinduliwa Julai 15, mwaka jana ambapo watu 240 walipoteza maisha na wengine 2,900 kujeruhiwa. “Nashukuru Mungu raia wa Uturuki waliitetea demokrasia ya nchi yao na napenda kuwataarifu kuwa tuna ushahidi wa kutosha kuwa waliofanya jaribio lile la mapinduzi ni wanachama wa chama cha kigaidi cha kundi la Fethullah,” alisema.
Alizionya nchi za Afrika na Tanzania kwa ujumla kuwa makini na kundi hilo kwani lipo katika nchi mbalimbali duniani ikiwemo Afrika. “Naamini rafiki yangu Magufuli atanisaidia katika hili, nchi yangu imejipanga kupambana na kundi hili kikamilifu,” alieleza.
HABARI LEO.

No comments:

 

ADVERTISE WITH US

AFRICAN FASHION

PLACE YOUR ADS HERE!