SERIKALI imewataka wananchi watakaotozwa fedha ili kupatiwa damu hospitalini watoe taarifa kwa mamlaka husika ili wahusika wachukuliwe hatua stahiki, ikisisitiza kumuuzia damu mgonjwa ni kosa lisilovumilika.
Aidha, imesema tangu Mpango wa Taifa wa Damu Salama uanze, imeibuka tabia ya baadhi ya watumishi wa afya wasio waaminifu kuwauzia damu wagonjwa, jambo ambalo ni kinyume cha sheria.
Kauli hiyo ya serikali imetolewa na Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Ummy Mwalimu kwenye uzinduzi wa kampeni ya “Bodaboda Changia Damu Mwenzio Aishi” iliyofanyika jana katika Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH), iliyoandaliwa na Taasisi ya APEC, Chama cha Bodaboda Mkoa wa Dar es Salaam, MNH na Mpango wa Taifa wa Damu Salama ambapo pia baadhi ya waendesha pikipiki walichangia damu.
Ummy aliyewakilishwa na Meneja wa Kanda ya Mashariki wampango wa Taifa wa Damu Salama (NBTS), Dk Avelina Mgasa alisema mpango wa damu salama hutoa damu bila malipo kwa hospitali zote zinazotoa tiba ya damu, hivyo wagonjwa wanatakiwa kupewa damu bure.
“Maisha ya watu wengi yanaokolewa kila mwaka nchini kwa kuongezewa damu, nchini kinamama wengi na watoto hupoteza maisha kwa kukosa damu,” alisema.
Alisema takwimu za hivi karibuni nchini zinaonesha makundi yanayotumia damu kwa kiasi kikubwa ni wajawazito kwa asilimia 30, watoto wenye umri wa chini ya miaka mitano kwa asilimia 50, ajali za mara kwa mara zikiwamo za madereva wa bodaboda asilimia 15 na magonjwa mengine kama saratani, upasuaji mkubwa wa moyo kwa asilimia tano.
Aliongeza kuwa, mpango huo haujafikia lengo la kukusanya chupa za damu zinazokidhi mahitaji ya nchi nzima.
Alisema mahitaji ya damu katika mkoa wa Dar es Salaam wenye hospitali takribani 120 zinazotoa huduma ya kuongezea wagonjwa damu ni wastani wa chupa 4,500 kwa mwezi, lakini damu iliyokusanywa na na Mpango wa Taifa wa Damu Salama kupitia Kanda ya Mashariki ni chupa 2,000 sawa na asilimia 50 ya mahitaji.
Alisisitiza kuwa damu ni uhai na haipatikani kwa njia nyingine isipokuwa kwa kuchangiwa na binadamu mwingine, hivyo jamii inapaswa kuona umuhimu wa kuchangia damu kwa hiari.
Katibu wa Chama cha Madereva na Wamiliki wa Pikipiki Dar es Salaam, Daud Laurian alisema, kupitia kampeni hiyo wamejipanga kuhakikisha wanachangia damu isiyopungua lita 200 katika benki ya damu.
No comments:
Post a Comment