Monday 5 December 2016

Ndege 4 za abiria kuwasili kabla ya Juni 2018




Rais wa Tanzania Dkt. John Magufuli

 Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli 
amekutana na kufanya mazungumzo na Mkurugenzi wa Masoko ya Afrika 
wa Kampuni ya utengenezaji wa ndege ya Boeing yenye makao yake nchini 
Marekani Bw. Jim Deboo.


Mazungumzo hayo ambayo ni sehemu ya juhudi za Serikali za kununua ndege kubwa kutoka kampuni hiyo, yamefanyika Ikulu Jijini Dar es Salaam na kuhudhuriwa na Katibu Mkuu Uchukuzi Dkt. Leonard Chamriho na Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha na Mipango Bw. Doto James.
Baada ya Mazungumzo hayo Rais Magufuli amesema Serikali yake ya Awamu ya Tano imedhamiria kununua ndege nyingine nne zikiwemo ndege kubwa 3 ambazo zitasaidia kuinua uchumi wa nchi kwa kuwezesha watalii kuja hapa nchini moja kwa moja kutoka nchi zao.
"Sisi hapa tunazungumza kuwa watalii hawajafika hata milioni 2 kwa mwaka, lakini nchi kama Morocco inapata watalii zaidi ya milioni 12 kwa mwaka, hii yote ni kwa sababu hatuna mashirika ya ndege ya kwetu, watalii wakitaka kuja hapa ni lazima waje kwa kuungaunga, wafikie nchi nyingine halafu ndipo wapate moyo wa kuja huku, licha ya kwamba sisi Tanzania ni miongoni mwa nchi 5 duniani zenye maeneo mazuri yenye utalii. 
"Kwa hiyo niwaombe tu Watanzania wapende mali zao, kwa sababu wakati mwingine nikiangalia mitandao na magazeti ni ajabu huwezi kuamini kama hao ni Watanzania, unakuta wanasifia tu ndege za watu wengine na wanazibeza za kwao" amesisitiza Rais Magufuli.
Mhe. Rais Magufuli ametaja aina ya ndege mpya ambazo Serikali itazinunua kuwa ni ndege 1 aina Bombardier Q400 Dash 8 NextGen inayotarajiwa kufika nchini Mwezi Juni 2017, ndege 2 aina ya Bombardier CS300 zenye uwezo wa kuchukua kati ya abiria 137 na 150 na zinazotarajiwa kuwasili nchini kati ya Mei na Juni, 2018 na ndege moja aina ya Boeing 787 Dash 8 Dream Liner yenye uwezo wa kuchukua abiria 262 na inayotarajiwa kuwasili nchini Juni, 2018. Malipo ya awali kwa ndege hizi yameshafanyika.
Dkt. Magufuli amewataka Watanzania kuunga mkono juhudi hizi za Serikali zenye lengo la kuinua utalii na kuimarisha uchumi wa nchi.
"Tumeleta ndege aina ya Bombardier hapa, zimepunguza gharama za safari mfano kutoka Dar es Salaam hadi Mwanza, sasa wanalipa kati ya 160,000/ hadi 200,000/- wakati nauli ilishafika Shilingi laki 8 na kitu, lakini watu wengine utakuta wanazungumzazungumza wee maneno ya hovyo kwa kutumiwa, tumeshaamua na tutafanya hivyo" amesisitiza Rais Magufuli.

EATV.

No comments:

 

ADVERTISE WITH US

AFRICAN FASHION

PLACE YOUR ADS HERE!