WIZARA ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto imelaani vikali mauaji ya mtoto Witness Andrew (9) ambaye alichunwa ngozi na watu wasiojulikana. Wizara hiyo imeziagiza mamlaka husika kuhakikisha zinawasaka na kuwakamata watuhumiwa waliofanya ukatili huo.
Witness alitekwa wakati akichunga mifugo. Ameuawa wakati dunia na taifa likiwa linaadhimisha Siku 16 za kupinga Ukatili wa Kijinsia.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Msemaji wa wizara hiyo, Erasto Ching’oro, wizara imesikitishwa na mauaji ya mtoto huyo ambaye alitekwa na baadaye kuokotwa akiwa amechunwa ngozi wilayani Karatu katika Mkoa wa Arusha.
“Wizara imesikitishwa na mauaji ya binti huyo... mauaji haya ni ukatili wa hali ya juu na ni ukiukwaji mkubwa wa haki ya kuishi ya mtoto ambayo ndiyo haki ya msingi kati ya haki zote za mtoto,” ilieleza taarifa hiyo.
Taarifa hiyo ilieleza kuwa haki ya kuishi inapovunjwa ndani ya jamii inatia doa jamii husika katika kujenga jamii inayofaa kuwa mahali salama kwa mtoto kuishi.
Wizara hiyo ilisema kuwa inaamini mamlaka zinazohusika na ulinzi wa mtoto dhidi ya ukatili katika Mkoa wa Arusha hususan wilaya ya Karatu, zitahakikisha watuhumiwa wanasakwa na kukamatwa ili sheria stahiki iweze kuchukua mkondo wake.
Kutokana na hatua hiyo, wizara hiyo imepanga kuzindua Mpango Kazi wa taifa wa Kutokomeza Ukatili wiki ijayo.
Mpango huo ambao ni jumuishi unalenga kuendeleza juhudi za serikali na wadau katika kushirikiana kwa pamoja kuzuia ukatili na kutoa huduma stahiki kwa waathirika.
Wizara hiyo imetoa pole kwa wazazi, ndugu na familia ya mtoto huyo ambaye ameuawa katika umri mdogo na kuwataka kuwa wavumilivu katika kipindi cha matatizo hayo.
No comments:
Post a Comment