Sunday, 20 November 2016

Watu 96 Wafariki Baada ya Treni Kuacha Njia India

treni
WATU zaidi ya 96 wamefariki dunia leo baada ya mabehewa 14 ya treni kuacha njia kaskazini mwa Jimbo la Uttar Pradesh, India.
Ajali hiyo iliyohusisha treni linalosafiri kati ya Indore na Patna ilitokea saa tisa usiku wa kuamkia leo karibu na mji wa Kanpur ambapo waokoaji walibidi kuyakata mabehewa yaliyokuwa yamejikunja ili kutoa  watu wapatao 150 ambao walijeruhiwa. 


Mabehewa yaliyohusika katika ajali hiyo  ni yale yaliyokuwa mbele karibu na injini.
Chanzo cha mabehewa hayo kuacha njia karibu na Kijiji cha Pukhrayan hakikufahamika.  Krishna Keshav aliyekuwa anasafiri katika treni hilo, aliliambia shirika la habari la BBC: “Tuliamka kwa mshituko kunako saa tisa.  Mabehewa kadhaa yaliacha njia, kila mtu alishituka.   Niliona watu kadhaa waliokufa na waliojeruhiwa.”
ajali-ya-treni-1
Wananchi wakiwa eneo la tukio.
Ofisa mmoja wa reli jijini Delhi, Anil Saxena, alisema watu wengi  walikuwa wamenaswa kwenye mabehewa hayo na  polisi wapatao 250 walipelekwa kusaidia uokoaji ambapo baadhi ya walionusurika ni watoto.
Waziri Mkuu wa India, Narendra Modi, ametuma salamu za rambirambi kwa wafiwa kupitia mtandao akielezea masikitiko yake kuhusu ajali hiyo ambapo alisema alikuwa amepewa maelezo na Waziri wa Reli, Suresh Prabhu.

Ajali mbaya zaidi za treni nchini India:
  • Watu 250 walikufa huko Bihar, Juni 6, 1981 treni lilipoacha njia darajani na kutumbukia katika mto Baghmati ambapo mamia ya watu hawakupatikana na kufanya makadirio ya vifo kuwa kati ya 500 na 800.
  • Watu 358 walifariki huko Firozabad, Agosti 20, 1995 ambapo treni liligonga treni lililokuwa limesimama.
  • Watu wasiopungua 290 walikufa huko Gaisal, Assam, Agosti 2, 1999 treni mbili zilizokuwa zimebeba abiria 2,500 zilipogongana.
ajali-ya-treni-2
Ajali ya Gaisal, Assam, Agosti 2, 1999 iliyoua watu 290.
  • Watu zaidi ya 212 walikufa huko Khanna, Novemba 26, 1998 treni moja lilipogongana na lile ambalo lilikuwa limeacha njia.
  • Huko Rafiganj, treni liliacha njia kwenye daraja Septemba 10,2002 na kuua watu zaidi ya 130.
  • Watu zaidi ya 100 walikufa huko Midnapore, West Bengal, Mei 28,  2010 wakati treni lenye kusafiri kati ya Calcutta na Mumbai lilipoacha njia.

No comments:

 

ADVERTISE WITH US

AFRICAN FASHION

PLACE YOUR ADS HERE!