IDADI ya washitakiwa katika mashitaka ya mauaji ya watafiti wa Selian imefikia 17 baada ya wanne kuunganishwa katika kesi hiyo jana.
Washitakiwa wote wanajitetea wenyewe katika kesi hiyo. Awali walikuwa wakituhumiwa kwa pamoja.
Oktoba Mosi mwaka huu katika kijiji cha Iringa Mvumi, tarafa ya Makang'wa, wilaya ya Chamwino, mkoani Dodoma, watafiti wawili na dereva wa Kituo cha Utafiti cha Udongo na Maendeleo ya Ardhi cha Selian, Nicas Magazine, Theresia Nguma na Faraji Mafuru, ingawa walijitambulisha, waliuawa na gari lao lenye namba za usajili STJ 9570 aina ya Toyota Hilux Double Cabin, lilichomwa moto.
Washitakiwa wanne ambao wameungana na wenzao walisomewa kila mmoja shitaka la mauaji ya watafiti hao wawili kwa kuwadhania kuwa ni wanyonya damu.
Akisoma mashtaka yao mbele ya Hakimu Mkazi wa Mahakama ya Mkoa wa Dodoma, Joseph Fovo, Wakili wa Serikali, Beatrice Nsana, alisema kuwa kila mshitakiwa anakabiliwa na kosa la kuua kwa kusudia ambapo waliwaua Nicas Magazine, Theresia Nguma na Faraji Mafuru kinyume na kifungu cha sheria cha 196 na 197 cha kanuni ya adhabu.
Aidha alifafanua kuwa kutokana na washitakiwa hao kuongezeka, aliiomba mahakama hiyo, kubadilisha hati ya mashitaka kwa mujibu wa sheria namba 234 kifungu kidogo cha kwanza sura ya 20 ya Sheria ya Mwenendo wa Makosa ya Jinai kama ilivyofanyiwa marekebisho mwaka 2002.
Wakili huyo aliwataja washitakiwa walioongezeka katika kesi hiyo kuwa ni Bruno Lebedu, Jonas Makwawa, Erasto Masaka na Juma Chitongo.
Wengine ni Cesilia Mwalu, Dorca Mbehu, Edna Nuno, Grace Masaulwa, Juma Madeha, Alberth Chimanga, Sosteness Mseche, Julius Chimanga, David Chimanga, Lazaro Kwanga, Yoram Samamba, Edward Lungwa na Simon Samamba.
Hakimu Mkazi, Fovo aliwataka watuhumiwa hao kutojibu chochote hadi hapo upelelezi utakapokamilika na watuhumiwa wote 17 wamerudishwa rumande.
Oktoba 17 mwaka huu watu hao kwa pamoja walishtakiwa kwa kosa la kuwaua watumishi hao. Kesi hiyo imeahirishwa hadi itakapotajwa tena Novemba 28 mwaka huu.
No comments:
Post a Comment