Wednesday 16 November 2016

Panga la NACTE latua vyuo 26

BARAZA la Taifa la Elimu ya Ufundi (NACTE) limevifungia vyuo vya ufundi 26 kutokana na makosa mbalimbali, ikiwamo kushindwa kuzingatia masharti yaliyowekwa na kutoa mafunzo ambayo hayajathibitishwa.


Pia baraza hilo limesimamisha programu zisizosajiliwa katika vyuo 20, huku vyuo viwili vikisimamishwa kutokana na kutokuwa na usajili wa baraza hilo.
Akizungumza na waandishi wa habari Dar es Salaam jana, Kaimu Katibu Mtendaji wa Nacte, Dk Adolf Rutayuga, alisema wamekuwa wakifuatilia vyuo vya ufundi ili kuona kama vinafuata viwango vya ubora wa kitaaluma vilivyowekwa na Nacte katika kutoa mafunzo.
“Kama ilivyoelezwa katika sheria za Usajili na Kanuni za leseni, kutozingatia matakwa yoyote yaliyowekwa na Nacte ni kosa kisheria. Kanuni zinasema kuwa hatua kali zinaweza kuchukuliwa kwa kila kosa,” alisema Dk Rutayuga.
Dk Rutayuga alisema kulingana na matokeo ya ufuatiliaji uliofanywa na timu maalumu, baraza hilo lina uwezo wa kuchukua hatua dhidi ya taasisi au vyuo vinavyoshindwa kutekeleza kanuni zilizowekwa.
Alisema baada ya kufanya utafiti wao, wamebaini vyuo 26 vilishindwa kuzingatia masharti yaliyowekwa na Nacte katika cheti cha usajili, huku vyuo 20 vikitoa mafunzo ambayo hayajathibitishwa chini ya idara isiyotambulika, wakati vyuo viwili vikiwa na vituo vya satellite/kampasi ambavyo navyo havijathibitishwa na chombo husika.
“Baraza linaufahamisha umma kwamba limechukua hatua mbalimbali kwa vyuo vya ufundi 48 kutokana na makosa mbalimbali, yaliyofanywa na vyuo hivyo ambapo limesitisha vyeti vilivyotolewa kwa vyuo 20 vilivyoshindwa kuzingatia masharti yaliyowekwa kwenye Cheti cha Usajili. “Uamuzi huu umefanywa kwa mujibu wa Kanuni ya 20 ya Usajili waVyuo vya Ufundi ya mwaka 2001,” alisisitiza.
Rutayuga alisema kwamba vyuo vilivyofutiwa usajili kutokana na kosa la kutoa mafunzo ambayo hayajathibitishwa chini ya idara isiyotambulika ni 26.
“Vyuo vya ufundi vinatakiwa kupata idhini ya baraza kabla ya kuanza kutoa mafunzo yoyote. Idhini hiyo inahusu uthibitisho wa mtaala kwa ajili ya mafunzo yaliyokusudiwa na utambuzi wa idara iliyopangwa kutoa mafunzo hayo,” alisema.
Juu ya vyuo vyenye vituo vya satellite/kampasi, Dk Rutayuga alisema baraza linahitaji mafunzo kutolewa katika vituo vilivyosajiliwa/ kampasi za vyuo vikuu baada ya kuthibitishwa kwamba vinastahili kutoa mafunzo.
“Hata hivyo, taasisi mbili zimebainika kutoa mafunzo katika vituo vya satellite/vyuo vikuu ambavyo havijasajiliwa na Baraza na hivyo kuadhibiwa. Vyuo hivyo navyo vimefutiwa leseni,” alisema Rutayuga.
Nacte ni bodi iliyoanzishwa kisheria chini ya Sheria ya Baraza la Taifa la Elimu ya Ufundi, kifungu cha 129, kusimamia na kuratibu utoaji wa elimu ya ufundi na mafunzo nchini Tanzania.
Chini ya sheria hiyo, ili kufikia na kudumisha hali ya mtoa mafunzo, vyuo vyote vinatakiwa viwe vimesajiliwa, viwe na vibali na kuwa mitaala iliyopitishwa na baraza. Vyuo haviruhusiwi kuanza kutoa huduma yoyote ya mafunzo bila idhini ya baraza.
Vyuo vilivyofutiwa usajili ni Institute of Management and Development Studies – Iringa, Mbengwenya College of Business and Information Technology –Mbinga na Green Hill Institute, Institute of Business and Social Studies, Loyal College of Africa, Mbeya Training College, New Focus College na Shukrani International College of Business and Administration vyote vya Mbeya.
Vingine ni Majority Teachers College – Mbeya, Rukwa College of Health Sciences – Sumbawanga, MAM Institute of Education – Mbeya, Belvedere Business and Technology College – Mwanza, Geita Medical Laboratory Sciences and Nursing Training College – Geita, Global Community College – Geita na Muleba Academy Institute – Muleba.
Aidha, vingine ni St. Bernard Health Training Institute – Katoro, Geita Victoria Institute of Tourism and Hotel Management – Mwanza, Gisan Institute of Health Sciences – Mwanza, Dar es Salaam Institute of Business Management, SAMFELIS College of Business Studies – Dar es Salaam na Ellys Institute of Technology – Mara.
Vyuo vingine vilivyofutiwa usajili ni Tanzania Institute of Chartered Secretaries and Administrators – Arusha, Emmanuel Community College – Kibaha, Modern Commercial Institute – Dar es Salaam na Marian College of Law – Dar es Salaam.
Alivitaja vyuo vinavyotoa mafunzo ambayo hayajathibitishwa kuwa ni MISO Teachers College – Mafinga, Tusaale Teachers College – Mafinga, The St. Joseph’s College Institute of Business and Management (SJCIBM) – Morogoro, The Golden Training Institute – Dar es Salaam na Nkrumah Mkoka Teachers College –Dodoma.
Vingine ni National Institute of Agriculture (Chuo cha Kilimo cha Taifa) – Arusha, Musoma Utalii Training College, Mwanza Polytechnic Institute, Mwanza Polytechnic Institute – Maswa na Ruter Institute of Financial Management – Mwanza.
Aidha, vyuo vingine ni Dar es Salaam Institute of Journalism and Mass Communication – Geita, Kahama, Simiyu, Mwanza na Bukoba, Singni International Training Institute – Bukoba, Richrise Teachers College – Geita, Twiga Training Institute – Musoma, Zoom Polytechnic Institute – Bukoba na St. Thomas Training College – Shinyanga.
Alivitaja vyuo vya ufundi vyenye satellite/kampasi kuwa MISO Teachers College – Mafinga na Rungemba Teachers College – Mafinga.

No comments:

 

ADVERTISE WITH US

AFRICAN FASHION

PLACE YOUR ADS HERE!