NAJARIBU kuwaza, huduma ya usambazaji umeme ingekuwa na kampuni nyingi kama ilivyo kwa huduma ya simu za mkononi, ingekuwaje? Bila shaka kungekuwa na ushindani mkubwa. Huduma ingekuwa ni ya haraka. Dhana ya ‘mteja ni mfalme’ ingetawala. Kampuni za umeme zingepishana mitaani kusaka wateja. Kila moja ingejaribu kuleta ubunifu kuhakikisha inapata wateja wengi.
Wasingeonekana watu wasio na umeme kama ambavyo hivi sasa Watanzania wengi wanamiliki simu za mkononi kutokana na urahisi wa huduma. Tungekuwa tunashuhudia promosheni za hapa na pale ambazo si tu zingerahisha maisha kwa wateja, bali pia zingeingiza kipato kwa kampuni husika.
Mteja angekuwa na uamuzi wa kuchagua kampuni anayoona inamhudumia vizuri. Ina maana mteja wa umeme ndiye angekuwa anatafutwa badala ya yeye kusaka huduma kwa kubembeleza na hata wakati mwingine kwa kulazimika kutoa ‘chochote’ kwa wafanyakazi wa Shirika la Umeme (Tanesco).
Mawazo haya yameniijia baada ya Tanesco kutangaza azma yake ya kupandisha bei ya umeme kwa asilimia 18.19 ifikapo Januari mwakani.
Nawashukuru na kuwapongeza wadau akiwemo Waziri wa Nishati na Madini, Profesa, Sospeter Muhongo kupitia mkutano wa wadau, ambao wamepinga maombi hayo wakisisitiza bei inapaswa kuwa rahisi.
Ningekuwapo kwenye mkutano huo ulioandaliwa na Ewura kujadili maombi hayo ya Tanesco, ningepigilia msumari na kueleza matamanio yangu ya kuiona Tanesco ikiwa na ‘mwenza’ kama ilivyo kwa kampuni za simu za mkononi.
Hata mimi ningepinga kitendo cha Tanesco kutaka kuongeza bei ya umeme huku sababu mojawapo ikiwa ni madeni. Naungana na Ewura ambayo imeitaka Tanesco kufikiria kukusanya deni la Sh bilioni 275.661 inazodai watu na taasisi mbalimbali nchini badala ya kufikiria kupandisha bei ya umeme.
Nishati ya umeme ni muhimu sana katika maisha ya binadamu inayopaswa kuongezwa kwenye mahitaji muhimu ya binadamu ambayo ni chakula, malazi na mavazi.
Ni jukumu la Tanesco kutafuta mikakati ya kuongeza mapato badala ya kukariri njia moja ya kupandisha bei . Mikakati iwe ya kuongeza idadi ya wateja badala ya kukamua wateja wachache waliopo.
Naamini kama kungekuwa na ‘wafanyabiashara’ wengi wa umeme, hata gharama zingeshuka kwa lengo la kuvuta wateja wengi. Fikiria, ni watu wangapi ambao wangependa kutumia umeme lakini wamekwazwa na gharama za kuuvuta? Je, watu hao ambao hawajavuta umeme, wangebuniwa mkakati maalumu kuwawezesha wawe na huduma, Tanesco haioni ingeliingizia shirika faida kubwa badala ya kukimbilia kuongeza deni kwa wachache wenye huduma?
Wapo watu wengi ambao wanaishi maeneo yenye umeme lakini hawana uwezo wa kulipia kwa mkupuo gharama za kuunganishwa. Inawezekana kabisa Tanesco ikawatafutia utaratibu wa kuwawezesha kupata huduma hata kwa mkopo huku wakiendelea kulipa taratibu.
Ikiachwa hao ambao hushindwa kuingiziwa umeme, lipo kundi lingine la watu ambao licha ya kuomba umeme, huzungushwa kwa sababu zisizo na maana kana kwamba wanaomba huduma ya bure. Haya yote yanatokana na Tanesco kuhodhi huduma kwani ndilo shirika pekee.
Hivyo baadhi ya wafanyakazi wasio waaminifu hutumia fursa hiyo kuwazungusha wateja wanaohitaji kufungiwa umeme. Unakuta mteja amelipia, lakini anaweza kukaa zaidi ya miezi mitatu bila kufungiwa umeme.
Wameshuhudiwa baadhi ya wafanyakazi wa Tanesco wakishawishi wapewe chochote ndipo wawaharakishie huduma. Hapo ndipo huwa najiuliza, ni aina gani hii ya biashara ambayo mfanyabiashara anabembelezwa badala ya yeye kuwabembeleza wateja watumie huduma/bidhaa zake?
Jibu ni kwamba, mfanyabiashara akishakuwa peke yake kwenye eneo, basi ndiye hugeuka mfalme badala ya mteja.
Si ajabu hata kwenye simu, ingebaki kampuni moja, ndivyo ambavyo tungesotea kupata huduma ya mawasiliano. Lakini angalia sasa namna kampuni za simu zimekuwa zikipishana mitaani na kwenye taasisi mbalimbali kuhakikisha kila mtu anatumia mtandao wake na kuwaongezea mapato!
Angalia zinavyowashawishi watu wajiunge na huduma kiasi cha kubuni hata mikakati ya kuwakopesha wateja muda wa maongezi na kuwakata kidogo kidogo kwa lengo la kuongeza kipato.
Hivi sasa wameibuka pia wafanyabiashara ambao wamegundua pengo lililopo katika kupata huduma ya umeme.
Wanaendesha biashara ya vifaa vya umeme unaotokana na mwanga wa jua. Biashara hii imevutia kampuni ambazo zimekuwa zikiwafungia bure wateja wao vifaa vya umeme wa jua kisha wateja hulipa malipo ya kila mwezi kwa kampuni. Je, Tanesco haioni kuwa inaweza kuja na ubunifu wa namna hii na kujikusanyia mapato haya?
Kwa kuwa Waziri Muhongo ameahidi kukaa na Tanesco kujadili masuala mbalimbali ikiwamo gharama ya umeme, wasiache kuja na mikakati ya kuhakikisha kila mtu anayehitaji umeme aupate, uwe wa uhakika na wenye bei rahisi.
Kadri wateja watakavyokuwa wengi, ndivyo na mapato yatakavyoongezeka badala ya kutegemea kuongeza gharama kwa wachache waliopo. twessige@yahoo.com
No comments:
Post a Comment