Friday, 25 November 2016

Magufuli atoa siku 7 wastaafu walipwe

RAIS John Magufuli ametoa wiki moja kwa Hazina kuwalipa wastaafu waliokuwa watumishi wa Chuo Kikuu Huria Tanzania (OUT) ambao hawajalipwa stahiki zao kipindi cha miaka saba sasa.


Ametoa agizo hilo wakati wa mahafali ya 31 yaliyofanyika makao makuu ya chuo hicho Bungo, wilayani Kibaha, baada ya Makamu Mkuu wa chuo Profesa Elifas Bisanda kuomba kulipwa wastaafu hao. Magufuli alisema kuwa wastaafu hao walipwe katika kipindi hicho na endapo Waziri hataweza kufanya hivyo basi apelekewe taarifa kama imeshindikana.
“Sijajua ni wastaafu wangapi, lakini peleka taarifa ya madai hayo kwa waziri ili wastaafu hao waweze kulipwa na isizidi wiki moja na kama haijafanyika hivyo nipe taarifa,” amesema Magufuli.
Makamu Mkuu wa chuo Profesa Bisanda amesema, uhakiki ulishafanywa mara mbili kuhusu wastaafu ambao walikuwa na mikataba na wanadai malipo.
Amesema, baadhi ya wastaafu wamekufa hivyo kusababisha watoto waende ofisini kudai malipo ya wazazi wao.
Profesa Bisanda amesema, wastaafu hao wengi wao ni wazee wenye umri kati ya miaka zaidi ya 80 na 100, hivyo kuna haja ya kuliangalia suala hilo kwa kina ili wapate stahiki zao ili waendelee na maisha yao.
“Rais tunaomba utusaidie wastaafu wetu hao waweze kulipwa mafao yao kwani kwa sasa ni miaka saba imepita hakuna kilichofanyika licha ya kuhakikiwa ili walipwe," amesema.
Alibainisha kuwa baadhi ya vyuo vikuu vingine walifanyiwa malipo lakini wanashangaa wastaafu wao kushindwa kulipwa huku wakiwa kila wakati wanakwenda kulalamika kwao.

No comments:

 

ADVERTISE WITH US

AFRICAN FASHION

PLACE YOUR ADS HERE!