KAWAIDA mara baada ya kuzaliwa watoto huanza kupitia hatua mbalimbali za ukuaji na wanapofikia miezi mitatu au mine waanza kukaa, kiasi wanavyokua huota meno, kutambaa, kusimama na kutamka baadhi ya maneno mepesi kama ‘dada’, ‘baba’ na hapo furaha ndani ya familia huzidi kuongezeka.
Daktari Bingwa wa Magonjwa ya Masikio, Pua na Koo (ENT) wa Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH), Dk. Edwin Liyombo, anaeleza kuwa wazazi wanalazimika kufuatia na kutambua kila hatua za ukuaji wa watoto wao ikiwamo kutamka maneno ili kuutambua na kukabiliana na ulemavu wa kutokusikia.
Anasema mtoto anapozaliwa anatakiwa awe na usikivu na anapofikisha umri wa miezi tisa tangu kuzaliwa, huanza kutamka baadhi ya maneno ambayo ni rahisi kuyasema.
Bingwa Liyombo, anazungumza na gazeti hili wakati MNH inatoa taarifa ya ongezeko kubwa la watoto wenye matatizo ya usikivu duni unaotokana na sababu mbalimbali.
Anasema chanzo cha mtoto kutokuna na usikivu kinahusisha mambo mengi, ambayo kwa kiasi kikubwa hayafahamiki na kwamba inatokea wengine huzaliwa na tatizo hilo.
Mtaalamu huyu anasema sababu mojawapo zinazofahamika ni matumizi ya mara kwa mara na pengine yasiyo sahihi ya dawa ya kutibu malaria ya kwinini na wakati mwingine mtoto kuwa na rangi ya manjano mara baada ya kuzaliwa.
Sababu nyingine ni magonjwa ya maambukizi ambayo mama anaweza kuugua wakati wa ujauzito na kusababisha mtoto kuzaliwa na maradhi hayo ya kuambukizwa.
Anaeleza kwamba mtoto akipata ajali inaweza kuwa ni sababu nyingine. Iwapo ataugua homa ya uti wa mgongo atakuwa na hatari ya kuwa na usikivu hafifu.
Kufuatia kuongezeka kwa tatizo hilo, anasema MNH itaanza kuwafanyia uchunguzi watoto wanaozaliwa ili kubaini iwapo wana matatizo hayo, kwa kutumia vifaa maalum.
Anataja tatizo la baadhi ya watoto kuzaliwa na upungufu kwenye usikivu kwani seli za kusikia hazipo vizuri kuruhusu usikivu.
Anasema watoto 45 wamekwishafanyiwa upasuaji wa sikio na kuwekewa kifaa cha kuongeza usikivu kiitwacho cochlea implant na kwamba ili kugundua watoto walio na tatizo hilo , Januari mwakani MNH itaanza kuwafanyia uchunguzi nchi nzima watoto wachanga tangu wanapozaliwa kwa kutumia vifaa hivyo.
KIFAA CHA USIKIVU
Bingwa Liyombo anasema ili mtoto aliye na tatizo hili aweze kurejea katika hali ya usikivu, anafanyika upasuaji kichwani pembeni ya sikio na kuwekewa kifaa ambacho kitaruhusu mawasiliano na kitakachowekwa nje sikioni.
Anasema watoto wanaofanyiwa upasuaji na kuwekewa kifaa hicho tangu wakiwa na umri wa mwaka mmoja hadi sita, wana uwezekano wa kuanza kuongea, kusikia lakini kwa kuanzishiwa mafunzo ya matamshi yanayotolewa na walimu maalum.
MWENYE TATIZO
Mtoto Apuhile Bohela (5), ni kati ya waliofanyiwa upasuaji na kuwekewa kifaa hicho ili kuimarisha usikivu.
Mama yake mtoto huyo, Hilda Bohela anasema aligundua mtoto wake kuwa ana tatizo hilo tangu akiwa na miaka miwili na miezi miwili.
Anakumbuka kuwa alikuwa hasikii akitamka maneno na alikuwa kimya, akifanya vitendo zaidi ndipo alipoamua kuanza matibabu MNH.
Anasema Desemba mwaka 2012 alikwenda nchini India kwa ajili ya matibabu na kisha kurudi tena Januari 2013 kwa ajili ya upasuaji na kuwekewa kifaa hicho.
‘Mara baada ya kuwekewa cochlea implant nilitegemea atazungumza mara moja kumbe inachukua muda, hadi aweze kutamka maneno kwa kumfundisha kama alivyo mtoto mdogo. Alikuwa na miaka miwili na nusu alipowekewa kifaa hicho, hivyo ilibidi arudi hatua zaidi nyuma kama mtoto wa miezi tisa, anayeanza kutamka, dada, baba,” anasema.
Anasem kwa kuwa kifaa hicho kinavaliwa nje ya sikio, changamoto ni uwezekano wa kuharibika haraka au kuibiwa na baadhi ya watu wanaodhani kuwa ni simu.
“Watu mtaani tunakoishi wanadhani kavaa simu kwa makusudi, kumbe kinamfanya asikie, hivyo inabidi kumlinda kila mara na kinauzwa kwa gharama kubwa,” anasema.
MAMILIONI YAOKOLEWA
Mkurugenzi Mtendaji wa MNH, Profesa Lawrence Museru, akizungumza jijini Dar es Salaam wakati wa uzinduzi huduma ya uwekaji wa vifaa vya kuimarisha usikivu kwa watoto 45, anasema tiba na vifaa hivyo ni gharama kubwa hasa kuwasafirisha wagonjwa nje ili kutibiwa.
Anaeleza kuwa kwa kipindi cha miaka mitatu serikali ilitumia zaidi ya Sh. milioni 80 kwa mtoto mmoja kwa ajili ya kutibiwa India kufanyiwa upasuaji na kuweka kifaa cha usikivu, ambacho ni maalumu kwa ajili ya kumuwezesha kusikia baada ya operesheni.
Profesa Museru anasema hivi sasa huduma ya kuweka programu ya kifaa hicho inafanyika nchini kwa vile sasa wapo wataalamu akieleza kuwa kuna wengine saba waliorejea nchini baada ya kuhitimu mafunzo nje.
"Lengo la serikali ni kupunguza gharama za matibabu nje ya nchi ili zitolewe hapa nchini ndiyo maana MNH imeokoa zaidi ya Sh. milioni 300 ambazo zingetumika kwa ajili matibabu haya kama wagonjwa hawa 45 wangekwenda nje," anasema.
WIZARA
Katibu Mkuu Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Dk. Ulisubisya Mpoki, aneleza kwamba idadi ya watoto wenye matatizo hayo wanaofikishwa katika hospitali hiyo, ni ndogo ikilinganishwa na ambao wako nyumbani au wazazi hawajawagundua.
Anawashauri wazazi kufuatilia na kutambua mafanikio na matatizo ya maendeleo ya ukuaji wa watoto kila hatua kwa ni sehemu ya afya bora
No comments:
Post a Comment