Thursday 28 July 2016

POLISI ALIYEMUUA MWANGOSI JELA MIAKA 15


JAJI wa Mahakama Kuu, Kanda ya Iringa, Dk Paulo Kihwelo amesema mahakama ni mahali pa sheria na wala si pa kusikiliza maoni ya watu wakati akimhukumu miaka 15 jela askari Polisi Pacificius Cleophace Simoni (27) aliyekutwa na hatia ya kumuua bila kukusudia aliyekuwa mwandishi wa Channel Ten Tv mkoani Iringa, Daudi Mwangosi.


Simoni alifikishwa kwa mara ya kwanza mahakamani hapo Septemba 12, 2012 akituhumiwa kumuua Mwangosi kwa kukusudia katika tukio lilitokea katika kijiji cha Nyololo, wilayani Mufindi mkoani Iringa. Akitoa hukumu hiyo iliyomchukua takribani dakika 22 kuisoma jana, Jaji Kihwelo alisema mtuhumiwa alikaa miaka minne mahabusu mara baada ya kutuhumiwa.
“Haki itatendeka iwapo mtuhumiwa atakwenda jela miaka mingine 15, hiyo ni kwa kuzingatia ukubwa wa kosa ambalo amekutwa nalo mahakamani.”
Alisema upande wa utetezi uliiomba mahakama hiyo imuachie huru mtuhumiwa na upande wa Jamhuri uliomba afungwe maisha lakini yeye (Jaji) hakuafikiana na ombi la utetezi kwa sababu msingi wa adhabu unatakiwa ufanane na kosa.
Akizungumza baada ya hukumu hiyo, mke wa marehemu, Itika Mwangosi alisema pamoja na kifo kilichomkuta mumewe wakati akitekeleza wajibu wake, aliwatia moyo wanahabari akiwataka wasiogope vikwazo vya dola, wasonge mbele katika kazi zao za kuhabarisha umma kwa kuwa bila wao jamii haiwezi kujua kinachoendelea.
Rais wa Umoja wa Klabu za Waandishi wa Habari Tanzania (UTPC), Deo Nsokolo alisema wanaishukuru mahakama kwa maamuzi hayo.

No comments:

 

ADVERTISE WITH US

AFRICAN FASHION

PLACE YOUR ADS HERE!