Friday 1 July 2016

Aliyemtusi Magufuli matatani tena


MKAZI wa Arusha, Isaac Emilly (40), aliyehukumiwa kulipa faini ya Sh. milioni saba baada ya Mahakama ya Hakimu Mkazi Arusha kumkuta na hatia ya kumtukana Rais John Magufuli, huenda akajikuta tena matatani.




Waziri wa Katiba na Sheria, Dk. Harrison Mwakyembe, alisema jana kuwa hatua hiyo inatokana na taarifa za kuchangiwa fedha ili kulipa faini na kwamba suala lake limepelekwa kwa Mkurugenzi wa Mashtaka nchini (DPP).
Aidha, Waziri huyo alisema hatua hiyo imechukuliwa baada ya kuona suala hilo la mhukumiwa huyo kuchangisha fedha za kulipa faini linaweza kuharibu maana ya hukumu.
Kauli hiyo ya Dk. Mwakyembe bungeni mjini hapa ilitokana na mwongozo ulioombwa na Mbunge wa Chemba (CCM), Juma Nkamia, na kurejewa tena na Mbunge wa Mtera (CCM), Livingstone Lusinde (CCM), kuhusu hukumu aliyopewa Emilly.
Katika maelezo yao, wabunge hao wote walidai adhabu aliyopewa mshtakiwa huyo hailingani na kosa lililomtia hatiani.
Akitoa kauli ya mawaziri bungeni, Dk. Mwakyembe alisema mshtakiwa analifanya suala hilo la siasa na adhabu aliyopewa aliiona kama burudani ya kisiasa kwenye mitandao ya kijamii.

Waziri huyo alisema waendesha mashitaka nchini wanapaswa kuwa macho na waweke mbele weledi na maslahi mapana ya taifa na wasiyumbishwe na mihemko ya kisiasa katika jamii.
Alisema kwa kuwa awamu ya kwanza ya malipo ya faini inaishia Julai 8, mwaka huu, na awamu ya pili ni Agosti 8, mwaka huu, amewasilisha kwa DPP suala hilo kwa hatua stahiki ili kulinda dhana na dhamira ya adhabu katika mfumo wa haki jinai.
Alisema matarajio ni mhukumiwa kujutia kosa lake na wengine wajifunze toka kwake, lakini akaeleza kuwa hayawezi kufikiwa kwa mwenendo huo wa kuingiza siasa kwenye utekelezaji wa hukumu.
Machi 7, mwaka huu, Emily alituma ujumbe wa maneno katika akaunti yake ya mtandao wa kijamii wa Facebook akisema: “Hizi ni siasa za maigizo, halafu mnamlinganisha huyu bwege na Nyerere wapi bwana.”

NIPASHE.

No comments:

 

ADVERTISE WITH US

AFRICAN FASHION

PLACE YOUR ADS HERE!