Tuesday 28 June 2016

WATUHUMIWA WAWILI WA MAUAJI WAUAWA DAR




JESHI la Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam limewaua majambazi sugu wawili katika matukio mawili tofauti, ambao wanatuhumiwa kuwa vinara wa matukio ya mauaji yaliyotokea msikitini Mwanza na jijini Tanga.


Akizungumza na waandishi wa habari jana jijini Dar es Salaam, Kamishna wa Polisi Kanda Maalumu, Simon Sirro alisema katika tukio la kwanza Polisi wakati wa ufuatiliaji wa mtuhumiwa wa mauaji ya msikitini jijini Mwanza, Salum Said alikimbilia Dar es Salaam baada ya kufanya tukio hilo.
Kamanda Sirro alisema jeshi hilo, lilimkamata mtuhumiwa huyo baada ya kupata taarifa kutoka kwa wasamaria wema kuwa mtuhumiwa huyo amekimbilia Dar es Salaam baada ya kufanya mauaji.
Aliongeza kuwa baada ya taarifa hizo, Polisi walifika katika nyumba aliyokuwa amepanga eneo la Buguruni katika Manispaa ya Ilala na kuzingira nyumba yake, lakini mtuhumiwa huyo alipatiwa taarifa kuwa kuna askari wamezingira nyumba ndipo alipoamua kutoka na kukimbia huku akirusha risasi.
Sirro alisema mtuhumiwa huyo alipoona amezidiwa, aliamua kurusha bomu alilokuwa nalo na kupasuka bila kuleta madhara, ndipo polisi walipofanikiwa kumpiga risasi ya mguu wa kulia na kumkamata.
“Nilipoambiwa ameumizwa nikawataka polisi wampeleke hospitali, lakini bahati mbaya alifariki lakini naamini kikundi chake bado nipo na ninasikia wapo hapa, niwaambie tu tutawatafuta na tutawakamata lakini kabla ya yote hayo naomba wajisalimishe wenyewe,” alisema Kamanda Sirro.
Alisema kabla ya kuuawa, mtuhumiwa huyo aliwahi kufanya matukio mbalimbali ya wizi ikiwemo wizi katika maduka ya huduma ya kutuma na kupokea fedha kwa njia ya simu za mkononi. Katika tukio jingine, polisi wamemuua mtuhumiwa wa mauaji ya watu wanane yaliyotokea mkoani Tanga.
Kamanda Sirro alisema mtuhumiwa huyo, pia aliwahi kusambaza video kuwa Rais hana jeshi. Alisema mtuhumiwa huyo aliyefahamika kwa jina la Mohamed Abdala, alikutwa akiwa na bastola, risasi 19 na bomu la mkono.
Alisema mtuhumiwa huyo alikimbilia Dar es Salaam baada ya kufanya mauaji huko Tanga.
Alisema polisi baada ya kupata taarifa, walikwenda kuzingira nyumba yake, lakini tayari mtuhumiwa huyo alikuwa amepata taarifa za polisi kuzingira nyumba yake, hivyo alitoka kwa kutumia dirisha ndipo polisi walipoanza kumshambulia na alipoona anazidiwa alirusha bomu la mkono ambalo halikuweza kulipuka.
Alisema polisi walimpiga risasi na kumjeruhi sehemu mbalimbali, lakini wakati wakimpeleka hospitali alifariki. Sirro alisema mtuhumiwa huyo kabla ya kuuawa, alifanya matukio mbalimbali ikiwemo uporaji katika duka la mikate jijini Tanga ambako watu watatu waliuawa na kujeruhi wengine wawili.
Hivi karibuni, kulikuwapo na matukio ya mauaji katika mikoa ya Tanga na Mwanza ambako jijini Tanga watu watatu waliuawa katika duka la mikate na kisha kutokea mauaji ya kuchinjwa kwa watu wanane katika Kitongoji cha Kibatini Kata ya Mzizima jijini humo.
Aidha, mkoani Mwanza, katika watu watatu akiwamo Imamu waliuawa katika Msikiti wa Rahman katika eneo la Ibanda Relini katika Mtaa wa Utemini Kata ya Mkolani wilayani Nyamagana.





No comments:

 

ADVERTISE WITH US

AFRICAN FASHION

PLACE YOUR ADS HERE!