Saturday 18 June 2016

Wabunge wengine Ukawa watimuliwa

WAKATI wabunge wa Ukawa wakisusa kuingia bungeni, huku wakivumilia kukatwa posho, Naibu Spika, Dk Tulia Ackson, ambaye ndiye anayedaiwa kuwa sababu ya kususa kwao, amewasimamisha kazi wabunge wawili wa viti maalumu Chadema kwa kosa la kusema uongo bungeni.


Wabunge hao ni Susan Lyimo aliyesimamishwa vikao vitano na Anatropia Theonest, aliyesimamishwa vikao vitatu kuanzia jana, ambao walifikishwa katika Kamati ya Haki, Maadili na Madaraka ya Bunge kujitetea kabla ya kukutwa na hatia.
Dk Tulia alitangaza hatua hiyo bungeni jana, baada ya Kamati hiyo kuwasilisha taarifa ya kuwakuta na hatia ambapo pia ilieleza kuwa Suzan alishindwa kuthibitisha ukweli wa kauli yake, huku Anatropia akikiri kosa la kusema uongo bungeni.
Adhabu hizo kwa mujibu wa taarifa ya Kamati ya Haki, Maadili na Madaraka ya Bunge, zimeelezwa kuzingatia masharti ya Kanuni ya 75, ambapo wabunge hao wamezuiwa kuingia sehemu yoyote ya ukumbi wa Bunge na maeneo ya Bunge, ambapo pia watalipwa nusu mshahara na nusu posho zinazoambatana na mshahara wake.
Suzan Akiwasilisha taarifa iliyowatia hatiani wabunge hao, Makamu Mwenyekiti wa Kamati ya Haki, Maadili na Madaraka ya Bunge, Mbunge wa Tabora Kaskazini, Almas Maige (CCM), alieleza kauli ya Susan iliyomtia matatani.
Mei 11 mwaka huu Suzan alipokuwa akichangia mjadala wa Hotuba ya Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, alidai kuwa Serikali imenunua magari 777 ya `washawasha’, ambapo alidai kuwa ni magari 50 tu yaliyotumika kwenye uchaguzi.
Katika mahesabu yake yaliyonukuliwa na taarifa rasmi za Bunge, Susan alisema katika ununuzi huo Serikali ilitumia zaidi ya Sh bilioni 420, ambapo kama Serikali ingetaka kutumia fedha hizo kununua magari ya wagonjwa kila kata nchini, ambazo alisema ziko kata 3,990 ingepata moja huku akishangiliwa na wabunge wenzake wa Ukawa.
Baada ya kusema hivyo, Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani, Yusuph Hamad Masauni siku iliyofuata aliomba mwongozo na kusema taarifa alizonazo ni kwamba magari ya ‘washawasha’ yaliyonunuliwa, yalikuwa 32 na si 777 yaliyotajwa na Susan.
Taarifa hiyo imeonesha kuwa, Susan alipopewa nafasi ya kufuta maneno hayo na Spika au atoe uthibitisho, mbunge huyo wa Viti Maalumu alionekana kuwa tayari kuthibitisha na kwa kuwa uthibitisho wake ulionekana ungeweza kuchukua muda mrefu, alitakiwa aupeleke katika kamati hiyo.
Ushahidi wa MwanaHalisi Alipoitwa kwenye kamati hiyo, Susan alipeleka ushahidi aliodai ni wa Mwananchi Online, taarifa rasmi za Bunge kuhusu majibu ya Masauni alipojibu swali la nyongeza kuhusu ununuzi wa magari ya ‘washawasha’, taarifa za mtandao wa Alibaba ambako alidai kuulizia bei ya magari ya wagonjwa na kielelezo kutoka Habarikablog.blogspot.com.
Hata hivyo kamati hiyo ilipofanya uchambuzi wa vielelezo hivyo, Maige alisema haikukuta kielelezo cha Mwananchi Online, bali cha Mwanahalisi Online na pia kielelezo cha Habarikablog. blogspot.com hakikuainishwa.
Katika taarifa rasmi za Bunge kuhusu majibu ya Masauni, ilibainika yalieleza kuwa Serikali imenunua magari 777 ya Polisi na kati ya hayo, magari 32 tu ndiyo ya ‘washawasha’. Kwa kuwa hakuna kielelezo hata kimoja kilichothibitisha kuwa Serikali imenunua magari hayo 777 ya ‘washawasha’, kamati hiyo ikamtia hatiani kwa kusema uongo bungeni.
Anatropia
Anatropia yeye alishtakiwa kwa Spika na Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, William Lukuvi, kwa barua kuwa Februari 3 mwaka huu, mbunge huyo akichangia hoja kuhusu Kamati ya Mipango, alisema kuwa Waziri huyo mwaka 2011 alipokuwa Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, alipora viwanja.
Mbunge huyo wa Chadema, alidai bungeni kuwa Lukuvi akiwa Mkuu wa Mkoa mwaka 2011, alihusika na uporaji wa maeneo yaliyopo Tegeta, ambayo walipewa wananchi waliokuwa wakiishi mabondeni, wakiwemo wa Jimbo la Segerea na wananchi wa Ilala, ambao sasa wanataka maeneo yao huku wakidai kuwa Lukuvi alihusika kuyapora.
Lukuvi katika barua hiyo, aliomba tu Anatropia afute kauli yake airekebishe, kwa kuwa mwaka 2011, alikuwa Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Sera, Uratibu na Bunge na si Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam na wala hakuhusika na tuhuma hizo.
Hata alipoitwa katika Kamati hiyo, Lukuvi alisema tuhuma zilizotolewa na Anatropia, si tu zilikuwa za uongo, bali pia zimemfedhehesha kwa kumhusisha na uporaji wa viwanja vya watu wanyonge.
Akiri ni muongo
Alipoitwa Anatropia mbele ya Kamati, Maige alisema mbunge huyo wa Chadema; “alikiri mbele ya Kamati kuwa alisema uongo bungeni kwa kuwa ni kweli Lukuvi hakuwa Mkuu wa Mkoa mwaka 2011, hivyo asingeweza kuhusika na uporaji wa viwanja vya waathirika wa mafuriko.”
Anatropia ameelezwa katika taarifa hiyo kuwa, alisema kwamba iwapo angeambiwa jambo hilo akiwa bungeni, kuwa kauli aliyokuwa ameitoa siku hiyo ilikuwa ya uongo angeifuta.
“Alionesha kusikitika kuona suala hili limefika Kamati ya Maadili, ambalo lingeweza kumalizika ndani ya ukumbi wa Bunge, ikiwa angepata fursa,” alisema Maige na kuongeza kuwa Kamati ilimtia hatiani mbunge huyo.
Ufafanuzi wa Dk Tulia Akifafanua adhabu hizo, Dk Tulia alisema kwa kuwa wabunge hao walionesha kuwa wangeweza kuthibitisha, ndio maana walipelekwa katika Kamati hiyo kwenda kutoa ushahidi na kwa kuwa wameshindwa, Spika anaweza kutoa adhabu ya kumsimamisha mbunge vikao visivyozidi vitano, hivyo mapendekezo ya kamati hiyo, ameyaafiki.
Kutokana na adhabu hiyo, sasa Suzan na Anatropia, wanafikisha idadi ya wabunge wanane waliosimamishwa bungeni kwa kukiuka kanuni.
Wengine ni Mbunge wa Kigoma Mjini, Zitto Kabwe (ACT), Mbunge wa Arusha Mjini, Godbless Lema, Mbunge wa Tarime Vijijini, John Heche, Mbunge wa Kawe, Halima Mdee, Mbunge wa Babati Mjini, Pauline Gekul na Mbunge wa Bunda Mjini, Esther Bulaya, wote wa Chadema.

No comments:

 

ADVERTISE WITH US

AFRICAN FASHION

PLACE YOUR ADS HERE!