BAADA ya wakazi wa Jiji la Dar es Salaam na mikoa ya jirani kuteseka kwa muda mrefu kubeba vyakula kuwapelekea wagonjwa, Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH), imeanzisha utaratibu mpya wa kutoa huduma hiyo bure kwa wagonjwa.



Hospitali ya Taifa Muhimbili hulaza zaidi ya wagonjwa 1,300 wa jijini Dar es Salaam na wale wanaotoka mikoani.
Akitangaza utaratibu huo mpya ambao utaanza kutumika Julai mosi, mwaka huu, Mkurugenzi wa Huduma za Uuguzi wa Muhimbili, Agnes Mtawa, alisema huduma hiyo itatolewa nyakati za asubuhi, mchana na jioni.
“Hospitali inakusudia kutoa chakula chenye ubora na viwango vinavyotakiwa kwa wagonjwa ikiwamo kutoa chakula maalumu (special diet) kwa wagonjwa wenye mahitaji hayo na wale ambao wanakula kwa kutumia mrija,” alisema.Mtawa alisema walitangaza zabuni ya kazi hiyo na ikapatikana Kampuni ya Usambara Cartering Services.
Alisema atapika chakula na kukisambaza nje ya wodi zote ambako kuna wagonjwa wamelazwa na jukumu la kumpa mgonjwa kifungua kinywa, chakula cha mchana na jioni linabaki kwa wauguzi.
UTARATIBU WA KUWAONA WAGONJWA
“Kutokana na uamuzi huu, utaratibu wa ndugu kuleta chakula kwa wagonjwa waliolazwa wakati wa mchana umefutwa na hivyo mchana hatutakuwa na nafasi ya ndugu kuja kutembelea wagonjwa,” alisema.

Alisema muda wa kutembelea wagonjwa utakuwa asubuhi saa 12.00 hadi 1.00 na saa 10.00 jioni hadi saa 12.00 jioni.
Alisema wakati huo watu wataruhusiwa kuingia ndani kuwaona ndugu zao waliolazwa na kuruhusiwa kwenda na chakula chochote cha kumuongezea mgonjwa wao .

GHARAMA ZA CHAKULA
Akizungumzia gharama za chakula atakachokula mgonjwa siku zote atakazolazwa katika hospitali hiyo, Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano, Aminiel Aligaesha, alisema mgonjwa atachangia Sh. 50,000.

Alisema Sh. 10,000 kwa ajili ya gharama ya kumuona daktari, Sh. 10,000 ya kulazwa na Sh. 30,000 italipia chakula kwa kipindi chote mgonjwa atakapokuwa hospitalini.
“Kwa sasa hospitali inatoa chakula kwa wagonjwa 650 ambao wanaopata rufaa kutoka hospitali za nje ya mkoa wa Dar es Salaam na hugharimu wastani wa Sh. bilioni 1.8 kwa mwaka, sawa na Sh. milioni 150 kwa mwezi kwa vyakula pamoja na gharama nyingine kama vile za nishati,” alisema Aligaesha.
Alisema wagonjwa kati ya 600 na 700 waliokuwa na rufaa kutoka hospitali za Dar es Salaam walikuwa hawapati chakula na kulazimika kupelekewa chakula na ndugu.
“Uongozi wa hospitali unaamini kwamba mabadiliko haya hayataongezea gharama kwa wagonjwa, bali yatampunguzia pamoja na adha walizokuwa wakizipata watu wanaowaletea vyakula,” alisema.
RATIBA YA MLO KWA SIKU
Aligaesha alisema, mgonjwa atapatiwa uji wa unga wa soya au wa unga wa dona na yai la kuchemsha moja kila siku asubuhi, mchana atakula ugali, mboga za majani na matunda na jioni atakula wali, nyama na matunda.Alisema mboga watakazopikiwa ni mboga za majani mchanganyiko, maharage, nyama na kabichi.

Alisema kwa wiki watakula ugali mara tano, wali mara tatu, pilau mara mbili na viazi mara mbili.Alisema wauguzi ndio watakuwa na jukumu la kuwalisha wagonjwa ambao hawawezi kula wenyewe.
“Kama kuna mtu atataka kumuongezea mgonjwa wake chakula anachokitaka atakileta wakati wa usiku. Kazi ya kuwapa chakula wagonjwa ni ya wauguzi hivyo watafanya hivyo na pia kuna dawati la malalamiko kwa ajili ya wale ambao watahudumiwa vibaya,” alisema.
SABABU ZA KUWEKA HUDUMA
Awali akizungumzia sababu za hospitali hiyo kuweka utaratibu huo, Aligaesha alisema, lengo ni kujikita katika majukumu yake ya msingi ya ushauri, uchunguzi na tiba.

Alisema lengo lingine ni kuwaondolea adha ndugu wa wagonjwa ambao wamekuwa wakiingia gharama kubwa hususani usafiri wa kwenda na kurudi hospitalini hapo mara tatu kwa siku.
“Tumefanya utafiti, tumebaini kuwa, ndugu jamaa na marafiki hutumia Sh. 6,000 hadi 10,000 kwa siku kama usafiri wa kuja hospitalini hapa kulingana na mahali anapoishi, bila kugharamia fedha za matayarisho ya chakula na kuwaondolea usumbufu wa kuacha shughuli zao,” alisema.
Aligaesha, alisema pia mpango huo, utapunguza msongamano wa watu ndani ya hospitali ambao umekuwa ukisababisha kulinganisha na huduma wanazotoa madaktari na kusababisha wagonjwa kukosa huduma stahiki.
Alisema pia kuwepo kwa mzabuni huyo, kutapunguza gharama za huduma za nishati, matengenezo ya jiko na pia wahudumu kufanya shughuli nyingine za kusaidia wagonjwa.