Monday 20 June 2016

GONJWA LA AJABU LILILOIBUKA KONDOA CHEMBA SI KIMETA



SERIKALI imefafanua kuwa ugonjwa wa ajabu ulioibuka katika Wilaya za Chemba na Kondoa na kusababisha vifo vya watu saba hadi sasa, hauna uhusiano wowote na ugonjwa wa kimeta.



Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Ummy Mwalimu, alisema tafiti za awali zilizofanywa kwa kushirikiana na Ofisi ya Mganga Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, zimebaini kuwa ugonjwa huo hauna uhusiano wowote na kimeta.

Waziri Mwalimu amesema ilibainika kuwa ugonjwa huo ulianza kujitokeza baada ya wananchi kula nyama ya ng’ombe ayechinjwa kutokana na kuvunjika mguu katika kijiji cha Mwai Kisabe kata ya Kimaha Wilaya ya Chemba mkoani Dodoma.
Alisema baada ya kula nyama hiyo, watu tisa wa familia moja waliugua ugonjwa huo na watatu kati yao, walifariki dunia.
Hata hivyo, alisema wanakijiji wengine waliokula nyama hiyo, hawakuugua.

“Mpaka kufikia Juni 18, mwaka huu, wagonjwa wameendelea kuongezeka siku hadi siku na kufikia wagonjwa 21 ambao kati yao, saba wamefariki dunia na watoto wawili hali zao ni mbaya,” alisema Waziri Mwalimu.
Aliongeza kuwa wizara yake imeunda kamati maalum kwa kushirikiana na Ofisi ya Mganga Mkuu wa Mkoa wa Dodoma kwa ajili ya kutibu dalili za ugonjwa huo ili kuzuia maambukizi mapya.
Alisema timu nyingine ya wataalam kutoka ngazi ya taifa inayoundwa na daktari bingwa kutoka Hospitali ya Taifa ya Muhimbili, wataalam kutoka Ofisi ya Mkemia Mkuu wa Serikali, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi) na Mamlaka ya Chakula na Dawa Tanzania (TFDA) ambayo ilitarajiwa kuwasili jana kuongeza nguvu za uchunguzi zaidi.
Aidha, alisema timu hiyo itasaidiana na wataalam wa sekta ya kilimo na mifugo kwa kuwa inadhaniwa ugonjwa huo huenda unahusishwa na vyakula vyenye sumu.
“Vipimo vya awali vilivyofanywa Maabara Kuu ya Taifa vinaonyesha kutokuwapo kwa homa ya manjano. Hata hivyo, Maabara Kuu inaendelea kufanya vipimo vingine ikiwamo homa ya Bonde la Ufa,” alisema Mwalimu.
Aliongeza kuwa wizara yake inaendelea kushirikiana na wadau mbalimbali wa afya likiwamo Shirika la Afya Duniani (WHO) na Kituo cha Kudhibiti magonjwa katika kuhakikisha ugonjwa huo unatambuliwa kwa haraka na hivyo kupunguza wingu la wasiwasi lililowajaa wakazi wa Dodoma juu ya ugonjwa huo.
Naye Mganga Mkuu wa Hospitali ya Mkoa wa Dodoma, Dk. James Kiologwe, alisema hali za wagonjwa waliolazwa hapo zinaendelea vizuri isipokuwa watoto wawili ambao si nzuri.
Dk. Kiologwe alisema Hospitali ya Mkoa kwa kushirikiana na Hospitali ya Wilaya ya Kondoa, inaendelea na tiba yakinifu ili kuhakikisha ugonjwa huo ambao mpaka sasa chanzo chake hakijafahamika kitaalam, hauendelei kuenea ndani ya Mkoa wa Dodoma na mikoa ya jirani.
MWANANCHI.

No comments:

 

ADVERTISE WITH US

AFRICAN FASHION

PLACE YOUR ADS HERE!