Saturday 18 June 2016

Biashara kwenye mataa Dar marufuku!

WAZIRI wa Nchi katika Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi), George Simbachawene amemuagiza Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda kushirikiana na viongozi wa Mkoa kuhakikisha kuanzia leo hakuna mfanyabiashara atakayefanya biashara katika maeneo ya ‘mataa’.


Alimtaka pia kuhakikisha anawaondoa ombaomba wote waliopo katika makutano hayo na katikati ya jiji. Simbachawene alitoa agizo hilo jana alipofanya ziara katika Mradi wa Mabasi yaendayo Haraka (UDART).
Alisema lengo la kuwaondoa wafanyabiashara na ombaomba hao ni kutaka kulifanya Jiji la Dar es Salaam kuwa na mwonekano mzuri.
“Kuanzia kesho (leo) sitaki kumuona mfanyabiashara katika maeneo hayo ya makutano na pembezoni mwa barabara watafutieni utaratibu ambao utawafanya wakae maeneo ambayo ni tofauti,” alisema na kuongeza kuwa, anataka katika maeneo hayo kuwepo na askari saa 24 ambao watahakikisha hakuna mfanyabiashara atakayefanya biashara baada ya kuondolewa.
“Acheni kukamata mama ntilie nataka askari hao watumike kuwakamata wafanyabiashara hao.., nataka askari hao wakae hapo saa 24,” alisema Simbachawene na kuongeza kuwa uchafuzi wa mazingira katika maeneo ya jiji kunachangiwa na uwepo wa biashara zinazofanywa katika mazingira ambayo sio rasmi.
Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda alimuahidi Waziri huyo kuwa watatekeleza maagizo yote na kuahidi kuanza operesheni hiyo leo kama alivyomuelekeza. Simbachawene pia amewataka wamiliki wa vyombo vya usafiri kufuata sheria na kuacha kutumia barabara za mwendo kasi hususani pikipiki na maguta.
Alisema ili pia kukabiliana na changamoto ya foleni, serikali imejipanga kusimamia awamu ya pili ya utekelezaji wa barabara za mabasi yaendayo haraka inayotarajiwa kuanza mwakani. Simbachawene alisema tayari wameshafanya tathmini na utatumia miaka miwili hadi kukamilika kwake pia wapo katika mchakato wa kumtafuta mkandarasi kwa ajili ya ujenzi.
“Hii awamu ya pili itaanzia katika barabara ya Sokoine kuelekea barabara ya Kilwa hadi Mbagala na kutakuwa na barabara za juu katika makutano ya barabara ya Kawawa na Nyerere,” aliongeza.

No comments:

 

ADVERTISE WITH US

AFRICAN FASHION

PLACE YOUR ADS HERE!