Watu 11 wanahofiwa kufa maji usiku wa kuamkia jana katika Ziwa Nyasa wakati wakisafiri kwa boti kutoka Bandari ya Mbambay mkoani Ruvuma kwenda Malawi kwa shughuli za kibiashara.
Kutokana na taarifa hizo, ndugu wa waathirika hao jana waliweka kambi katika bandari hiyo wakisubiri taarifa zozote kuhusu miili au ndugu zao. Watu hao wanaohofiwa kufa maji walikuwa wanasafiri kwa boti ya MM Mapeza kwenda kuuza na kununua bidhaa mbalimbali ikiwamo sukari na mitambo ya umeme jua.
Wakizungumza na Mwananchi jana ndugu wa waathirika hao walisema wameshtushwa na taarifa za kuzama boti hiyo na kwamba wanaamini kuwa ndugu zao wameshafariki dunia kutokana na hali ya ziwa kuchafuka.
Huku akibubujikwa machozi, mke wa mfanyabiashara John Komba, Veronica Chiwinga alisema mumewe alisafiri juzi saa saba usiku na yeye alimsindikiza hadi kwenye boti hiyo na wakaagana na muda mfupi baadaye alipigiwa simu na mumewe huyo akimuuliza kama alifika nyumbani salama na tangu hapo hajapokea taarifa yoyote. “Nina uchungu mkubwa, sina taarifa zozote, nimeumia mume wangu kafa tunafichwa tu na hadi sasa hatujapata taarifa za kuonekana kwake wala simu. Ninaamini amefariki tu... kwani hii ni mara yake ya pili kupata ajali; mara ya kwanza alinusurika kufa wakati alipofuata sola Malawi lakini hakuacha kutokana na kuwa bei ya sola Malawi ipo chini kuliko Dar es Salaam,” alisema Veronica.
Mwanamama huyo ameiomba Serikali kupeleka usafiri wa uhakika ili kunusuru ajali za mara kwa mara zinazotokea Ziwa Nyasa. Vilevile, ameiomba Serikali kumsaidia kusomesha watoto watatu alioachiwa na marehemu mumewe akisema hana uwezo.
Garous Azimbiwe, baba mzazi wa Samwel Azimbiwe (35) ambaye alikuwa mbeba mzigo katika boti hiyo, ameelezea kuumizwa na taarifa za kuzama mwanaye pamoja na mpwawe aliyemtaja kwa jina la Ramso Mfaume (28). Mzee huyo ameiomba Serikali kupeleka kikosi cha wanamaji kutoka Jeshi la Wananchi au Jeshi la Polisi ili kusaidia kutafuta ndugu zao kwani bado anaamini kuwa watapatikana wakiwa hai.
Alisema alipata taarifa za kuzama boti hiyo kutoka kwa binamu yake kwamba ilikosa uelekeo. Baada ya taarifa hiyo walishirikiana na wenzao kuchangisha fedha kwa ajili ya kununua mafuta ili wawaokoe ndugu zao kwa kutumia boti nyingine lakini hadi jana saa 11 jioni hakukuwa na taarifa zozote.
MWANANCHI.
MWANANCHI.
No comments:
Post a Comment