Dar es Salaam. Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete (JKCI) iliyopo katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili (MNH) wiki hii imeanza kufanya upasuaji wa Moyo kwa wagonjwa 80 wengi wao wakiwa watoto, kwa kushirikiana na wataalamu kutoka Australia, Saudi Arabia na Uingereza.
Aidha,inatarajia kujifunza kutoka kwa kambi mbalimbali za wataalamu wa moyo kutoka nje ya nchi jinsi ya kutumia Teknolojia ya upasuaji wa Moyo bila kupasua kifua.
Mkuu wa Taasisi ya JKCI, Prof Mohammed Janabi, amesema hayo leo wakati wa ziara ya Naibu Balozi wa Uingereza nchini, Matt Sutherland alipotembelea kambi ya wataalamu wa moyo inayoendelea katika taasisi hiyo na kueleza mwaka 2015 walifanya upasuaji kwa wagonjwa 207.
Amesema katika kambi hiyo iliyoanza April 30 hadi Mei 7 mwaka huu, itafanya upasuaji kwa wagonjwa 80 kwa kutumia wataalamu kutoka nchini Saudia Arabia na Uingereza kwa ufadhili wa taasisi ya Al-Mundada Aid kati yao 20 wakitokea Zanzibar.
Amesema asilimia 80 ya wagonjwa watakaopasuliwa ni watoto na mpaka leo tayari wamefanyia upasuaji 40 kutoka sehemu mbalimbali nchini kwani katika Mwezi Januari kulikuwa na wagonjwa 500 waliohitaji upasuaji na kufikia mwezi Machi walifanyia wagonjwa 86.
Amesema kwa sasa taasisi hiyo kila siku inafanyia upasuaji wagonjwa wawili hadi watatu hata kama hakuna kambi za wataalamu kutoka nje huku wagonjwa wanne au sita wakifanyiwa vipimo mbalimbali hospitalini hapo kwa ajili ya maandalizi ya upasuaji.
“Mwaka huu tunatarajia kuwa na kambi nane za upasuaji kwa wataalamu kutoka nje ya nchi zitakazosaidia kupunguza gharama ya kuhudumia wagonjwa hao ikiwa ni pamoja na sisi wataalamu katika kada mbalimbali kuongeza ujuzi kwa teknolojia mpya,” amesema Profesa Janabi.
Akizungumza katika ziara yake, Naibu balozi wa Uingereza hapa nchini, Matt Sutherland ameisifu taasisi ya JKCI, kwa kuratibu kambi ya upasuaji wa moyo kwa kushirikiana na madaktari kutoka nje kwa mafanikio makubwa.
“Nimefurahishwa sana na uamuzi wa JKCI wa kuratibu zoezi hili kwa ushirikiano na wataalamu wa magonjwa ya moyo kutoka nje ya nchi, najua taasisi ya hiari kutoka Uingereza imekusanya fedha na kwa kushirikiana na madaktari wengine, wamewezesha zoezi hili kufanyika kwa mafanikio,” amesema Balozi Sutherland.
Taasisi ya Muntada Aid, ni taasisi ya Kiislamu yenye makazi yake nchini Uingereza, ambayo ndiyo iliyowezesha kuwaleta madaktari na vifaa na hatimaye kwa kushirikiana na madaktari na wataalamu wengine kutoka JKCI wameweza kufanya upasuaji wa watoto 40 hadi sasa.
No comments:
Post a Comment