SERIKALI ya Kijiji cha Sanya Hoye, Wilaya ya Siha, mkoani Kilimanjaro imetangaza adhabu ya kuchapwa viboko 15 na kulipa faini ya Sh. 50,000 kwa mkazi yeyote atayekutwa baa nyakati za usiku, akiwa ameambatana na mtoto mwenye umri chini ya miaka 18.




Uamuzi huo umefikiwa juzi na wakazi wa kijiji hicho, katika mkutano uliofanyika Wilayani hapa.
Mwenyekiti wa Kijiji cha Sanya Hoye, Mosses Munuo, alisema wapitisha azimio la kutoa adhabu ya viboko na faini kwa kuwa ni malezi mabaya ya wazazi au walezi, baada ya wanafunzi kutoka shule.
“Kwenda baa na watoto nyakati za jioni au wakati wa kazi, huo ni ukatili na ni kinyume kabisa cha haki za watoto,” alisema Munuo.
“Kimsingi, jambo hili la baadhi ya wazazi au walezi kwenda baa na watoto na kukaa nao wakati mwingine hadi saa 3 mpaka saa 5 usiku halikubaliki.
Ndio maana wananchi wamesema watakaokutwa hatua zichukuliwe,” alisema.
Munuo alisema hali hiyo kwa sasa ni tatizo sugu kwa baadhi ya wakazi wa kijiji hicho, hivyo kusababisha ongezeko la watoto wanaoishi katika mazingira hatarishi na magumu.
Ulevi, pia, umesababisha watoto wengine kuachwa nyumbani bila ya uangalizi wowote, alisema Mwenyekiti huyo.
“Wakati wa jioni watoto wanastahili kuoga, kupumzika na baadaye kurejea yale waliyofundishwa darasani,” alisema Munuo na kuongeza:

“Sasa hawa wanaobeba watoto mgongoni na kwenda nao baa, wananchi wangu na hata mimi mwenyewe hatuliafiki. Na ndio maana wakataka tuanze kuchukua hatua.”
Serikali ya kijiji hicho pia imepiga marufuku uuzwaji pombe nyakati za kazi, na kutoa amri kwa baa zote kuanza biashara saa 9:00 alasiri kila siku na kuzifunga ifikapo saa 5:00 usiku.
Mei 12, mwaka huu wakazi zaidi ya 200 wa Kata ya Karansi wilayani humo, wakiwa katika mkutano ulioandaliwa na wazee wa mila wa kabila la Wameru, nao walipitisha uamuzi wa kuacharazwa viboko 60 hadi 70, wanaume watakaovaa suruali chini ya kiuno na wanawake watakaokutwa wamevaa sketi fupi.
NIPASHE