Thursday, 26 May 2016

RUFANI YA JAMHURI VS KITILYA JUMANNE


Mbali na Kitilya, washitakiwa wengine katika kesi hiyo ambao wote wanasota rumande ni aliyekuwa Miss Tanzania mwaka 1996, Shose Sinare na mwanasheria wa Benki ya Stanbic, Sioi Solomon.



Mkurugenzi wa Mashtaka nchini (DPP), alikata rufaa mahakamani hapo kupinga uamuzi wa Mahakama Kuu Tanzania, Kanda ya Dar es Salaam kutupa rufaa yake ya kupinga kuondolewa shtaka la kutakatisha fedha na Mahakama ya Hakimu Mkazi ya Kisutu ya jijini.

Rufaa hiyo itasikilizwa mbele ya jopo la Majaji watatu Jaji Bernad Luanda, Salum Massati na Aristoclas Kaijage wa mahakama hiyo.
Mei 6, mwaka huu, Mahakama Kuu iliyokuwa imeketi chini ya Jaji Mfawidhi Mosses Mzuna, ilitupilia mbali rufaa hiyo baada ya upande wa Jamhuri kuwasilisha pingamizi la awali kwamba rufaa hiyo imewasilishwa kinyume cha sheria.
Aidha, mahakama hiyo ilikubaliana na pingamizi la upande wa utetezi kwamba haina mamlaka ya kusikiliza rufaa hiyo dhidi ya washtakiwa.

Upande wa Jamhuri uliongozwa na Wakili wa Serikali Mkuu, Timon Vitalis akisaidiana na Mawakili wa Serikali Waandamizi, Theophil Mutakyawa na Shadrack Kimaro.
Upande wa Utetezi, uliongozwa na Mawakili, Dk. Ringo Tenga, Majura Magafu, Steve Axwesso, Alex Mgongolwa na Godiwn Nyaisa.
Jaji Mzuna alisema mahakama yake baada ya kupitia nakala mbalimbali za uamuzi uliotolewa katika kesi tofauti, amegundua haina mamlaka ya kusikiliza rufaa ya uamuzi mdogo ulioamriwa na mahakama ya chini.
“Rufaa hii haina miguu ya kusimama mahakamani hapa Upande wa Jamhuri una nafasi ya kuomba kufanya mabadiliko ya shtaka ama hati yote ya mashtaka dhidi ya washtakiwa,” alisema Jaji Mzuna.
"Pingamizi la utetezi limekubaliwa, mahakama hii haina mamlaka ya kusikiliza rufaa hiyo."

Washitakiwa hao walifikishwa mahakamani hapo kwa mara ya kwanza Aprili mosi, mwaka huu, wakikabiliwa na mashitaka manane likiwamo la kutakatisha Dola milioni sita za Marekani mali ya serikali.
Kitilya na wenzake wanakabiliwa na mashitaka hayo yanayohusu tuhuma za ufisadi katika kuiwezesha Serikali ya Tanzania kupata mkopo kutoka Benki ya Standard ya Uingereza kupitia mshirika wake Benki ya Stanbic Tanzania

NIPASHE.

No comments:

 

ADVERTISE WITH US

AFRICAN FASHION

PLACE YOUR ADS HERE!