Tuesday 24 May 2016

‘Marufuku kampuni kununua mashamba, kupima viwanja’

WAZIRI wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, William Lukuvi amepiga marufuku ununuzi wa mashamba, unaofanywa na kampuni binafsi na kuyapima kuwa viwanja. Akihitimisha mjadala wa hotuba ya bajeti ya wizara hiyo, Lukuvi alisema atakayenunua shamba, anapaswa kuhakikisha linabaki hivyo na kama anataka liwe viwanja, ni vema akakabidhi halmashauri libadilishwe matumizi.


“Kama kuna mtu binafsi amenunua mashamba kwa lengo la kupima viwanja imekula kwako kabidhi halmashauri itapanga, kupima na kumilikisha wenyewe kwani kuna watu wanakuja na brief case zao na kutajirika kwa kupima viwanja,” alisema Lukuvi.
Lukuvi aliagiza halmashauri kutofikiri ardhi ni kwa ajili ya kujitajirisha pekee na kusisitiza kuwa kuanzia sasa hati za viwanja zitatolewa baada ya mwezi mmoja badala ya ilivyokuwa awali miaka miwili.
Akizungumzia ujenzi holela, alisema awali serikali ilikuwa na jukumu la kupima na upangaji pekee yake, lakini hawakufanya vya kutosha jambo lililosababisha wananchi kuwatangulia na kujenga.
Kuhusu utoaji hati, alisema ofisini kwake kuna hati zaidi ya 4, 800 za watu waliokuwa hawajachukua wakiwemo walio nje ya nchi. Alisema mlundikano huo wa hati, unatokana na hisia za wamiliki kudhani zingechukua muda mrefu.
Alisisitiza wahusika waende kuzichukua. na kuwataka kwenda kuchukua. Lukuvi alisema kuanzia sasa utoaji hati utaishia wilayani baada ya kugawa mamlaka kwenye kanda kanda nane ambako yuko msajili atakayesaini.
Alisema vifaa vipo kwenye kanda. Aidha, alisema wameanzisha programu ya kupima na kupanga ardhi kwa kushirikiana na sekta binafsi kwa kuanzisha kampuni 58 za kupanga na kupima zilizosajiliwa.
Alisema kampuni binafsi zitapima na kupanga, lakini uamuzi wa mwisho utakuwa wa halmashauri. Akizungumzia suala la fidia, Waziri alisema lipo kisheria ikiwa eneo limechukuliwa kwa maendeleo au huduma.
Alitaka wananchi waliochukuliwa maeneo hayo, kutokuwa na wasiwasi na alisisitiza ni sawa na wameweka fedha benki kwa kuwa wakicheleweshewa fidia, watalipwa na riba.
Akizungumzia migogoro ya ardhi, alisema wizara yake imejipanga kushirikiana na Wizara ya Maliasili na Utalii, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi) na Wizara ya Kilimo na kufikia mipaka ya kijiji na kijiji, wakiwa na wataalamu na kufanya marekebisho ya mipaka ikibidi.

No comments:

 

ADVERTISE WITH US

AFRICAN FASHION

PLACE YOUR ADS HERE!