NDOTO ya Tanzania kuwa nchi ya viwanda, inaelekea kutimia baada ya Serikali ya Awamu ya Tano kuonesha kwa vitendo dhamira yake ya kuhakikisha ndoto hiyo inatimia.
Tangu wakati wa kampeni Ilani ya CCM ya mwaka 2015 iliponadiwa pamoja na kauli mbalimbali za wagombea wa chama hicho wakiongozwa na aliyekuwa mgombea urais, Dk John Magufuli, ahadi kubwa ilikuwa ni kujenga uchumi wa nchi kupitia viwanda. Ahadi hiyo inatokana na ukweli kuwa Tanzania imedhamiria kuhakikisha ifikapo mwaka 2025, inakuwa ni miongoni mwa nchi zilizo na uchumi wa kati.
Katika kuhakikisha ndoto hiyo inatimia, kupitia bajeti ya kwanza chini ya Serikali ya Awamu ya Tano ya Wizara ya Viwanda, Biashara na Uwekezaji, kipaumbele kikubwa kimewekwa katika sekta nzima ya viwanda. Hali hiyo ilijidhihirisha tangu, Serikali ilipowasilisha mapendekezo ya kiwango cha ukomo wa bajeti ya serikali kwa mwaka wa fedha 2016/17 ambayo inaonesha kuwa itatumika Sh trilioni 29.53 ikiwa ni ongezeko la trilioni 7 ikilinganishwa na bajeti ya mwaka wa fedha uliopita.
Sura hiyo ya bajeti ya mwaka 2016/17 inatofautiana na iliyopita iliyokuwa ya Sh trilioni 22.45 katika maeneo mengi, ikiwa ni pamoja na kiwango cha fedha kitakachotengwa kwa ajili ya shughuli za maendeleo, ambacho ni zaidi ya mara mbili ya fedha za eneo hilo katika bajeti iliyopita. Aidha katika mapendekezo hayo yaliyowasilishwa na Waziri wa Fedha, Dk Philip Mpango, shughuli zitakazopewa kipaumbele kwenye mipango hiyo ya maendeleo zimegawanywa katika maeneo manne.
Maeneo hayo ni viwanda vya kukuza uchumi na ujenzi wa msingi wa uchumi wa viwanda, kufungamanisha maendeleo ya uchumi na rasilimali watu, mazingira wezeshi kwa uendeshaji biashara na uwekezaji na pia usimamizi wa utekelezaji wa mpango. Katika kuthibitisha azma hiyo kwa vitendo, Waziri wa Viwanda, Biashara na Uwekezaji, Charles Mwijage, anapowasilisha hivi karibuni bungeni Dodoma makadirio ya mapato na matumizi kwa mwaka wa fedha wa 2016/17 ya wizara hiyo, alibainisha wazi kuwa kipaumbele kikubwa katika bajeti hiyo ni kuinua sekta ya viwanda.
Anasema katika kutimiza dhana ya Serikali ya kuijenga Tanzania yenye uchumi wa viwanda, wizara yake imejipanga kuhamasisha sekta binafsi miongoni mwa Watanzania na wageni kuwekeza kwenye sekta ya viwanda vidogo, vya kati na vikubwa. Anasema Serikali itawekeza nguvu zaidi kwenye viwanda vidogo na vya kati (SMEs) kwa kuwa ndio kwa sasa vinavyoongoza nchini kwa kutengeneza ajira na kuongeza pato la mtu mmoja mmoja.
Anafafanua kuwa kwa mujibu wa utafiti uliofanywa na wizara hiyo, sekta ya SMEs imetengeneza ajira takribani milioni 52 za Watanzania na kuchangia asilimia 28 kwenye Pato la Taifa (GDP). “Wizara hii itawezesha upatikanaji wa maeneo ya kujenga viwanda na kutoa ushauri kuhusu upatikanaji wa mitaji na teknolojia za kisasa. “Kwa ujumla wizara itabeba jukumu la kuibua wana viwanda, kuwakuza na kuwaendeleza,” anasisitiza Mwijage.
Anaeleza kuwa kwa kuzingatia msimamo huo, wizara hiyo itahakikisha viwanda vilivyopo vinafanya kazi kwa uwezo mkubwa kadri iwezekanavyo ili kudhibiti bidhaa za nje zinazoingia nchini bila ushindani ulio sawa. Anasema pia wizara hiyo itaondoa vikwazo vinavyopunguza uwezo wa kiushindani kwa viwanda vilivyopo nchini, itahamasisha wananchi kuwekeza katika sekta ya viwanda na itahamasisha wawekezaji wakubwa wa ndani na nje ya nchi kuwekeza katika sekta hiyo.
“Nawaahidi, tutapigana kufa au kupona ili tuwe na miundombinu wezeshi na saidizi iliyo tayari katika maeneo ya uwekezaji ngazi ya kanda na taifa. Nawashawishi wazawa wanaomiliki viwanda huu ndio wakati. Tutalinda viwanda vyenu , siwezi kulisha mtoto wa kware, na kuacha mtoto wa kuku afe,” anasema. Akizungumzia maendeleo ya viwanda nchini, Mwijage anabainisha kuwa idadi ya viwanda nchini imeendelea kuongezeka kutoka viwanda 125 mwaka 1961 baada ya Tanzania kupata Uhuru hadi kufikia viwanda 49,243 mwaka 2013.
Anasema kutokana na ukweli huo Serikali ya Awamu ya Tano imejipanga kuhakikisha inatimiza kwa kutekeleza ahadi yake ya kuijenga Tanzania ya viwanda kwa kuhakikisha viwanda vinajengwa na kusambazwa nchi nzima. Kwa mujibu wa Serikali kasi ya ukuaji wa viwanda imekua kati ya mwaka 2006 hadi mwaka 2013 ambapo vimeongezeka kutoka viwanda 5,153 mwaka 2005 hadi viwanda 49,243 mwaka 2013.
Pamoja na hayo, Mwijage anabainisha kuwa ni lengo la Serikali ya Awamu ya Tano kuona viwanda vyote vilivyobinafsishwa vinafanyakazi ambapo hadi sasa ni kati ya viwanda 106 vilivyofanyiwa tathmini, 45 vinafanya kazi vizuri, 24 vinasuasua na 37 vimefungwa. Anasema kutokana na ongezeko hilo la viwanda, viwanda vikubwa vinavyoajiri kuanzia watu 100 ni 247, viwanda vya kati vinavyoajiri kati ya watu 50 na 99 ni 170, viwanda vidogo vinavyoajiri kati ya watu watano na 49 ni 6,907 na viwanda vidogo sana vinavyoajiri chini ya watu watano ni 41,919.
Anasisitiza kuwa ni lengo la Serikali ya Awamu ya Tano kuona kuwa viwanda vyote vilivyobinafsishwa vinafanya kazi. “Viongozi wakuu wa nchi wamekuwa wakisisitiza utekelezaji wa lengo hilo na wizara yetu kwa kushirikiana na Msajili wa Hazina tunafuatilia jukumu hilo siku hadi siku,” anasema. Anafafanua kuwa mpango wa Serikali ni kuhakikisha kuwa viwanda 37 vilivyofungwa baada ya kubinafsishwa vinafanyiwa tathmini haraka kabla ya nusu ya kwanza ya mwaka wa fedha unaoanza Julai Mosi, mwaka huu.
“Nasisitiza kabisa kuhusu kuwa hatma ya viwanda visivyofanya kazi ni kwa wamiliki waliopewa kutekeleza mikataba ya mauzo au kupewa wawekezaji wapya ili waviendeshe,” anasema. Aidha, Mwijage anaeleza kuwa kupitia bajeti hiyo na mikakati ambayo Serikali hiyo imejiwekea, itahakikisha inahimiza na kusimamia mpango wa viwanda sehemu zote za nchi. Anasema tayari mamlaka za mikoa na wilaya zimeelekezwa kutenga maeneo kwa ajili ya shughuli ya viwanda na biashara.
“Hapa tutahakikisha kila eneo linakuwa na kiwanda kulingana na mahitaji ya eneo husika. Kwa mfano Tanga wanalima sana matunda hivyo viwanda vyake vitajikita katika eneo la kuzalisha bidhaa za matunda kama vile juisi.” Mwijage alisema katika kutimiza dhana ya kujenga Tanzania yenye uchumi wa viwanda, Wizara ya Viwanda imejipanga kuhamasisha sekta binafsi kwa Watanzania na wageni kuwekeza kwenye sekta ya viwanda vidogo, vya kati na vikubwa.
Makamu Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Viwanda na Biashara, Vicky Kamata anapongeza hatua ya Serikali ya Awamu ya Tano ya kuleta mapinduzi ya viwanda na kushauri hatua madhubuti zichukuliwe katika kushughulikia changamoto zinazoweza kukwamisha ndoto hiyo. “Serikali iweke kipaumbele katika suala la kutenga ardhi kwa ajili ya viwanda kwa kushirikisha halmashauri za wilaya na mikoa ikiwa ni pamoja na kujenga miundombinu bora kama vile barabara, reli, maji, umeme na mawasiliano,” anasisitiza.
No comments:
Post a Comment