Tuesday, 24 May 2016

AKAMATWA AKIPAKIA KETE ZA HEROIN NA COCAINE



Dar es Salaam.Mfanyabiashara maarufu wa Magomeni Makanya amekamatwa akiwa nyumbani kwake kwa tuhuma za kukutwa na kilo moja ya dawa za kulevya zenye mchanganyiko wa aina ya heroin na cocaine.



Mfanyabiashara huyo, Omary Kaunga (49), alikamatwa Mei 17 akidaiwa kufunga dawa hizo kwenye nailoni, akiwa tayari ameshatengeneza pipi 66 kwa ajili ya kusafirishwa.
Kamanda wa Kikosi cha Kuzuia na Kupambana na Dawa za Kulevya, Mihayo Msikhela alisema walipewa taarifa na raia mwema kuwa mtuhumiwa huyo huwa anafanya biashara ya dawa hizo.
Msikhela alisema baada ya kupewa taarifa hizo, Jeshi la Polisi lilipitia Serikali ya Mtaa huo kwenda kumkamata mtuhumiwa huyo.
“Tulifika nyumbani kwa mtuhumiwa huyo na kufanya upekuzi. Tulibaini dawa hizo za kulevya kazifunga kwenye nailoni mfano wa pipi ambazo zilikuwa 66 zenye uzito wa kilo moja,” alisema Msikhela.
Alisema baada ya kuzikamata, zilipelekwa kwa Mkemia Mkuu wa Serikali na utafiti wa awali umebaini kuwa ulikuwa mseto kati ya cocaine na heroin.
Msikhela alisema upelelezi umekamilika na wanatarajia kumfikisha mtuhumiwa huyo Mahakama ya Kisutu.
Kamanda huyo alitoa wito kwa wananchi kutoa ushirikiano kwa Jeshi la Polisi ili liweze kuwakamata watu wanaojihusisha na biashara ya dawa hizo ambazo zimepigwa marufuku.
Alisema Jeshi la Polisi kwa kushirikiana na vyombo vya usalama na wadau wa kudhibiti dawa hizo, wamejipanga ili kupambana na wafanyabiashara wa dawa hizo.


MWANANCHI.

No comments:

 

ADVERTISE WITH US

AFRICAN FASHION

PLACE YOUR ADS HERE!