Monday, 18 April 2016

Serikali yaongeza bajeti ya dawa hadi bil.251/-

SERIKALI ya Rais John Magufuli imeongeza bajeti yake ya kununua dawa kutoka Sh bilioni 41 kwa mwaka 2014/15 hadi Sh bilioni 251 mwaka huu.


Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Wazee na Watoto, Ummy Mwalimu amesema lengo la hatua hiyo ni kudhibiti uhaba wa dawa nchini.
Alisema hayo wilayani Kahama mkoani Shinyanga juzi, alipoelezea upatikanaji wa dawa nchini baada ya kuzindua kampeni ya kitaifa ya kupima Virusi Vya Ukimwi (VVU) kwa wasichana.
Uzinduzi huo ulifanyika viwanja vya Shule ya Msingi Kakola wilayani hapa. Ummy alisema Serikali ya Awamu ya Tano, itahakikisha hakuna mgonjwa atakayekufa kwa kukosa dawa, kwani katika bajeti ya mwaka huu imetenga fedha za kutosha kwa ajili ya kununua dawa.
“Bajeti ya dawa imeongezeka kutoka shilingi bilioni 41 hadi kufikia shilingi bilioni 251 hii inadhihirisha kuwa Serikali ya Awamu ya Tano imejipanga vyema kuwahudumia wananchi wake, ama hakika Hapa ni Kazi tu,” alisema.
Aliwahakikishia vijana wa kike waliojitokeza kwa wingi kupima afya zao kuwa hakuna atakayekosa dawa baada ya kugundulika ameathirika na maambukizi ya Virusi Vya Ukimwi.
“Mheshimiwa Rais amenipa Wizara ya Afya akijua mimi sio daktari, lakini ninawahakikishia kuwa kila mtoto atakayezaliwa hapa nchini atazaliwa bila ya maambukizi ya Virusi Vya Ukimwi maana zipo dawa za kutosha,” alisema Ummy.
Kaimu Katibu Tawala wa Mkoa wa Shinyanga, Mohamedi Njila alisema Serikali mkoani Shinyanga itahakikisha wananchi wake, wanapata huduma za afya kama inavyostahili sanjari na kuipongeza Wizara kuzindua kampeni maalumu ya kitaifa ya kupima maambukizi ya Virusi Vya Ukimwi kwa wasichana.

No comments:

 

ADVERTISE WITH US

AFRICAN FASHION

PLACE YOUR ADS HERE!