Sunday, 10 April 2016

Polisi bado yajipanga wizi kontena 11,019



JESHI la Polisi limesema bado linakusanya ushahidi ili kuwafikisha mahakamani watumishi 25 wa Bandari ya Dar es Salaam, ambao wanatuhumiwa kula njama za kutorosha makontena 11,019 na magari 2,019



kutoka bandari kavu (ICD) bila kulipa tozo ya Mamlaka ya Bandari (TPA).
Akizungumza na Nipashe, Kamishina wa Kanda Maalum ya Dar es Salaam, Simon Sirro alisema jana kuwa upelelezi dhidi ya watuhumiwa hao haujakamilika hivyo kusababishia kutokufikishwa kwao mahakamani.

Alisema Polisi inaendelea na uchunguzi wake dhidi ya waliohusika katika sakata la utoroshaji wa makontena bila kulipa tozo za Mamlaka ya Bandari.
“Upelelezi haujakamilika hivyo huwezi kuwapeleka watu mahakamani mpaka upelelezi ukamilike," alisema Sirro. "Ukiona tumechelewa kuwafikisha ujue upelelezi hujakamilika.
"Tunaendelea kukusanya upelelezi ili tuwatie hatiani.”
Alisema idadi ya watuhumiwa kwenye sakata hilo ambao wanawahoji kuhusiana na sakata hilo ataitoa Jumatano.
Kumekuwa na tetezi kuwa kuchelewa kufikishwa mahakamani kwa washukiwa hao kumechangiwa na kuwepo kwa mtoto wa kigogo wa zamani wa Polisi, aliyekuwa akifanya kazi bandarini.
Mtoto huyo wa kigogo ni miongoni mwa watumishi 25 wa Bandari waliosimamishwa kazi kwa kudaiwa kula njama kukwepa tozo za TPA.
Meneja wa Bandari ya Dar es Salaam, Hebel Mhanga, aliliambia gazeti hili wiki iliyopita kuwa jumla ya wafanyakazi 25 wameshasimamsihwa kazi kwa shutuma hiyo na wamewakabidhi polisi ushahidi wa nyaraka zilizotumiwa na wafanyakazi hao kufanikisha ukwepaji wa kodi.
“Polisi wamekuwa wakituomba ushahidi na tunawapa nyaraka zote muhimu wanazohitaji kwa ajili ya upelelezi na kama watajitaji nyaraka zingine sisi tuko tayari wakati wowote kuwapatia,” alisema Mhanga.
Alikiri kuwa upelelezi huo umechukua muda mrefu kwasababu uchunguzi wa kesi za kughushi huchukua muda mrefu kuzithibitisha.
“Sisi tunao ushahidi kwamba walikula njama za kusaidia uhalifu ufanyike maana huwezi kuruhusu mzigo utoke kama hujajiridhisha kwenye 'system' kwamba kweli malipo yamefanyika ndipo utoe ruhusa," alisema.
"Kuna ujanja ujanja ulikuwa ukifanyika na sisi tumeugundua ndiyo sababu tumewasimamisha.”
Nipashe ilimtafuta Mkurugenzi wa Mashtaka (DPP), Biswalo Mganga wiki hii, lakini hata hivyo alikataa kuzungumzia suala hilo limefikia wapi akisema kuwa maadili ya kazi yake hayamruhusu kutoa taarifa kama hizo kwenye vyombo vya habari.
“Kama taaluma yako ilivyo na miiko na taaluma ya waendesha mashitaka na wapelelezi ina miiko yake pia, huwezi kutoa taarifa kama hizo kabla hazijakamilka," alisema Biswalo.
"Msiwe na haraka mtaambiwa tu mambo yatakapokuwa tayari…."
Hivi karibuni, wafanyakazi wengine saba wa Mamlaka ya Bandari walikamatwa kwa tuhuma za kuipotezea Serikali mapato ya Sh. bilioni 48.55.
Kaimu Maneja Mawasiliano wa TPA, Janeth Ruzangi alisema mfanyakazi mmoja hajapatikana na polisi wanaendelea kumsaka ili afikishwe kwenye vyombo vya sheria.
NIPASHE

No comments:

 

ADVERTISE WITH US

AFRICAN FASHION

PLACE YOUR ADS HERE!