Tuesday 5 April 2016

Msaada MCC sawa na unga usio nyumbani mwako

Ni usemi wautumiao watu wa kabila la Wafipa kutoka mkoani Rukwa ambao kwa lugha yao husema, “Usu usi ung’anda umwako Itwi! Maana ya usemi huu ni kuwa kitu chochote japo kiwe na uzuri wa namna gani, kama unakipata kutoka kwa jirani haupaswi kukitegemea kwa asilimia 100. Ukiwekeza matumaini yote ya kukipata kila siku basi utambue kuwa ipo siku utaadhirika.
Maana ya usemi huo hautofautiani na kinachoonekana kati ya Tanzania na Shirika la Marekani la Changamoto za Milenia (MCC). Ni kwa miaka kadhaa shirika hilo limekuwa likiisaidia Tanzania fedha kwa ajili ya kuendesha miradi mbalimbali ya kimaendeleo. Miongoni mwa miradi iliyotekelezwa na fedha kutoka MCC ni pamoja na barabara ya Tunduma-Sumbawanga na pia miradi ya umeme vijijini. Hivi karibuni MCC imetangaza kusitisha msaada wa Dola za Marekani milioni 473 sawa na Sh trilioni moja kwa serikali ya Tanzania.
Shirika hilo limezuia fedha hizo za maendeleo kutokana na Tanzania kuitisha Uchaguzi wa marudio Zanzibar pamoja na kutumika kwa Sheria ya makosa ya Mitandao. Chini ya Mpango wa Uwekezaji wa MCC-2, fedha hizo zilikuwa ziende katika kuboresha huduma za umeme, ikiwemo usambazaji wa nishati hiyo katika vijiji vingine zaidi nchini. Kupitia MCC Tanzania imeweza kupiga hatua katika matumizi ya umeme kutoka asilimia 10 ya wakazi mwaka 2005 hadi asilimia 46.
Ongezeko hilo la matumizi ya umeme kwa Watanzania sehemu kubwa limetokana na MCC-1. Katika awamu ya kwanza Tanzania ilipokea kiasi cha Dola za Marekani milioni 698 ambazo zilitumika kwa ujenzi wa barabara za Tunduma-Sumbawanga,Tanga- Horohoro, Namtumbo-Songea hadi Mbinga. Fedha hizo pia zilitumika kujenga upya mfumo wa huduma za maji kwa ajili ya miji ya Dar es Salaam na Morogoro na pia kusambaza umeme katika vijiji vya mikoa 10 ya Tanzania bara.
Zilitumika pia kutandaza njia ya pili ya kusafirisha umeme chini ya Bahari ya Hindi kati ya Bara na Tanzania visiwani na pia kujenga barabara zote kuu za Kisiwa cha Pemba na baadhi ya barabara za Unguja kwa kiwango cha lami. Ukweli ni kuwa msaada huo ulikuwa muhimu na umeleta mabadiliko makubwa nchini. Kuboreshwa kwa barabara katika maeneo yaliyokuwa yamesahaulika kama ile ya Tunduma- Sumbawanga kumefungua fursa nyingi za kimaendeleo.
Ni wazi kwa mwananchi kama mkazi wa Rukwa unapomweleza suala la MCC kusitisha kuleta fedha nchini atasikitika kwakuwa ni mnufaika wa moja kwa moja. Lakini fedha hizi ukweli si za Watanzania hivyo ni sawa na unga wa kuomba kwa jirani. Unga wa kuomba kwa jirani hauwezi ukaupangia bajeti na kutegemea kuupata wakati wote maana mwenye nao anaweza kusitisha mara moja. Hata kama una imani na jirani anayekupa unga huo ni lazima pia ujue anakupa kutokana na kufurahi kwake,au kutosheka kwake.
Siku akiona haukumfurahisha au unga wake hautoshelezi ni wazi atabadili mawazo. Msaada wa MCC umekuwa kama jirani na unga wako kwa kuwa uamuzi huo wa jirani MCC kujiondoa katika miradi aliyokuwa akiifadhili Tanzania ni fundisho tosha kwa Watanzania katika vita yao ya kukabili umasikini na kujiletea maendeleo. Msaada wa unga wa jirani sasa umekuwa majivu na sasa inawapasa Watanzania kutafuta unga wao ili wasijikute wanakula majivu.
Kusitishwa kwa msaada huo kumeonekana kuwa gumzo kubwa ndani na nje ya Tanzania. Wadau mbalimbali wameonekana kuwa na michango tofauti ya kimawazo juu ya uamuzi huu. Mitandayo ya kijamii imejaa maoni mbalimbali ya wachangiaji juu ya hoja hiyo. Wapo wanaoonesha woga wakisema sasa Tanzania itakuwa kwenye wakati mgumu na wapo wale wanaosema ni wakati wa kujipanga vyema na kujitegemea.
Uamuzi huo ya MCC umekuja wakati serikali ya Tanzania chini ya Rais John Magufuli ikichukua hatua mbalimbali katika kuimarisha uchumi ili kuondokana na tabia ya kutembeza bakuli na kuitwa ombaomba kwa mataifa wahisani.
Tayari Watanzania wameshuhudia jitihada kadhaa zinazofanywa na serikali ya Rais Magufuli katika kuimarisha uchumi wa taifa lao. Miongoni mwa ambayo yaliyokwishafanyika ni pamoja na udhibiti wa mapato katika bandari kuu ya Dar es Salaam, ufuatiliaji wa malipo halali ya kodi sambamba na kuokoa fedha zilizokuwa zikipotea kwa kulipa mishahara wafanyakazi hewa.
Katika gazeti la HabariLeo la Machi 30 mwaka huu, Waziri wa Fedha na Mipango, Dk Phillip Mpango amekaririwa akisema serikali haishaangazwi na uamuzi wa MCC kwa kuwa dalili zilikwishaanza kuonekana tangu Desemba mwaka jana. “Tangu Desemba mwaka jana tulishasoma alama za nyakati na ndiyo sababu hatukuzijumuisha fedha za MCC-2 katika maandalizi ya Bajeti ya Serikali yanayoendelea kwa mwaka ujao wa fedha,” anasema Dk Mpango.
Anaendelea kusema, “tulisoma kwenye mitandao matamshi ya viongozi wa mfuko huo ndiyo maana tukaamua kutozijumuisha fedha za MCC kwenye bajeti ya mwaka ujao wa fedha,hivyo Watanzania wasiwe na wasiwasi juu ya kusitishwa kwa msaada huo.” Hata kabla ya kusitishwa kwa fedha za MCC, Rais John Magufuli amekuwa akikaririwa na vyombo vya habari akihimiza matumizi sahihi ya rasilimali zilizopo Tanzania pamoja na kila mwananchi kuwajibika katika kutoa kodi.
“Kila mmoja akifanya kazi, nchi haitahitaji wala kubembeleza misaada ya masharti kutoka nje kwa kuwa Tanzania ni nchi yenye neema, ina kila kitu na ikisimama imara na kila mmoja akatimiza wajibu wake, itakuwa ni nchi inayotoa msaada kwa nchi nyingine duniani” anasema Rais Magufuli. Magufuli amekuwa akisisitiza umuhimu wa kuifanya kazi na kusimamia vyema rasilimali za Taifa ili kuondokana na dhana ya kutegemea wahisani.
Magufuli alisikika mara nyingi akiwaambia wapiga kura kuwa kinachokosekana kwa Tanzania ni usimamizi imara wa rasilimali zilizopo ili ziweza kunufaisha Taifa kwa ujumla badala ya kunufaisha watu wachache. Magufuli ambaye anafanya kazi kwa manufaa ya wote bila kujali itikadi za kisiasa ameonesha umahiri mkubwa kwa kufanyia kazi mambo ambayo vyama vya upinzani wamekuwa wakilalamikia ikiwamo mfumo wa usimamizi rasilimali za Taifa.
Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) ni miongoni mwa vyama ambavyo viongozi wake wamekuwa wakililia mfumo wa usimamizi rasilimali za Taifa na kutoa angalizo juu ya kutegemea msaada wa MCC. Ni wazi kuwa kusitishwa kwa msaada huo wa Wamarekani ni fundisho kwa Watanzania na Waafrika wote kwa ujumla kuwa ni vyema kujenga moyo wa kujitegemea kuliko kutegemea misaada yenye masharti magumu yasiyokuwa na tija kwa Taifa.
NA JOACHIM NYAMBO.

No comments:

 

ADVERTISE WITH US

AFRICAN FASHION

PLACE YOUR ADS HERE!