RAIS John Magufuli amesema Mradi wa Mabasi Yaendayo Haraka jijini Dar es Salaam (Dart), utaanza karibuni huku nauli zake zikiwa nafuu kuliko zilizotangazwa awali, kufuatia Serikali kuzima jaribio la utapeli wa asilimia 49 ya hisa zake katika mradi huo.
Alisema hayo jana wakati akiweka jiwe la msingi la ujenzi wa barabara ya kwanza ya juu (Flyover) kwenye makutano ya barabara za Mandela na Nyerere, katika eneo la Tazara, kwa ufadhili wa Serikali ya Japan.
“Haiwezekani Serikali ikope Sh bilioni 388 kutoka Benki ya Dunia kwa ajili ya mradi huo halafu atokee mtu na kupewa nafasi ya pekee ya kutumia barabara tuliyolipa Watanzania wote, kisha aseme ni fedha zake.
Huo ni utapeli wa ajabu na mbele ya Serikali yangu nimefunga makufuli nikasema hiyo haiwezekani,” alisema. Aliwataka wakazi wa jiji hilo wasione kama walicheleweshwa kwa makusudi, bali uchelewaji huo ulifanywa kwa maslahi yao ili pia fedha zilizokopwa kwa niaba ya Watanzania zitumike kwa manufaa yao.
Alisema hiyo ndiyo sababu ilipotangazwa nauli ya juu kuliko hata ya daladala Serikali ilisema hilo haliwezekani. “Yaani fedha zikopwe na Watanzania, halafu nauli ipangwe kubwa kuliko hata ya daladala! Nauli zile nilisema haziwezekani, sasa tuko katika hatua za mwisho na magari yataanza kuonekana yakifanya kazi,”alisema na kuongeza kuwa, katika uongozi wake hakutakuwa na nafasi ya kuchezea Watanzania.
Kabla ya Serikali kuingilia kati mradi huo, kampuni inayoendesha mabasi hayo ya UDA-RT, ilipeleka mapendekezo ya nauli kwa Mamlaka ya Usafiri wa Nchi Kavu na Majini (Sumatra).
Kampuni hiyo ilipanga nauli ya chini kuwa ni Sh 700, tofauti na Sh 400 inayolipwa sasa katika usafiri wa daladala, ambapo pia wanafunzi watakaotumia usafiri huo, wangepaswa kulipa nusu yake, yaani Sh 350, tofauti na sasa ambapo wanalipa Sh 200.
UDA-RT ilipendekeza nauli ya safari kwenye njia kuu kuwa Sh 1,200 na safari katika njia kuu na pembeni kuwa Sh 1,400 ambapo wanafunzi katika njia hizo wangetakiwa kulipa nusu ya nauli hizo, yaani Sh 600 na Sh 700.
Kuhusu awamu ya pili ya mradi wa Dart, Rais Magufuli alisema utahusisha barabara ya Kilwa, Chang’ombe hadi Kawawa na barabara ya Juu katika makutano ya barabara ya Kilwa na barabara ya Mandela na makutano ya barabara ya Nyerere na Chang’ombe ambapo kwa sasa maandalizi yanaendelea kwa utafadhili wa Benki ya Maendeleo ya Afrika (ADB).
Alisema, awamu ya tatu ya mradi huo itahusisha barabara ya Nyerere, Gongo la Mboto, Uhuru na Azikiwe na sasa Serikali inaendelea na mazungumzo na Benki ya Dunia kupata mkopo wa kugharimia awamu hiyo ya tatu.
No comments:
Post a Comment