Monday, 11 April 2016

MAAJABU YA KITUNGUU SAUMU, PARACHICHI NA KAROTI KATIKA KUPAMBANA NA KISUKARI


Kisukari ni ugonjwa unaotishia kwa kasi afya za watu duniani na hata kusababisha vifo katika nchi nyingi hususan zinazoendelea, Tanzania ikiwamo. 

Chanzo kikubwa cha ugonjwa huo, ambao umesababisha baadhi ya watu kukatwa sehemu za miili ni unywaji wa pombe kupita kiasi, uvutaji wa sigara, ulaji wa vyakula usiofaa na mwili kukosa mazoezi.
Sambamba na sababu hizo, inaelezwa kuwa namna ya maisha wanayoishi watu katika siku hizi, yanayodaikwa kuwa ya kileo, pia huchangia ongezeko la maradhi hayo. 
Hatua hiyo husababisha watu kuwa na uzito mkubwa kupita kiasi, unene uliopitiliza na mwili kushindwa kuhimili harubu za maisha ya kila siku, hivyo mtu kujisikia kuchoka mara kwa mara. 
Kwa mujibu wa Shirika la Afya Duniani (WHO), zaidi ya watu milioni 380 diniani kote wanaugua kisukari huku mamilioni ya watu wakipoteza maisha kila mwaka kwa magonjwa yanasosababishwa na tatizo hilo.
Nchini Marekani, kwa mfano, zaidi ya watu milioni 19 wanaugua kisukari  na asilimia nane kati yao wamekumbwa na maradhi ya figo, moyo na upofu kwa kuchangiwa na kisukari.
Katika Tanzania, inaelezwa kuwa asilimia 9.1 ya watu wake wanaugua  kisukari na sababu kubwa zinazochangia ongezeko la ugonjwa huo ni pamoja na sigara, unywaji wapombe uliopitiliza na kutokufanya mazoezi. 
Dk. Omary Ubuguyu waHospitali ya Taifa ya Muhimbili(MNH), alinukuliwa hivi karibuni na vyombo vya habari akisema: “Unywaji wa pombe kuanzia chupa tano kwa wanaume na chupa nne kwa wanawake huchangia ongezeko la ugonjwa huu.”
WHO katika taarifa yake, inabaibnisha kwamba ugonjwa huo hivi sasa ni tishio kutokana na ongezeko la vifo mwaka hadi mwaka. Mwaka 2005 kwa mfano, watu milioni 1.1 walifariki dunia.
Kutokana na kasi hiyo, unaelezwa kwamba miaka 10 ijayo ugonjwa huo unaweza kusababisha ongezeko la vifo kwa asilimia 50 kulinganisha na ilivyo sasa.  
Kutokana na takwimu hizo, jitihada kubwa zinahitajika ili kudhibiti ugonjwa huo kuenea Zaidi, ili usiendelee kugharimu maisha ya mamilioni ya watu na hatimaye kupunguza nguvukazi katika mataifa mbalimbali.  
Katika kuhakikisha jitihada hizo zinafanikiwa, wataalamu wa afya wanashauri kwamba kila mtu anapaswa kufanya mazoezi mara mbili kwa siku- asubuhi na jioni. 
Mazoezi husaidia mfumo wa mwili kuimarisha na damu kuwa katika kiwango cha kawaida, hivyo kumwezesha mtu kuwa katika nafasi ya kuepuka kupata ugonjwa huo. 
VYAKULA MUHIMU 
Mbali na mazoezi, suala la lishe ni muhimu. Madaktari wanasema ili kujiepusha na kisukari, watu wanapaswa kula vyakula visivyo na mafuta mengi. Wanashauri kuwa vyakula ambavyo ni muhimu kwa afya ni vile vyenye protini ambavyo hujenga wili na vile vya kulinda mwili kwa maana ya mboga na matunda. 
Wataalamu wa afya wanapendekeza vyakula mbalimbali ambavyo vinaweza kumwepusha mtu kupatwa na kisukari na kwa yule ambaye ana ugonjwa huo, vinaweza kupunguza kiwango cha sukari katika damu na kuwa na siha njema.
Kitunguu swaumu
Hivi ni vyakula aina ya mizizi ambavyo vinaelezwa kuwa vina maajabu makubwa kiafya hasa vinapotumika mara kwa mara. Vinaelezwa kuwa ni kinga mujarabu dhidi ya magonjwa mbalimbali katika mwili wa binadamu.
Kwa mujibu wa watafiti kutoka Shule kuu ya Afya ya Jamii ya Chuo Kikuu cha Harvard, Marekani, vitunguu swaumu husaidia kupunguza kiwango cha sukari katika damu. Mtu mwenye kisukari anaweza kutumia vitunguu hivyo kwa kuchanganya na chakula kingine au kula sambamba na vyakula anavyoshauriwa na matabibu. 
“Kitunguu swaumu kina ‘allicin’, ‘allyl propyl disulfide’na ‘S-allyl cysteine sulfoxide’ ambazo huweka vizuri kiwango cha insulin. Pia hulinda ini kushambuliwa na maradhi mbalimbali,” inaeleza taarifa hiyo.
Wataalamu pia wanasema mtu mwenye kisukari anapotumia kitunguu swaumu, hukingwa au kupunguziwa maradhi yatokanayo na kisukari kama vile shinikizo la damu, figo kushindwa kufanya kazi hivyo kuhitaji kusafishwa mara kwa mara au kubadilishwa, magonjwa ya moyo, kiharusi, kuharibika kwa mfumo wa neva, kukatwa viungo vya mwili na upofu.
“Kwa ujumla, kitunguu swaumu kina faida nyingi katika kupambana na kisukari au kumsaidia mwenye kisukari kwani hupunguza kiwango cha sukari katika damu, kupambana na maambukizi, kupunguza lehemu mbaya, kuimarisha kinga ya mwili, kurekebisha shinikizo kla damu, na kuongeza msukumo wa damu,” inabainisha taarifa hiyo.
Aidha, taarifa ya utafiti ya Idara ya Sayansi ya Tiba ya Chuo Kikuu cha King Faisal, Saudi Arabia, inasema kitunguu swaumu kina nguvu katika kupambana na kisukari pamoja na shinikizo la damu.
Wataalamu hao walifanya utafiti kupitia makundi manne ya panya kwa siku 28. Kila kundi liliwekewa miligramu 200 za vitunguu swaumu na tangawizi na jamii zingine za vyakula tiba. 
Baada ya wiki nne, panya waliokuwa wamebainika kuwa na kisukari, ambao walipewa kitunguu swaumu, kiwango cha insulin kiliongezeka kwa asilimia 37. 
Parachichi
Hili ni tunda linalopatikana katika maeneo mengi nchini Tanzania na zaidi linastawi katika mikoa ya Kilimanjaro, Iringa, Mbeya na Arusha. Wataalamu wanaeleza kuwa.
Chama cha Kisukari cha Marekeni kinapendekeza watu wenye ugonjwa huo, kula parachichi kutokana na vitamin zilizomo, ambazo husaidia kupamabana na maradhi hayo au yale yasababishwayo na ugonjwa huo. 
Kwa mujibu wa chama hicho, parachichi lina viinilishe vingi ikiwamo ‘oleic acid’ ambayo husaidia kupunguza sukari katika damu na kupambana na maradhi ya moyo.
Wataalamu pia wanasema tunda hilo husaidia kuongeza kiwango cha insulin na ‘glucose’. Hata mafuta ya kupikia yatokanayo na parachichi yanaelezwa kuwa mazuri kwa afya ya binadamu.
Parachichi pia linaelezwa kuwa na vitamin C nyingi ambazo husaidia kuimarisha mishipa ya damu, hususan katika kapilari ndogo ambazo huwa katika hatari ya kuharibiwa kutokana na kisukari. Pia husaidia kuimarisha kinga ya mwili. 
“Kwa wagonjwa wa kisukari, parachichi lina nafasi kubwa katika kuuweka mwili sawa kutokana na kusawazisha sukari katika damu. 
Vitamini C husaidia pia kupunguza hatari za mwili kukumbwa na ugonjwa wa moyo, msongo wa mawazo na maradhi mengine,” inabainisha taarifa hiyo.
Sambamba na faida hizo, parachichi pia lina madini ya potasiamu ambayo hupendekezwa na wataalamu kwa wagonjwa wa kisukari kula vyakula vyenye madini hayo. 
Kazi kubwa ya madini hayo, ambayo hupatikana katika ndizi, ni kulinda moyo dhidi ya magonjwa, kurekebisha mfumo wa damu, kupambana na shinikizo la damu   
Kongosho pia huhitaji madini ya potasiamu ili kufanya kazi yake vizuri. Madini hayo pia huchangia kwa kiasi kikubwa katika kuiwezesha insulin kufanya kazi yake. 
Wataalamu wanaongeza kuwa parachichi lina vitamini E ambazo huisaidia kinga katika mishipa ya ateri. Wingiwa vitamin E, kwamujibu wa wataalamu, husaidia kupunguza lehemu mwilini na pia kuziimarisha ateri dhidi ya maradhi ya moyo na kiharusi.
Sambamba na faida hizo, Vitamini E hutoa ulinzi wa mwili dhidi ya kuharibika kwa mishipa ya neva, kwa mtu mwenye aina ya pili ya kisukari (type-2 diabetes). 
Licha ya kuwa na vitamini C, potasiamu na vitamini E, parachichi linaelezwa kuwa na virutubisho muhimu kwa mgonjwa wa kisukari. Virutubisho hivyo ni vitamin B ambavyo husaidia kulinda figo na mishipa ya moyo. 
Ndani ya parachichi pia kuna vitamini B6, ambazo kitaalamu huitwa ‘pyridoxine’ ni aina nyingine ya virutubisho vilivyomo katika vitamin B ambavyo pia ni muhimu kwa mgonjwa wa kisukari. Vitamini hizi husaidia kuweka sawa kiwango cha sukari mwilini. 
Aina hii ya vitamini hupatikana katika vyakula vya jamii ya mafuta kama vile mbegu za maboga, karanga na alizeti, ambazo pia madini ainja ya magnesium hupatikana humo.
Karoti
Karoti nijamii ya mimea ambayo katika familia nyingi hutumia kama kiungo cha mboga. Baadhi kuisaga na kutengeneza juisi. Lakini wataalamu wanaeleza kuwa ni muhimu sana katika kupambana na kisukari. 
Kwa mujibu wa wanasayansi wa Shule Kuu ya Tiba ya Chuo Kikuu cha Stanford, California nchinmi Marekani, watu wanaotumia karoti wanapata vitamin A ambavyo hupunguza hatari ya kukumbwa na kisukari. 
Sambamba na hilo, wanasema katika karoti kuna ‘gamma tocopherol’, ambazo zina vitamini E, zinazopatikana pia katika mafuta ya vyakula yatokanayo na mimea ambayo huzuia mwili kukumbwa na maradhi. 
Matunda 
Ulaji matunda kama vile zambarau, tufaa (apples) na yale ya jamii ya mizabibu, hupunguza hatari ya mtu kukumbwa na kisukari hasa kile cha aina ya pili.
Kwa mujibu wa Jarida la Tiba la Uingereza, matunda husaidia kupunguza athari za kukumbwa na maradhi hayo kwa kati ya asilimia 15 na 26 kulingana na aina ya tunda. 
Jarida hilo linazidi kubainisha kuwa ulaji wa matunda ya jamii ya zabibu, ni kinga murua kwa kinga dhidi ya kisukari kwa kuwa kusaidia kupunguza hatari ya kukumbwa na ugonjwa huo kwa asilimia 26, kulinganisha na mengine kama embe na machungwa ambayo yana asilimia ndogo.
Utafiti juu ya faida za ulaji matunda dhidi ya kisukari ulifanywa kwa kuchukua sampuli ya zaidi ya watu 187,000 nchini Marekani na kuonyesha manufaa hayo.Matunda ambayo yalihusishwa katika utafiti huo ni zabibu, zambarau, ndizi, mapeasi, matufaa, machungwa na ‘strawberries’.
Katika utafiti huo, ilibainika kwamba ulaji wa zabibu, ‘strawberries’ mapeasi, ndizi na tufaa, yana uwezo mkubwa wa kupunguza mtu kukumbwa na kisukari. 
Watafiti hao wanasema ulaji wa matunmda hayo asngalau mara tatu kwa wiki, yanamfanya mtu kuwa katika kinga dhidi ya kisukari. Hata hivyo wanasema matunda yote yana umuhimu katika mwili kujikinga na kisukari isipokuwa yale yenye sukari nyingi kama mananasi. 
Baadhi ya watu, badala ya kula matunda, hupendelea zaidi kutengeneza na kuwa juisi. Wataalamu wanasema juisi si nzuri kwa kujikinga na maradhi, kisukari kikiwemo. 
Profesa Qi Sun wa Shule Kuu ya Tiba ya Chuo Kikuu cha Harvard anasema: “Unapochakata matunda ili kutengeneza juisi, unaacha virutubisho muhimu ambavyo ni kinga dhidi ya maradhi. Kwa hiyo juisi si kinga dhidi ya magonjwa bali ni kiburudisho kama unavyokunya kimiminika kingine chochote.”
Profesa Sun, ambaye ni profesa mshiriki katika chuo hicho, anasema juisi za matunda zina virutubisho vyak iwango cha chini kulinganisha na tunda zima.
"Jambo lingine ambalo jamii inapaswa kujifunza ni kwamba kutengeneza juisi kutokana na matunda kunasababisha kimiminika hicho kuongezwa sukari wakati mwingine. Hatua hii inachangia kuongezeka kwa sukari katika damu na kupandisha kiwango cha insulin,” anasisitiza.
Profesa Sun anaongeza kuwa: “Kila siku jitahidi kupunguza hatari za kukumbwa na kisukari kadri uwezavyo. Moja ya hatua unazopaswa kuchukua ni kupunguza unywaji wa juisi na kuongeza ulaji wa matunda.” 
Wataalamu wanasema njia nzuri ya kupunguza kukumbwa na maradhi ya kisukari ni kula mlo kamili na wenye afya ambao unajumuisha matunda na mboga za majani. 
Naye Dk. Matthew Hobbs, Mkuu wa Kitengo cha Utafiti cha Taasisi ya Kisukari nchini Uingereza (Diabetes UK), anasema ushahidi wa kitafiti iunaonyesha kuwa matunda ni sehemu ya mlo kamili ambao hupunguza hatari ya kukumbwa na kisukari. 
Kamlesh Khunti, profesa wa afya ya msingi katika huduma za kisukari na maradhi ya moyo katika Chuo Kikuu cha Leicester, Uingereza, anasema ulaji matunda ni kinga tosha dhidi ya maradhi.
“Ulaji wa matunda ya aina zote ni kinga muhimu kwa mwili kwani husaidia kwa kiasi kikubwa katika kuukinga dhidi ya maradhi. Utafiti unaonyesha kuwa ulaji matunda unapunguza hatari ya kukummbwa na magonjwa,” anasema.
Anasema kutokana na umuhimu huo, serikali ya Uingereza kupitia wizara yake ya afya, inapendekeza ulaji wa vipande vitano vya matunda na mboga kila siku. 
Sambamba na hiyo, wataalamu hao pia wanashauri mtu kila siku kuuweka mwili wake ukiwa vizuri kwa kufanya mazoezi. Imeandaliwa Luhwago kwa msaada wa vyanzo mbalimbali vya habari. 

No comments:

 

ADVERTISE WITH US

AFRICAN FASHION

PLACE YOUR ADS HERE!