Friday, 4 March 2016

WABENA KABILA LENYE UTAJIRI WA MANENO

Chifu Elias Mkongwa akisimikwa kuwa mkuu wa kabila la Wabena Mkoa wa Njombe.

WABENA ni kabila la kibantu linalopatikana katika eneo la Nyanda za Juu Kusini mwa Tanzania wilaya ya Njombe mkoa wa Iringa.

Lugha yao inaitwa Kibena na makao yao makuu yanaitwa Ubena. Makao makuu ya Wabena ni Iringa katika eneo maarufu la Ubena, idadi kubwa ya Wabena inapatikana pia katika wilaya jirani ikiwa ni pamoja na Ulanga mkoani Morogoro. Kwa mujibu wa utafiti wa Profesa Sethi Nyagava kuhusu historia ya Wabena hadi mwaka 1914, maeneo makuu ya Wabena yamegawanyika katika sehemu tano ndani ya wilaya ya Njombe ambayo ni Ivanging’ombe, Usovi, Ikilavugi, Nyikolwe na Mfirika.
Utafiti uliofanywa na Dk Kilemile wa miaka ya hivi karibuni unaonesha Kibena ni lugha pana yenye utajiri wa maneno na lahaja kuu tano ambazo ni Ki-Kilavwugi inayotumiwa na wakazi wa eneo ya Ilembula; Kisovi inayotumiwa na Wabena wa eneo la Lusisi hadi Makambako. Lahaja nyingine ni Kimaswamu inayotumiwa na wakazi wa Imalinyi, Njombe mjini na sehemu ya kata ya Mdandu, Ki-Lupembe inayotumiwa na wakazi wa Lupembe na Kimavemba ambacho kutumiwa na Wabena wa Uwemba na sehemu ya tarafa ya Igominyi.
Dk Joram Kilemile anafafanua kuwa lugha ni moja tu ila tofauti ni ndogondogo, zinazotokana na matamshi. Mfano kukaza “dz”, kwa lahaja zote isipokuwa Kikilavwugi ambacho ingawa inaandikwa “dzi” inatamkwa kama “dji” kama vile ‘umuhudji’. Watumiaji wa lahaja ya Kilupembe inaandikwa “dzi” lakini wanatamka kama “chi” umuhuchi, achile - amekuja, wakati “adjile” (Kikilawugi)... Wengine wote wanakaza adzile, umuhudzi. Tofauti nyingine ni ya kutumia herufi K na H.
Mfano katika maneno Kamwene wengine husema Hamwene, Kangi na hangi pia ukukulima na uhulima. Ingawa historia ya Wabena haitoi jibu sahihi huu ya jina la kabila, watafiti mbalimbali wanahisi kuwa limetokana na ama kazi ya kuvuna ulezi yaani kubena au kutengeneza chumvi kwa kuwa majina ya eneo yalitokana na majina ya watu maarufu au kazi muhimu yenye kuwaingizia wananchi wengi kipato.
Kutokana na tofauti za kijiografia, shughuli za Wabena hutofautiana kutoka eneo moja hadi jingine. Hata hivyo, kwa ujumla Wabena wote ambao hivi sasa hupatikana wilaya za Njombe, Mufindi, Kilombero na Songea ni wakulima hodari. Wabena wanaoshi sehemu zenye mito na mabonde hujishughulisha pia na uvuvi, wakati wale wa ukanda wa juu wanajishughulisha na kilimo na ufugaji.
Wabena wana historia nzuri ya kudumisha ujamaa na ushirikiano kutokana na mfumo wao wa wakibadilishana mazao na mali mbalimbali. Wabena, kabila linalosifika kwa ukaribu pia lina sifa ya kipekee katika historia ya hatua za maendeleo ya binadamu kwa kuwa lilikuwa hodari wa kufua chuma. Kwa mujibu wa utafiti wa akiololojia uliofawanya na Profesa Paul Msemwa mwaka 2001 katika na maeneo yanayozunguka mji wa Njombe walikuwepo wakulima ambao walifua chuma kuanzia kipindi cha kame ya tano au hata kabla ya hapo, jambo linalodhihirisha kuwa Wabena walikuwa wakifua chuma.
Utafiti huo wa kisayansi umefanyika kwa kuchimbua ardhi kwa lengo la kutafuta masalia ya zana mbalimbali zilizotumiwa na watu wa kale umeweza kuibua masalia ya vipande vya vyungu na masalia ya viwanda vya chuma katika eneo linalokaliwa na Wabena ikiwamno Mgala Isitu, tarafa ya Igominyi. Vipande vya vyungu vilivyopatikana Mgala Isitu vina marembo yanayoshabihiana na marembo ya vyungu vilivyowahi kupatikana nchi za Zimbabwe na Zambia, jambo linalodhihirisha kuwa baadhi ya tamaduni za makabila ya kibantu zina mwingiliano na zinashabihiana.
Utafiti huo umebaini kuwa Wabena wa kale walitunza mazingira kwa kuwa walijenga viwanda vya chuma mbali na makazi ya watu na pia hakuna shughuli ya kuichumi iliyofanyika karibu na vyanzo vya maji. Hata hivyo, kadri miaka ilivyosonga mbele shughuli za viwandani zilisogezwa katika makazi ya watu na kusababisha uharibifu wa mazingira ambayo matokeo yake ni kutoweka kwa asilimia kubwa ya misitu ya asili na vyanzo vya maji.
Sehemu pekee ya Ubena ambayo bado ilikuwa maarufu katika uyeyushaji wa chuma hadi mwanzoni mwa kame ya 20 ni Njombe Kusini (Umavemba) na Mashariki ya Wilaya ya Njombe ambako bado kulikuwa na misitu ya asili. Hivi sasa maeneo hayo nayo yamebakiwa na maeneo machache ya misitu ya asili kwa kuwa sehemu kubwa ya misitu imetoweka kutokana na miti kukatwa kwa ajili ya mkaa wa kuyeyusha na kutengenezea chuma.
Maeneo mengine ya Ubena ambayo bado yana misitu ya asili ni yale ambayo yana umuhimu kimila kwa baadhi ya koo au kwa jamii ya Wabena kwa ujumla. Umuhimu wa uyeyushaji chuma katika eneo la Ubena linadhihirishwa na kupatikana kwa wingi mabaki ya viwanda. Pia, katika maonesho ya wakulima yaliyofanyika Iringa mwaka 1951, Wabena walionesha jinsi ya kupata chuma kutokana na udongo wenye madini ya chuma unaofahamika kwa jina la Mdapo kwa Lugha ya Kibena.
Historia kwa njia ya simulizi inasema baadhi ya mila na desturi za Wabena zinashabihiana na mila za jamii mbalimbali za Nyanda za Juu Kusini. Kwa mujibu wa historia Wabena wana uhusiano wa karibu koo za watu wa makabila ya Wahehe na Wanyakyusa ambao walihamia eneo linalojulikana kama Nyumbanitu lililoko kati ya Njombe na Mdandu katika barabara ya Njombe na Mbeya.
Kabla ya kuanza kwa mfumo wa kuhakikisha kuwa watoto wote wenye umri wa kwenda shule wanaandikishwa na kuhudhuria masomo watoto wa Kibena walitumia muda mingi katika michezo. Michezo hiyo ilichezwa kwa kuzingatia rika na jinsia ambapo watoto wa kiume walicheza maporini wakati wa kuchunga ng’ombe pia kulikuwa na michezo ya majumbani baada ya kazi.
Mchezo wa Pia maarufu kama Dila au Mbila kwa lugha ya Kibena huchezwa na wavulana wenye umri wa miaka mitano hadi 16. Vijana wa kiume wenye umri kati ya miaka 17 hadi 24 hupendelea mchezo wa mieleka na mshindi hupongezwa na kuonekana mtu hodari na mwenye ujasiri. Mchezo wa Mbingambinga huchezwa na watoto wa rika zote. Mchezo huo hutumia kamba zenye rangi mbalimbali zinazofungwa kushoto na kulia kisha huchezwa kwa kuzunguka kama na kutambua kama yenye rangi fulani kulingana na maelekezo ya mtu anayeongoza mchezo.
Wabena wanasifika kwa kushika dini. Hata kabla ya kuingia kwa dini ya Kiislamu na ya Kikristo waliamini katika mungu mmoja ambaye wanamwita Nguluvi au Inguluvi. Kutoka na imani Wabena husema, “Nguluvi, Inguluvi, yeliya gavile ifinu fyonde” ikiwa na maana Mungu aliyeumba vitu vyote. Huamini kwa kuwa Mungu aliumba vitu vyote ndiye mwenye mamlaka juu ya viumbe vyote duniani, ana uwezo, huruma, ujuzi na mwenye kutoa baraka kwa watu wanaotenda matendo mema na kuwaadhibu wote wanaotenda uovu.
Falsafa hiyo ilitawala na kuwa mwongozo wa maisha yote ya Wabena halisi. Kama ilivyo kwa makabila mengine yanayomwamini Mungu, Wabena wanaamini kwamba kuna ulimwengu mwingine baada ya maisha ya hapa duniani. Wanapokutana katika msiba hutumia salamu maalumu inayosema: “Mumwamukile uyu nayu muyingo (akwadza)” ikiwa na maana kuwa mwezetu ametangulia tutakakofika wote.
Hata hivyo, wanaamini kuwa sio kila mtu atafika katika ulimwengu mpya na kuuona utukufu wa Mungu. Ili kufikia ulimwengu huo mpya ni lazima kila mtu awe na matendo mema katika ulimwengu wa sasa.

No comments:

 

ADVERTISE WITH US

AFRICAN FASHION

PLACE YOUR ADS HERE!