
Dar es Salaam. Pamoja na Rais John Magufuli kuhaha kuboresha huduma za afya katika Hospitali ya Taifa Muhimbili ili kupunguza msongamano wa wagonjwa hasa wajawazito, huenda asifanikiwe endapo hospitali za chini zitabaki kama zilivyo sasa.
Mara baada ya Rais Magufuli kuapishwa Novemba 5, 2015 alianza kwa kufanya ziara Muhimbili Novemba 7, 2015 na kushuhudia mashine za MRI na CT-Scan zikiwa zimeharibika. Aliagiza zitengenezwe pia alipeleka vitanda na magodoro katika wodi ya wazazi.
Mwezi uliopita, Rais Magufuli aliagiza watumishi wa Wizara ya Afya waliokuwa wakitumia jengo la Kitengo cha Afya ya Uzazi na Mtoto kuhamisha ofisi zao na kuliacha ili litumike kama wodi ya wazazi. Mambo yote yametekelezwa na Serikali imefunga mashine mpya za MRI na CT-Scan ilizonunua kutoka kampuni ya Siemens badala ya zile za Phillips zilizokuwa zinaharibika mara kwa mara.
Hata hivyo, uchunguzi wa gazeti hili unaonyesha kuwa, Muhimbili itaendelea kuwa kimbilio la wagonjwa na hasa wajawazito kwa sababu hospitali za rufaa za Mwananyamala, Amana na Temeke zinakabiliwa na ukosefu wa huduma bora, uhaba wa madaktari, upungufu wa dawa na vifaatiba.
Pia, zahanati na vituo vya afya vina matatizo chungu nzima.
Uchunguzi umebaini kuwa baadhi ya wagonjwa wakifikishwa kwenye zahanati au vituo vya afya huomba waandikiwe kibali kwenda kutibiwa kwenye hospitali kubwa za rufaa ikiwamo Muhimbili ambako wanaamini kuna huduma bora.
Huduma zilivyo
Mkoa wa Dar es Salaam una zaidi ya zahanati 392, kati ya hizo za Serikali ni 89 na za mashirika au watu binafsi ni 303. Kwa upande wa vituo vya afya, Serikali ina vitano na mashirika au watu binafsi 27.
Vituo vya afya vitatu vya Serikali; Mnazi Mmoja, Mbagala Rangi Tatu na Sinza vimeshapandishwa hadhi kuwa hospitali na vimepewa magari ya kubebea wagonjwa huku, zahanati zikiendelea kujengwa kwenye maeneo yaliyo pembezoni.
Dar es Salaam kuna jumla ya hospitali 36 kati ya hizo saba ni za Serikali na 29 ni za mashirika au watu binafsi. Hospitali za Amana, Mwananyamala na Temeke zilipandishwa hadhi na kuwa za rufaa na ziliwezeshwa kwa kupewa madaktari bingwa wa magonjwa ya ndani, upasuaji, mifupa, watoto na uzazi.
Pia, Amana iliwezeshwa zaidi hadi kufikia kutoa huduma ya kupima magonjwa ya mfumo wa chakula kwa kutumia kipimo cha endoscope ambacho awali kilikuwa kikipatikana Muhimbili pekee.
Pamoja na mikakati hiyo iliyolenga kupunguza rufaa zisizo za lazima kwenda Muhimbili, uchunguzi unaonyesha kuwa Mwananyamala, Amana na Temeke nazo zimeelemewa wagonjwa ambao walipaswa kuhudumiwa na vituo vya afya na zahanati.
Baadhi ya wagonjwa wamesema changamoto wanazokumbana nazo kwenye hospitali za chini ni kukosekana kwa vipimo hususan vinavyotumia mashine za mionzi (x-ray, MRI na CT Scan), uhaba wa vitanda hivyo baadhi yao kulala chini na rushwa kwa watumishi wasio waaminifu.
Mwajuma Issa aliyekuwa anamuuguza ndugu yake Amana alisema wagonjwa wengi, hasa wajawazito, wanakimbilia Muhimbili kutokana na hospitali za chini kushindwa kukidhi mahitaji yao.
Hospitali ya Amana
Pamoja na maboresho, wagonjwa katika wodi ya wazazi Amana wanalalamikia kauli mbaya za baadhi ya wauguzi, huduma mbovu pale mgonjwa anapohitaji msaada, rushwa na uzembe.
Mfano ni Amina Said, mkazi wa Kivule, Ilala ambaye alijifungua Februari 28 saa 10 jioni lakini mtoto wake alifariki dunia muda mfupi baadaye kutokana na kutohudumiwa vizuri.
“Nilianza kuumwa uchungu saa sita mchana. Niliteseka bila msaada wowote hadi saa 10 nilipojifungua. Hakuna aliyenigusa kwa wakati wote huo, japo nilihitaji msaada wa karibu,” alilalamika Amina hospitalini hapo.
“Baada ya kuwa nimeshajifungua nililazimika kumwita nesi ili aje amsaidie mtoto wangu kwani alikuwa ameshazaliwa. Nilimzaa akiwa mzima, nikashangaa baadaye alifariki,” alisema.
Hata baada ya Rais Magufuli na Serikali yake kuanza kutumbua majipu kwa kuwasimamisha watumishi wazembe, wavivu na wala rushwa, bado baadhi ya wahudumu wanaomba na kupokea rushwa.
Mume wa amina, Omar Mpambo alisema licha ya kutumia fedha nyingi kulipia gharama za matibabu ya mkewe, bado hakupata msaada wakati wa kujifungua jambo ambalo lilisababisha mtoto wake kufariki.
“Kuna wakati niliambiwa nitoe Sh20,000 mfukoni nikawa na Sh15,000 ikabidi niende kuhangaika ili nipate iliyobaki kuokoa maisha ya mke wangu na mtoto,” alisema.
“Sijui nifanye nini, ila napenda Serikali ijue kuwa wanawake wanateseka kwenye hospitali za Serikali hasa hapa Dar es Salaam. Ukiwa huna fedha huduma utakayoambulia ni balaa tupu, uzembe umepoteza mwanangu,” alilalamika.
Alisema alilipia kumuona daktari, kitanda na vifaatiba zikiwamo glovu kwa Sh20,000 kinyume cha sera ya Serikali. Mganga mkuu wa hospitali hiyo, Dk Meshack Shimwela alikiri kuwapo kwa kero ya uhaba wa vifaa na dawa akisema: “Napenda kukuhakikishia kuwa tutakabiliana na changamoto hii, wagonjwa watapatiwa huduma, tatizo hili litaisha.”
Dk Shimwela alisema madaktari na wauguzi wa hospitali hiyo wanajitahidi kutoa huduma bora kadri ya uwezo wao lakini wanaelemewa na msongamano wa wagonjwa. Kuhusu uzembe uliosababisha mzazi kutopatiwa msaada Dk Shimwela alisema: “Kama mgonjwa alilipia kitanda huenda alipelekwa kwenye wodi maalumu lakini kiuhalisia mjamzito matibabu yake ni bure. Unaweza kukuta kuna kina mama 100 wodini, 40 kati yao wanataka kujifungua huku wauguzi wakiwa wanne tu kwa shifti moja. Kiukweli hali ni mbaya na kuna wakati tunalemewa.”
Kwa mtazamo wake, kama Serikali ingetengeneza sera ya kuhakikisha kila ilipo shule ya msingi kuwe na zahanati yenye ubora, vifaa na wataalamu wa kutosha msongamano wa wagonjwa usingekuwapo.
Katibu wa Afya wa Manispaa ya Ilala, Christopher Shechambo alisema hospitali hiyo inakabiliwa na changamoto nyingi ikiwamo ya uchache wa majengo, vifaa na watumishi.
Alisema Amana ina madaktari bingwa tisa kati ya 20 wanaotakiwa na haina chumba cha huduma za uangalizi maalumu (ICU) hivyo wagonjwa waliozidiwa hupelekwa Muhimbili, japo wangeweza kutibiwa hapo.
Alisema chumba kidogo cha upasuaji na uhaba wa dawa unaotokana na Bohari Kuu ya Dawa (MSD) kutokidhi mahitaji ni changamoto nyingine.
“Unaweza kulipia dawa kwa asilimia 100, ukapewa asilimia 20 tu hapo usitegemee kama wagonjwa watahudumiwa. Nadhani Serikali ilete mshindani wa MSD itasaidia kuongeza uhakika wa dawa kwenye hospitali zetu,” alisema.
Mganga Mkuu wa Manispaa ya Ilala, Victorina Ludovick alisema: “Tupo kwenye ujenzi wa hospitali ya kina mama, Chanika, itakayokuwa na vitanda 260. Hiyo itasaidia kupunguza msongamano ambao ni tatizo.”
Alisema Amana ina vitanda 15, wakati na wagonjwa wanaohitaji huduma ya uzazi huweza kufikia 40 kwa wakati mmoja.
Hospitali ya Temeke
Huduma za kliniki kwa wajawazito na wenye matatizo ya uzazi hutolewa katika ghorofa ya tatu ya hospitali hiyo. Adha ipo katika kuifikia kliniki hiyo ambako pia kuna msongamano mkubwa wa wagonjwa wanaosubiri matibabu.
“Tumekuja hapa tangu saa moja asubuhi, hali ndo hii. Vyumba vya madaktari vimefungwa, tunaambiwa tusubiri funguo zimepotea wanazitafuta mpaka sasa hivi ni saa nne inaelekea saa tano,” alilalamika mama mmoja.
Kwa upande wake, Khadija Khamisi aliyekuwa akimhudumia baba yake aliyelazwa hospitalini hapo alisema mzazi wake alikaa hapo kwa siku nne bila kupata kitanda kutokana na wingi wa wagonjwa.
Hata hivyo, Mganga mkuu wa hospitali hiyo, Dk Amani Malima alisema wingi wa wagonjwa ni changamoto kwani kwa siku wanawahudumia hadi wagonjwa 2,000.
Kuhusu mlango kufungwa na madaktari kutoonekana, Dk Malima alisema: “Kuna baadhi ya watumishi, hawapendi kazi, waliofunga ofisi nitawafuatilia na nikiwabaini hatua za kinidhamu zitachukuliwa dhidi yao,” alisema.
Hospitali ya Mwananyamala
Kilio kikubwa Mwananyamala ni wagonjwa kulala chini hasa wajawazito kutokana na uhaba wa vitanda. Mmoja aliyekataa kutaja jina kwa hofu ya kununiwa na madaktari, alidai kutelekezwa kwa kutopewa huduma kwa zaidi ya siku nne.
“Nasumbuliwa na kisukari, sijapata matibabu yoyote siku ya nne leo, mguu wangu una jeraha na linatoa usaha hakuna wa kunisafisha,” alilalamika mama huyo.
Mmoja wa ndugu wa mgonjwa huyo, Amina Simai alisema kutokana na huduma mbovu wameamua kumhamishia hospitali ya binafsi.
Katika wodi ya watoto, baadhi ya wanawake walilalamikia msongamano wakisema katika kitanda kimoja wanalazwa hadi watoto watatu. “...ukituchanganya na sisi mama zao tunakuwa sita. Huwezi kukesha usiku kucha ukiwa umekaa inabidi ulale, hivyo huwa tunajibana au kutandika kanga chini.” Alisema mgonjwa mmoja.
Hajra Minyaminya, aliyelazwa kwenye wodi hiyo alisema ukweli ni kwamba hakuna huduma ya bure kama inavyodaiwa.
“Kuna vitu kama dawa, lazima ununue, hakuna huduma bure hata kidogo labda tusubiri labda zitaanza,” alisema.
Mjamzito mmoja aliyekuwa akitarajia kujifungua wakati wowote alidai kuwa alilipa Sh9, 000 kwa ajili ya vipimo, ikiwamo mkojo na damu.
Mgonjwa mwingine Rashid Mbago aliyekuwa amelazwa wodi ya wanaume alisema, kinachomtesa ni bei kubwa ya dawa anazotakiwa kulipia.
Mganga Mkuu wa Hospitali hiyo alisema hawezi kuzungumza chochote hadi apate kibali kutoka kwa Mganga Mkuu wa Wilaya (DMO) ambaye naye hakupatikana kutoa ufafanuzi wala kibali.
Mkuu wa Mkoa
Kutokana na adha hizo kwa wagonjwa, Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Saidi Mecky Sadiki ameitaka Serikali kuboresha hospitali hizo ili zitoe huduma bora kwa wananchi.
Akizungumza katika kikao cha Kamati ya Ushauri ya Mkoa (RCC), Sadiki alisema ruzuku inayotolewa kuhudumia hospitali hizo haikidhi mahitaji na idadi ya wagonjwa.
Alisema uwezo wa hospitali za Ilala, Amana na Temeke ni kupokea wagonjwa 300 lakini zinapokea zaidi ya wagonjwa 450 hali inayosababisha wengine kulala chini kutokana na uhaba wa vitanda. Alisema hali hiyo inasababisha baadhi wazazi wanaojifungua kuruhusiwa mapema hata kabla hawajafikisha saa 48.













No comments:
Post a Comment