Sunday, 6 March 2016

Tumepewa tahadhari kuhusu mvua za masika, tuizingatie




Katika nchi zilizoendelea, taarifa ya hali ya hewa ni muhimu kwa kila mwananchi kiasi kwamba mtu hawezi kutoka nyumbani kwake asubuhi bila kwanza kufahamu hali ya hewa ya siku hiyo itakuwaje ili ajiandae.


Hivyo, mtu hutoka nyumbani akiwa amejitayarisha kwa mvua, baridi, upepo au joto kwa sababu hali ya hewa yaweza kuwa kikwazo katika shughuli zake. Kwa bahati mbaya, desturi hiyo Watanzania hatunayo.


Lakini ukweli ni kwamba, taarifa hizo si muhimu kwa mwananchi mmoja mmoja tu, bali kwa masilahi mapana ya nchi kwa sababu hali ya hewa ni suala mtambuka linaloathiri nyanja za kiuchumi, kijamii na kiafya.
Jana, Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA) ilitoa mwelekeo wa mvua kwa kipindi cha Machi hadi Mei na kuonyesha kwamba maeneo mengi nchini yatapata mvua za wastani na juu ya wastani hivyo kuwataka wananchi na mamlaka mbalimbali ambazo kwa njia moja au nyingine mvua huwa zina faida kwao au huleta athari mbaya kuzingatia ushauri uliotolewa na mamlaka hiyo.
Kwa wadau katika sekta ya kilimo, TMA inasema kwa maeneo ambayo yatapata mvua za juu ya wastani, wakulima wanashauriwa kutumia mbinu za kuongeza uzalishaji na kuzingatia ushauri wa wataalamu katika matumizi sahihi ya ardhi na mbegu. Ama katika maeneo yanayotarajiwa kupata mvua za chini ya wastani, wanapaswa kuzingatia mbinu za kuhifadhi maji pamoja na kudhibiti ubora wa mavuno.
Mamlaka pia imetoa ushauri kwa sekta ya maliasili na utalii kwamba katika maeneo yanayotarajiwa kupata mvua za juu ya wastani, mamlaka za usimamizi wa shughuli za utalii zinapaswa kuchukua hatua stahiki katika kuzuia uharibifu wa miundombinu. Kwa upande wa madini, TMO imewataka wachimbaji kuchukua tahadhari ili kupunguza madhara yanayoweza kusababishwa na maji pamoja na mafuriko kuingia migodini.
Aidha, mamlaka imetoa ushauri kwa sekta za maji na nishati kwamba katika maeneo yanayotarajiwa kupata mvua za wastani, taratibu za kuvuna na kuhifadhi maji zizingatiwe hususan kwa matumizi ya uzalishaji wa nishati.
Ushauri umeendelea hadi kwa mamlaka za miji kwamba zihakikishe mifumo ya njia za kupitisha maji inafanya kazi ili mtiririko wa maji usiparaganyike na kusababisha mafuriko na uharibifu wa miundombinu. Kadhalika, wadau wa sekta ya afya nao wametakiwa wajiandae kukabiliana na athari zitakazojitokeza kama vile magonjwa ya milipuko.
Hata waandishi wa habari nao wametakiwa waache kutoa taarifa zisizo rasmi au zisizo sahihi/zisizothibitishwa kuhusu mienendo ya hali ya hewa.
Tunaipongeza TMA kwa kutoa taarifa hiyo kwa ajili ya kuhakikisha kwamba mvua zinazotarajiwa kunyesha katika maeneo mbalimbali nchini, hazileti madhara na badala yake zinakuwa kichocheo cha maendeleo ya kiuchumi na kwa wanajamii ni tahadhari ya kuokoa maisha na kuwa na uzalishaji mzuri wa chakula. Itakuwa ni aibu kwa Taifa kama mwakani tutasikia kuwa tuna upungufu wa chakula wakati hali ya unyevunyevu katika ardhi ilidumu nchini kwa kipindi cha kutosha.
Watanzania tunapaswa, tujifunze kufuatilia taarifa za hali ya hewa na kuzifanyia kazi kwa faida yetu na mazingira yetu. Mamlaka imetimiza wajibu wake, sasa kazi kwetu.

No comments:

 

ADVERTISE WITH US

AFRICAN FASHION

PLACE YOUR ADS HERE!