Saturday, 5 March 2016

SAA TANO ZA BOSS NSSF

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Jenista
Dar es Salaam. Haijawahi kutokea. Ndivyo unavyoweza kusema kutokana na uteuzi wa Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Taifa la Mfuko wa Hifadhi ya Jamii (NSSF), Dk Carina Wangwe kudumu kwa saa tano tu, kuanzia juzi saa 11.15 jioni hadi saa 4.15 usiku.


Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Jenista Mhagama ndiye aliyemteua Dk Wangwe na kumtambulisha katika kikao cha menejimenti ya shirika hilo kilichofanyika juzi na kuhudhuriwa na watendaji waandamizi wa NSSF, pamoja na naibu waziri wa wizara hiyo, Antony Mavunde.

Katika hali ambayo haikutarajiwa, saa tano baadaye Mhagama alitengua uteuzi huo kwa maelezo kuwa baadhi ya taratibu hazikukamilika. Kutokana na sintofahamu hiyo, Katibu Mkuu Kiongozi, Balozi ombeni Sefue aliliambia gazeti hili jana kwamba taarifa ya uteuzi wa Dk Wangwe ilikosewa na kwamba alikuwa ameteuliwa kuwa mwangalizi tu, na siyo kaimu mkurugenzi mkuu.
Baada ya kikao cha utambulisho ambacho kilichofanyika kwa saa 1.10, Dk Wangwe ambaye ni Mkurugenzi wa Teknolojia ya Habari, Elimu na Mawasiliano (Tehama), katika Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Hifadhi ya Jamii (SSRA), alipewa nafasi ya kuzungumza na kueleza mikakati yake.
Sakata hilo lililoonekana kama sinema au mchezo wa kuigiza, lilitawala katika mitandao ya kijamii jana, huku kukiwa na madai kuwa uteuzi huo ulifanyika kienyeji bila mamlaka husika kushirikishwa na kwamba Dk Wangwe si raia wa Tanzania, bali ni Mganda aliyeolewa na Mtanzania.
Dk Wangwe ambaye simu yake ilikuwa inaita bila kupokea kutwa nzima ya jana, aliteuliwa kukaimu nafasi hiyo baada ya, Dk Ramadhan Dau kuteuliwa na Rais John Magufuli kuwa balozi, Februari 15 na tangu hapo shirika hilo limebaki bila uongozi wala bodi baada ya iliyokuwapo kumaliza muda wake.
“Kwa mamlaka aliyonayo ya kusimamia Shirika la Taifa la Hifadhi ya Jamii (NSSF) amemteua Dk Carina Wangwe kuwa Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Taifa la Hifadhi ya Jamii (NSSF). Uteuzi unaanza Februari 27 hadi hapo Rais atakapoteua rasmi mkurugenzi mkuu wa shirika,” ilieleza sehemu ya taarifa ya uteuzi iliyosomwa kwa vyombo vya habari jana saa 1.07 usiku.Hata hivyo, sehemu ya taarifa kwa vyombo vya habari iliyotumwa na Kaimu Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, Ikulu juzi saa 4.15 usiku, ilieleza kutenguliwa kwa uteuzi huo ikisema ni; “kutokana na kutokamilika kwa baadhi ya taratibu,” na kwamba uteuzi mpya kwa mujibu wa mamlaka na sheria utakapofanyika taarifa zitatolewa kwa wananchi.”Kuhusu suala hilo, Balozi Sefue alisema: “Nafikiri kumekuwa na mwingiliano wa mawasiliano. Kimsingi, Dk Wangwe alipaswa awe mwangalizi tu (caretaker).”
“Unajua ametokea SSRA ambao ni wadhibiti wa mifuko ya jamii. Hii ni kawaida, maana hata katika sekta ambazo zina fedha za watu, ni kawaida kusikia Benki Kuu (BoT) imebaini tatizo katika benki fulani na inapeleka mtu wake kusimamia benki hiyo kwa muda.”
Alisema baada ya Dau kuondoka NSSF hakukuwa na mtu, hivyo SSRA kwa kushirikiana na waziri, walimteua Dk Wangwe kuwa mwangalizi.
“Sasa Kiswahili cha neno caretaker kilikosewa na kuandikwa kaimu mkurugenzi mkuu na hiyo imetokea wakati ambao taratibu za kupata kaimu hazijakamilika, kutokana na mkanganyiko huo waziri aliamua kutengua tu,” alisema Balozi Sefue.
“Kwa nafasi ambayo alikuwa ameteuliwa, Dk Wangwe asingeweza kufanya uamuzi wowote pale NSSF, nadhani waziri atatoa taarifa yake leo (jana) kuhusu suala hili.”
Alipoulizwa nani anayetakiwa kufanya uteuzi, Sefue alisema: “Uteuzi wa mkurugenzi nafikiri ni wa Rais ila huu wa kukaimu una taratibu zake ambazo hazikukamilika na ndiyo maana ulifutwa. Ilikuwa lazima utenguliwe na ndiyo yafuate maelezo mengine.”
Alisema mchakato wa kumpata mkurugenzi wa shirika hilo unaendelea na kwamba mtu yeyote atakayeteuliwa kuwa mwangalizi, hawezi kuomba nafasi hiyo itakapotangazwa.
Kuhusu madai ya uraia wa Dk Wangwe, Balozi Sefue alisema: “Sijui kama ni raia wa nchi nyingine, lakini kwa kuwa anafanya kazi SSRA, hilo ndilo lililomfanya ateuliwe kuwa mwangalizi. Waziri anapoteua mtu huwa kuna taratibu na kama si raia wa Tanzania tungejua tu.”
Alisema SSRA haiwezi kupitisha mtu ambaye ana shaka, kwamba nafasi ya uangalizi huwa ni ya muda mfupi mpaka hapo atakapoteuliwa mtu mwingine wa kukaimu.
“Yameibuka mambo mengi kuwa si raia na nini… ila sisi tukaona bora uteuzi ulivyofutwa ili tutazame upya jambo lote,” alisema Sefue.

MWANANCHI.

No comments:

 

ADVERTISE WITH US

AFRICAN FASHION

PLACE YOUR ADS HERE!