Wabunge Halima Mdee (37), Mwita Waitara (40) na wenzao wawili, wamefikishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, Dar es Salaam, wakikabiliwa na shtaka la kujeruhi.
Mdee, Mbunge wa Jimbo la Kawe na Waitara wa Ukonga (wote Chadema) walipandishwa kizimbani saa 7:30 mchana na wenzao pamoja na Diwani wa Kata ya Kimara, Ephraim Kinyafu (33) na mfanyabiashara Rafii Juma (21).
Washtakiwa hao walisomewa mashitaka mbele Hakimu Mkazi Mkuu Huruma Shahidi aliyepangiwa kusikiliza kesi hiyo.
Upande wa Jamhuri, uliongozwa na Wakili Mkuu wa Serikali Faraja Nchimbi akisaidiana na Wakili wa Serikali Mwandamizi, Mutalemwa Kishenyi na Wakili wa Serikali Mwanaamina Kombakono.
Kombakono alidai kuwa Februari 27, mwaka huu, katika ukumbi wa Karimjee, Ilala, jijini Dar es Salaam, washtakiwa kwa pamoja walimjeruhi na kumsababishia majeraha Katibu Tawala wa Mkoa wa Dar es Salaam, Theresia Mmbando.
Washtakiwa walikana mashitaka hayo kwa nyakati tofauti.
Upande wa Jamhuri ulidai kuwa upelelezi wa kesi hiyo haujakamilika na haukuwa na pingamizi la dhamana. Pia uliomba hati ya kukamatwa mshtakiwa wa nne, Diwani wa Kimanga, Manase Njema (56) ambaye hajafikishwa mahakamani hapo.
Wakili wa utetezi, Peter Kibatala, alidai kuwa washtakiwa wote wanaomba dhamana kwa masharti nafuu.
Aidha alidai kuwa hoja ya kutolewa hati ya kukamatwa mshtakiwa wa nne, haina msingi kwa sababu hayuko nje kwa dhamana.
Hakimu Shahidi alisema washtakiwa watajidhamini kwa hati ya maneno yenye thamani ya Sh. milioni mbili kila mmoja. hata hivyo, alisema hati ya kukamatwa mshtakiwa wa nne itatolewa na mahakama.
Mapema juzi saa 2:00 asubuhi wanaodaiwa kuwa wanachama na baadhi ya wabunge wa Chadema, walifurika katika viunga vya mahakama hiyo kutokana na tetesi za makada hao kushikiliwa na Jeshi la Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, tangu Jumatatu iliyopita.
Hata hivyo, watuhumiwa hao walipandishwa kizimbani jana na kuachiwa kwa dhamana hadi Machi 16, mwaka huu kesi itakapotajwa.
POLISI
Watuhumiwa hao waliondoka Kituo Kikuu cha Polisi, chini ya ulinzi wa askari saa 13:14 mchana kwenda Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, wakitumia gari aina ya Noah lenye namba Z 322 FN.
Kabla ya kutolewa kituoni hapo, wanahabari waliofika eneo hilo kwa ajili ya kupata habari, waliondolewa huku wakitishiwa na askari wenye silaha kuwa wasipotii watawapiga risasi.
Wakati waandishi wakiwa kituoni hapo mara baada ya kuruhusiwa kuingia kwa ajili ya kazi hiyo, ghafla alifika askari mwenye silaha ambaye alisema ametumwa na bosi wake aliyekuwa kwenye ngazi za kuingilia ndani ya jengo hilo, kuuliza hao ni kina nani.
Alipojibiwa, aliwaamuru waondoke mara moja eneo hilo ndipo walipoongezeka askari wenye silaha na kuwarushia maneno wanahabari, huku mmoja akisema endapo watakaidi atawapiga risasi.
“Kama mnataka habari muende City Centre (katikati ya jiji) au Feri. hapa hakuna habari, mkihitajika mtaitwa.. tokeni,” alisikika mmoja wao akisema.
Mbunge wa Kilombero aachiwa
MBUNGE wa Jimbo la Kilomberov kupitia Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Peter Lijualikali, ambaye juzi alikamatwa na polisi kwa madai ya kukaidi agizo la jeshi hilo, ameachiwa kwa dhamana.
Mbali na Lijualikali, dereva wake Steven Mdata, na dereva wa Mbunge wa Viti Maalum Mkoa wa Morogoro (Chadema), Devotha Minja, aliyetambiliwa kwa jina moja la John, pia waliachiwa baada ya kutoa maelezo.
Lijualikali alikamatwa juzi baada ya kukaidi agizo la Jeshi la Polisi lililomtaka kutii amri ya msimamizi wa uchaguzi ya kutoingia katika mkutano wa uchaguzi wa wa Mwenyekiti wa Halmshauri ya Wilaya ya Kilombero, uliofanyika juzi .
Katika uchaguzi huo uliokuwa na ushindani mkali, mgombea wa CCM, David Ligazio, alimshinda mgombea wa Chadema, Joachim Lwena, huku nafasi ya makamu mwenyekiti ikichukuliwa na Adam Sungura wa CUF, aliyemshinda mgombea wa CCM, Emael Ndagalasi.
Akizungumza kwa njia ya simu baada ya kuachiwa, Lijualikali alisema alikamatwa kwa sababu ya uonevu uliofanywa na jeshi hilo la polisi kwa kuwa yeye ni Mbunge wa Kilombero, hivyo alipaswa kushiriki katika mkutano huo pasipo masharti yoyote ikiwamo yale yaliyowekwa na msimamizi wa uchaguzi huo.
“Kwa nini wanizuie? Mimi ni Mbunge wa Kilombero na nilikuwa naenda kuangalia madiwani wangu wanavyoshiriki katika kumchagua mwenyekiti lakini wananizuia,” alisema.
Katika mkutano huo ambao uliahirishwa, Lijualikali aligoma hivyo kulazimika kutolewa nje na polisi waliokuwa wakilinda mkutano huo.
NIPASHE
No comments:
Post a Comment