Rais John Magufuli amewatahadharisha watumishi wa umma wanaolipwa mishahara mikubwa na kuishi kama malaika, wajiandae kuishi kama shetani.
Hiyo itatokana na kukata mishahara yao kwa wale wanaolipwa zaidi ya Sh. milioni 40 na kushushwa hadi Sh. milioni 15.
Akihutubia katika mkutano wa hadhara kwenye uwanja wa Soka Wilaya ya Chato mkoani Geita, Magufuli alisema serikali yake haitaendelea kuwaonea haya baadhi ya watumishi ambao wanalipwa mishahara mikubwa huku wengine wakilipwa Sh. 300,000 kwa mwezi.
"Katika utawala wa serikali yangu, sikubali wachache waishi kama malaika na wengi waishi kishetani. Niwahakikishieni kuanzia bunge lijalo, tutaanza kufanya kazi hiyo ili nao waishi kama shetani," alisema.
Aliongeza kuwa: “Bahati nzuri hivi sasa tuna wasomi wengi. Yule atakayeona hawezi kuishi kwa mshahara wa Sh. milioni 15, bora aachie ngazi ili waje wengine wanaofaa.”
Hata hivyo, Rais Magufuli alitumia fursa hiyo kuagiza kamati za shule nchini ambazo zimeshindwa kusimamia nidhamu na kusababisha wanafunzi wengi kupata ufaulu wa alama sifuri, ziachie ngazi.
Mbali na kamati za shule, pia aliwataka wakuu wa shule ambao shule zao zimefanya vibaya katika mitihani ya kidato cha nne, kujitathimini kabla ya kungoja kutumbuliwa.
Alisema itasikitisha kuona nchi inaingia kwenye shirikisho la nchi wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki wakati wanafunzi wakipata ufaulu sifuri.
Rais Magufuli aliwasili wilayani Chato nyumbani kwao kwa ajili ya mapumziko ya wiki moja.
No comments:
Post a Comment