Friday 19 February 2016

WASICHANA WANG'ARA MTIHANI WA KIDATO CHA NNE


BARAZA la Mitihani Tanzania (NECTA) limetangaza matokeo ya Kidato cha Nne 2015, yakionesha ufaulu wa watahiniwa wote umeshuka kwa asilimia 0.80, ikilinganishwa na mwaka 2014 huku zaidi ya asilimia 80 ya watahiniwa waliofanya mtihani huo wakifeli somo la Hisabati.


Hata hivyo, asilimia 24 .7 ya watahiniwa wa shule 94.941 waliofaulu wamepata Daraja la I hadi III, hivyo kuwa na nafasi ya kuendelea na Kidato cha Tano na watahiniwa 113,489 sawa na asilimia 32 wamefeli mtihani huo.
Katika matokeo hayo yaliyotangazwa jana Dar es Salaam, wasichana wameshika nafasi ya kwanza na ya pili katika wanafunzi 10 bora kitaifa, ambao ni Butogwa Shija wa Canossa ya Dar es Salaam aliyefuatiwa na Congcong Wang wa Feza Girls pia ya Dar es Salaam.
Akitangaza matokeo hayo, Katibu Mtendaji wa Necta, Dk Charles Msonde alisema watahiniwa 272,947 kati ya watahiniwa 433,633 wa kujitegemea na shule, wamefaulu mtihani huo ambao ni wasichana 131,913 na wavulana 141,034.
Akielezea kwa upande wa watahiniwa wa shule, Dk Msonde alisema watahiniwa 240,996 (asilimia 67.91) ya watahiniwa 384,300 waliofanya mtihani, wamefaulu mtihani huo. Mwaka 2014, watahiniwa wa shule waliofaulu walikuwa ni 167,643 (asilimia 69.76). Hivyo kwa mwaka huu ufaulu umeshuka kwa asilimia 1.85.
Alisema kwa watahiniwa wa kujitegemea waliofaulu mtihani huo ni 31,951 sawa na asilimia 64.80. Mwaka 2014 watahiniwa waliofaulu walikuwa ni 29,162 sawa na asilimia 61.12. Hata hiyo, watahiniwa wa shule 94,941 sawa na asilimia 24.73 wamepata Daraja la I hadi III huku zaidi ya nusu ya waliofaulu kwa watahiniwa wa shule 146,055 wakipata Daraja la Nne.
Mwaka 2014 asilimia 30.72 (watahiniwa 73,832) walipata madaraja ya Distinction, Merit na Credit kwa kutumia mfumo wa Wastani wa Alama (GPA). Dk Msonde alisema watahiniwa wa Mtihani wa Maarifa, waliofaulu ni watahiniwa 7,536 kati ya 16,162.
Kwa mwaka 2014, watahiniwa 6,810 walifaulu. Akizungumzia ufaulu wa masomo kwa watahiniwa wa shule, alisema masomo ya Civics, Historia, Jiografia, Kiingereza, Kemia, Baiolojia, Commerce na Book-Keeping, ufaulu wake umepanda kati ya asilimia 1.09 na 12.86 ikilinganishwa na mwaka 2014.
“Ufaulu wa juu kabisa ni wa somo la Kiswahili unaoonesha asilimia 77.63 ya watahiniwa wote wa shule waliofanya somo hili wamefaulu. Ufaulu wa chini ni somo la Hisabati ambao ni asilimia 16.76. Mwaka 2014 ufaulu ulikuwa ni asilimia 19.58.” alifafanua bosi huyo wa Necta.
Msonde aliongeza: “Ufaulu wa masomo mengi upo chini ya asilimia 50, hata idadi ya watahiniwa waliopata Daraja la I, II na III ni takribani robo ya watahiniwa waliofanya mtihani hivyo juhudi zinahitajika katika kuinua kiwango cha ufaulu wa masomo na kuimarika zaidi kwa ubora wa elimu.”
Akizungumzia upangaji wa shule kwa ubora wa ufaulu, Dk Msonde alizitaja shule 10 bora kuwa ni Kaizirege (Kagera), Alliance Girls (Mwanza), St Francis Girls (Mbeya), Alliance Boys (Mwanza), Canossa (Dar es Salaam), Marian Boys (Pwani), Alliance Rock Army (Mwanza), Feza Girls na Feza Boys (Dar es Salaam) na Uru Seminary (Kilimanjaro).
Alizitaja shule zilizofanya vibaya kuwa ni Pande (Lindi), Igawa (Morogoro), Korona (Arusha), Sofi (Morogoro), Kurui (Pwani), Patema (Tanga), Saviak (Dar es Salaam), Gubalk (Dodoma), Kichangani na Malinyi (Morogoro).
Dk Msonde aliwataja watahiniwa waliofanya vizuri zaidi na shule wanazotoka kwenye mabano kuwa ni Butogwa (Canossa), Congcong (Feza Girls), Innocent Lawrence (Feza Boys), Dominick Aidano (Msolwa, Morogoro), Sang’udie Sang’udie (Ilboru), Asteria Chilambo na Belinda Magere (Canossa), Humfrey Kimanya (Msolwa), Bright Mwang’onda na Erick Mwang’ingo (Marian Boys).
Wasichana
Aliwataja wasichana 10 bora ni Butogwa (Canossa), Congcong (Feza Girls), Asteria Chilambo na Belinda Magere (Canossa), Lilian Kiwone na Marynas Duduye (St Francis Girls), Julieth Mbalilaki (Baobao), Vaileth Lazaro (Kilakala), Nancy Shao (Canossa) na Emmy Shemdangiwa (St Marys Mazinde Juu).
Wavulana
Aliwataja wavulana 10 bora ni Innocent Lawrence (Feza Boys), Dominick Aidano (Morogoro), Sang’udie Sang’udie (Ilboru), Humfrey Kimanya (Msolwa), Bright Mwang’onda na Erick Mwang’ingo (Marian Boys), Mohamed Kigume (Marian Boys), David Joseph (Ilboru), Daniel Mabimbi (Alliance Boys), William Kihanza (Mzumbe).
Aidha, Dk Msonde alisema Baraza limefuta matokeo yote ya watahiniwa 87 waliobainika kufanya udanganyifu katika mtihani, kati ya hao 25 ni wa kujitegemea na 52 ni wa shule na 10 ni watahiniwa na Mtihani wa Maarifa.
Baraza pia limezuia kutoka matokeo ya watahiniwa 23 wa shule, waliopata matatizo ya kiafya na kushindwa kufanya baadhi ya masomo huku watahiniwa 98 walioshindwa kufanya masomo yote, wote watapewa nafasi ya kufanya mitihani hiyo.
Katika hatua nyingine, Katibu Mtendaji huyo wa Necta alisema Baraza katika Mkutano wa 109, wameamua kurejesha utunuku wa mfumo wa madaraja wa Jumla ya Alama (Divisheni) kuanzia matokeo ya Kidato cha Nne ya mwaka 2015 kutokana na maoni ya wadau, ambao wameona mfumo wa Divisheni unaeleweka ukilinganisha na ule wa Wastani wa Alama (GPA) uliokuwa ukitumika awali.
Dk Msonde alisema kutokana na mabadiliko hayo, alama za ufaulu zitakuwa kama ifuatavyo; A (alama 75-100), B (65-74), C (45-64), D (30-44) na F (0-29) wakati wa Kidato cha Sita madaraja yatakuwa A (80-100), B+ (70-79), B (60-69), C (50-59), D (40-49), S (35-39) na F (0- 34).
Dk Msonde alisema madaraja ya ufaulu kwa Kidato cha Pili na Nne yatakuwa ni Daraja la I (pointi 7-17), II (pointi 18-21), III (pointi 22- 25), IV (pointi 26-33) na Daraja 0 (pointi 34-35) huku wa Kidato cha Sita itakuwa ni Daraja la I (pointi 3-9), II (pointi 10-12), III (pointi 18-19) na Daraja 0 (pointi 20-21).

No comments:

 

ADVERTISE WITH US

AFRICAN FASHION

PLACE YOUR ADS HERE!