SERIKALI imesema inatarajia kuona viongozi wakitibiwa nchini, kwa sababu hospitali za ndani zina wataalamu wenye uwezo wa kutibu magonjwa ambayo watu wengi wanaamini yanaweza kutibiwa nje pekee.
Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Ummy Mwalimu alisema jana wakati wa mkutano wa Mufti Mkuu wa Tanzania, Shehe Abubakary Zuberi na Waandishi wa Habari katika ukumbi wa Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete (JKCI) kuwa, viongozi wakitibiwa nchini, kiasi kikubwa cha fedha zinazolipwa na Serikali kwa ajili ya matibabu yao kitaokolewa.
Mufti aliitisha mkutano huo kwenye taasisi hiyo iliyo katika Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH), ili kuujulisha umma kuhusu kuruhusiwa kwake kutoka hospitali, baada ya kupona. Ummy alisema, hatua ya Mufti kutibiwa hospitalini hapo imeisaidia Serikali kutuma ujumbe kwa wananchi kuwa hata viongozi wengine wanaweza kutibiwa katika hospitali za ndani.
Ummy alihoji, “Ikiwa kiongozi mkubwa kama Mufti ametibiwa Muhimbili, iweje Serikali igharamie matibabu ya viongozi na watu wengine nje ya nchi?” Alisema, Serikali inafanya jitihada mbalimbali kuendelea kuboresha huduma za afya ikiwa ni pamoja na kuongeza wataalamu na vifaa tiba.
Aliongeza kuwa, inahamasisha Watanzania kutumia hospitali za ndani na kuachana na dhana kuwa nje ya nchi ndiko kwenye matibabu bora. Alikiri kuwepo kwa changamoto mbalimbali katika huduma za afya nchini na kusema kuwa, Serikali inafanya liwezekanalo kuhakikisha huduma hizo zinakuwa bora sambamba na kuifanya JKCI kuwa bora kuliko zote barani Afrika.
“Uboreshaji wa huduma za afya utaigusa Hospitali ya Muhimbili pia ili itoe huduma za kimataifa,” alisema. Akizungumzia afya yake, Mufti Zubery alisema, awali hakuwa na imani kutibiwa nchini na alikuwa amejipanga kwenda nje ya nchi kwa ajili ya matibabu, hadi aliposhauriwa kupata huduma katika taasisi hiyo.
“Nilikuwa siamini kutibiwa nchini na ninapozungumza muda huu nina tiketi yangu ya ndege niliyopaswa kutumia kufuata matibabu nje,” alisema na kuongeza kuwa Profesa Mohammed Janabi ambaye ni Mkuu wa JKCI ndiye aliyemsihi kuwaamini madaktari wa ndani.
Alisema, Serikali inapaswa kuliangalia vizuri suala la madaktari kuhakikisha wanapewa kipaumbele, ikiwa ni pamoja na kuhakikisha hospitali zinakuwa na vitendea kazi vya kutosha. Alisema Serikali ikiboresha huduma za matibabu nchini, gharama za watu kwenda kutibiwa nje ya Tanzania zitapungua. Tangu taasisi hiyo ianze kufanya kazi, imekwishatoa matibabu kwa watu mbalimbali, akiwemo Askofu Mkuu wa Jimbo Kuu Katoliki, Dar es Salaam, Mwadhama Polycarp Kardinali Pengo na Waziri Mkuu
HABARI LEO
HABARI LEO
No comments:
Post a Comment