Tuesday, 16 February 2016

MWALIMU WA SEKONDARI KATOROKA NA FEDHA ZA MITIHANI



Wajumbe wa Kamati ya Maendeleo ya Kata ya Lanagangabili wilayani Itilima mkoani Simiyu, wameomba Serikali kuhakikisha inamkamata na kumchukulia hatua mwalimu wa Shule ya Sekondari Lagangabili kwa tuhuma za ubadhirifu wa fedha na mali za shule.


Inadaiwa mwalimu huyo alifuja zaidi ya Sh1.5 milioni, ambazo zilikuwa ni michango ya wanafunzi wa kidato cha kwanza na tatu kwa ajili mitihani ya mwaka jana inayoandaliwa na Umoja wa Wakuu wa Shule za Sekondari nchini (Tahossa).
Pia anatuhumiwa kwa upotevu wa mabati 18 na mifuko tisa ya saruji ambavyo vilinunuliwa kwa ajili ya ujenzi wa maabara. Wakiwa katika kikao cha Kamati ya Maendeleo ya Kata, wajumbe hao walidai kuwa mwalimu huyo amekwamisha maendeleo ya shule hiyo, huku wanafunzi hao hadi sasa wakivuka kidato bila matokeo yao baada ya Tahossa kuyashikilia kutokana na kutolipiwa.
“Tunashangaa kuona ameitia hasara shule na hasa watoto wetu kwa kukwamisha matokeo halafu anapewa ruhusa ya kwenda kusoma” alisema Mwenyekiti wa Kijiji cha Lagangabilili, Telly Kilugara.Mwenyekiti wa Kijiji cha Ng’hesha, Bunga Hima alisema siyo muda wa kuwafumbia macho watumishi ambao ni wahalifu kama ilivyo kwa mwalimu huyo. Ofisa Elimu Sekondari Wilaya ya Itilima, Marwa Gekondo alisema mwalimu huyo anatafutwa ili akabidhi shule na kujibu tuhuma zinazomkabili.
Gekondo alisema kutokana na utaratibu wa Serikali mwalimu mwenye diploma hapaswi kuwa kiongozi wa shule hivyo mtuhumiwa huyo alikuwa na diploma na hivyo aliomba kwenda kusoma na ndipo tuhuma dhidi yake zikaibuka.
Akizungumza kwa niaba ya Mkurugenzi mtendaji wa wilaya hiyo, Kelisa Wambura alisema wameshapeleka vielelezo kwa mwanasheria wa halmashauri, polisi na idara ya usalama mkoa ili kusakwa mwalimu huyo.
“Tumeshasimamisha mshahara wake. TSD ambayo ni mamlaka ya nidhamu walibaini kuwa ni kesi ya jinai, tumemfungulia mashtaka ya wizi na tutamsaka hadi apatikane ili hatua dhidi yake zichukuliwe,” alisema.

MWANANCHI.

No comments:

 

ADVERTISE WITH US

AFRICAN FASHION

PLACE YOUR ADS HERE!