Wednesday 17 February 2016

KIPINDUPINDU BADO NI TISHIO

Ugonjwa wa kipindupindu ambao ulilipuka mwaka jana, umeendelea kuwa tishio nchini kutokana na kuripotiwa kwa wagonjwa wapya na kuongezeka kwa vifo.

Ugonjwa huo ulipolipuka uliikumba mikoa mingi nchini na taarifa za sasa zinaonyesha kwamba bado ni tishio, hivyo kuhitajika jitihada za ziada kukabiliana nao.
Hali hiyo ilibainishwa na Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia na Watoto na Wazee, Ummy Mwalimu, juzi na kuutaja Mkoa  wa Iringa  kwamba unaongoza kwa kuwa na idadi kubwa ya  wagonjwa wapya wa kipindupindu kati ya mikoa 11 nchini.
Waziri Mwalimu alisema takwimu za wiki iliyopita zilionyesha kuwa kuanzia  Februari 8 hadi 15, mwaka huu, idadi ya wagonjwa walioripotiwa imeongezeka kutoka 242 hadi 528 na kuwa kati yao, watano walifariki dunia.
  
Kwa mujibu wa Mwalimu, tangu ugonjwa wa kipindupindu ulipolipuka, jumla ya watu 15,853 wameugua ugonjwa huo kati yao 243 walifariki dunia kufikia Februari 14, mwaka huu nchini.
Mkoa wa Iringa umetajwa kuwa kinara kwa kuwa na wagonjwa wapya 199 ukifuatiwa na Mkoa wa Mwanza wenye wagonjwa 87 na Mkoa wa Mara 84. Pia imo  Morogoro 54, Arusha 49, Simiyu 16, Dodoma 11, Mbeya wanane, Kilimanjaro wanane, Dar es Salaam sita na Manyara sita. 
Takwimu hizi zinabainisha wazi kwamba ugonjwa wa kipindupindu bado ni tatizo kwa Taifa na hauwezi kudhibitiwa bila kudhibiti uchafu na ndiyo maana unasambaa kwa kasi ya kuwa hata katika maeneo ambayo walifanikiwa kuudhibiti.
Hali hii inapaswa kutufumbua macho kwamba inahitajika tahadhari kubwa katika kukabiliana na ugonjwa huo ambao chanzo chake ni uchafu. Ulipolipuka, mamlaka za serikali katika maeneo mengi nchini ziliwatangazia wananchi kuchukua hatua kwa kuzingatia kanuni za usafi.
Tulisikia kauli nyingi zikitolewa na viongozi wa kata, wilaya, mikoa wakionya wananchi katika maeneo yao kuchukua hatua dhidi ya ugonjwa huo. Wapo waliotishia kuwafungulia mashitaka watu watakaougua kipindupindu baada ya kupona. 
Kosa ambalo linafanyika ni kwamba viongozi wa kisiasa wamekuwa na tabia ya kutoa kauli na hatua kama za zimamoto pale linapotokea tatizo, lakini baada ya muda mfupi hakuna kinachoendelea.
Katika kukabiliana na ugonjwa wa kipindupindu zinahitajika hatua na tahadhari za muda mrefu na ikiwezekana ziwe endelevu. Kwa mfano, watu wote wanapaswa kuwa na vyoo maeneo ya kutupa taka.
Mamlaka nazo kwa upande wake zinatakiwa kupiga marufuku uuzaji wa vyakula na pombe za kienyeji katika mazingira machafu.
Ipo haja kwa mamlaka za afya kuhakikisha kwamba kanuni za usafi zinazingatiwa na zisisite kuchukua hatua za kisheria kwa watu wote wanakaobainika wakitenda kinyume.
Rais John Magufuli, Desemba mwaka jana, alifuta maadhimisho ya kumbukumbu ya miaka 54 ya Uhuru wa Tanganyika na kuelekeza kwamba wananchi wafanya usafi katika maeneo yao kama hatua ya kukabiliana na mlipuko wa kipindupindu.
Aidha, serikali imetangaza kwamba kuanzia Jumamosi ya mwisho ya mwezi huu, wananchi kote nchini watatakiwa kuwa wanafanya usafi katika maeneo hayo.  Tunashauri kuwa utamaduni huo uendelee kwa kuwa utasaidia kuyaweka mazingira yetu katika hali ya usafi wakati wote.
Kila mmoja anatakiwa kutambua kwamba ugonjwa wa kipindupindu haujadhibitiwa nchini, isipokuwa utadhibitiwa kwa kuepukana na mazingira machafu wakati wote.

No comments:

 

ADVERTISE WITH US

AFRICAN FASHION

PLACE YOUR ADS HERE!