Wednesday 17 February 2016

IJUE MAANA YA SAIKOLOGIA




Safu hii ninayoiandikia makala kila Jumapili ilikuwa ikiitwa “Jitambue”. Baada ya miaka mitatu ilibadilishwa jina lake ikaitwa “Saikolojia” Tangu wakati huo kuna wasomaji wengi ambao wamekuwa wakiniuliza maana ya neno hili.


Kuna baadhi ya wasomaji ambao wameniambia kuwa hawaniulizi kuhusu neno saikolojia kwa sababu tu limetumika kama jina la safu hii bali, kwa kuwa huwa nalitumia mara kwa mara katika makala zangu.
Hata hivyo, kama ilivyo kawaida yangu kabla ya kuanza kuandika makala hii niliwauliza watu kadhaa maana ya saikolojia.
Wengi walinijibu kuwa hawajui maana ya neno hilo. Wale wachache waliojaribu kunieleza maana yake walisema saikolojia ni elimu inayohusiana na fikira za watu.
Kuna mtu mmoja aliniambia kuwa ametafuta maana ya neno saikolojia katika kamusi na amekuta neno saikolojia limetafsiriwa kwa maneno mawili tu yaani “elimu nafsia” Nadhani tafsiri hizi tulizozipata zinatosha kwa kuanzia majadiliano kuhusu saikolojia ni nini, ina manufaa gani? Kutumiwa na nani? Hutumika vipi? na maswali” mengine kadhaa ya mtindo huu.
Kabla sijaendelea hebu soma kisa hiki
Siku moja mtoto alikuwa akienda shule. Mara akamuona mzee mmoja aliyeonekana mpole na mcheshi amesimama kando ya njia. Baada ya yule mzee kumsalimu mtoto kwa maneno mazuri alianza kumuuliza maswali. Swali la kwanza lilikuwa “Ewe kijana unakwenda wapi? Kijana akajibu “Nakwenda shule” Yule mzee akauliza tena; “Ukitoka shuleni unakwenda wapi? Kijana akajibu “Nitarudi nyumbani, Yule mzee akatabasamu na kusema. “Vyema; wewe kijana maisha yako, siku zote ni nyumbani-shuleni, shuleni- nyumbani. Siku utakapomaliza shule utaenda wapi? Kijana akajibu, “Baada ya kumaliza masomo yangu nitapata kazi nzuri na nitakuwa na ofisi yangu” Yule mzee akadakia tena na kusema, “Haya ukipata ofisi itakuwa tena nyumbani ofisini, ofisini nyumbani. Kwani baada ya hapo utakwenda wapi tena? Mtoto akajibu, “Nitaoa na kupata watoto nitakaowasomesha nao baadaye watapata kazi, kuoa na kupata watoto.
Yule mtu aliyekuwa akimuhoji yule kijana ni mwanafilosofia maarufu ulimwenguni aliyeitwa Socrates. Kama ilivyo saikolojia, falsafa ni sayansi inayohusiana na mwenendo na tabia ya binadamu.
Lakini maana kamili ya saikolojia nini? Neno saikolojia linatokana na neno la kiyunani “Psyche“ lenye maana ya nafsi au roho. Hivyo, saikolojia ni sayansi ya kuchunguza au kujifunza kuhusu roho au nafasi inavyofanya kazi. Kwa maana nyingine inahusiana na kufahamu sababu za wanadamu na wanyama kufanya mambo fulani. Wanasaikolojia hupenda kufahamu kwa upana tabia za binadamu, ikiwa ni pamoja na mahitaji yake, motisha na hamasa zake, hisia zake yaani mwenendo wa fikara zake na mihemko yake yaani michomo ya moyo wake.
Ninaamini hadi hapa tulipofika wasomaji wangu wanajiuliza kama ipo haja ya kila mtu kujua saikojojia. Jibu ni rahisi. Madhali tunaishi katika jamii na maisha yetu yanahusiana na watu wanaotuzunguka nyumbani, kazini, kijijini na umma mzima wa ulimwengu, tunahitaji saikolojia. Ndiyo itakayotusaidia kuchukuzana au kuendana vyema na watu wengine na kuwa na maisha ya maelewano na ushirikiano mkubwa.
Je,tutajifunzaje saikolojia ili tuielewe na kuweza kuitumia katika maisha? Kila mtu anaposikia neno saikolojia huliona kama ni somo kubwa ambalo pengine inabidi ahudhurie mafunzo maalum kwenye chuo maalumu.
Hii siyo kweli. Inatubidi tufahamu kuwa kila mmoja wetu amekuwa akitumia nadharia za kisaikolojia bila kujua. Hebu tafakari mifano michache ya matumizi ya saikolojia. Baba anawambia watoto wake wanaosoma shule.
“Yeyote kati yenu atakayefuzu na kuingia shule ya sekondari nitamnunulia baiskeli au kompyuta mpakato” Mfano mwingine “Mama anawambia watoto ‘Yeyote kati yenu atakayetunza vizuri nguo zake za shule na za nyumbani nitamuandalia keki ya siku sherehe yake ya kuzaliwa.
Wengi wetu tunapokuwa tunahitaji msaada kutoka kwa mtu ambaye hatuna nasaba naye ya ukoo tunamwita ndugu na pengine hata kumsifu mbele ya watu wengine ili mradi atupatie msaada tunaouhitaji.
Nakumbuka tulipokuwa vijana tulipenda kuwaambia wapenzi wetu maneno kama vile sili, sishibi na silali mpenzi wangu ili kuwahamasisha watupende zaidi.
Lakini kundi la watu wanaohitaji kuifahamu saikolojia na kuweza kuitumia ni viongozi wa vikundi vya aina zote, kutoka kwenye ngazi ya familia hadi kwenye umma. Hii ni kwa sababu kiongozi hana budi kuweza kuendana vyema na wanakikundi anaowaongoza. Wakati fundi wa mitambo unaposhughulika na mitambo yake, kiongozi hushughulika na watu. Fundi wa mtambo hana budi kuelewa jinsi mtambo wake ulivyoundwa na jinsi unavyofanya kazi.
Vile vile kiongozi wa kikundi anapoona wanakikundi wake wamekwama kutekeleza shughuli za kikundi hana budi kutambua sababu ni nini na jinsi ya kuirekebisha hali hiyo. Saikolojia ndiyo inayompatia uelewa wa mahitaji ya binadamu na maisha yake. Kadri kiongozi anavyopata weledi wa kutosha kuhusu nafsi ya binadamu mmoja mmoja na mwelekeo wake katika kundi ndivyo kadri atakavyoweza kuitenda kazi yake ya ongozi vyema zaidi.

MWANANCHI.

No comments:

 

ADVERTISE WITH US

AFRICAN FASHION

PLACE YOUR ADS HERE!