Thursday 18 February 2016

ASKARI MAGEREZA MBARONI KWA KUMTOROSHA MSHITAKIWA.



Mwanasheria wa Serikali na askari magereza wawili wanashikiliwa na polisi mkoani Katavi kwa tuhuma za kumtorosha kwa siku 124 mshtakiwa wa kesi ya kujaribu kumuua mlemavu wa ngozi (albino).



Kamanda wa polisi Mkoa wa Katavi, Dhahiri Kidavashari alisema jana kuwa watuhumiwa hao walifanya kitendo hicho Oktoba 12 mwaka jana baada ya kupokea rushwa ya Sh3 milioni.
Kidavashari alisema watuhumiwa hao walikamatwa baada ya kupata taarifa za siri kutoka kwa raia wema.
Alisema uchunguzi ulifanyika Januari 19 na kubaini kuwa mshtakiwa huyo aliyetoroshwa alimkata kiganja cha mkono Limi Luchoma (30) na kufunguliwa shitaka.
Alisema ndugu wa mshtakiwa huyo ndiyo waliotekeleza mpanwa kutoroshwa mtuhumiwa huyo kisha kwenda kumficha Kijiji cha Kipande kilichopo mkoani Rukwa.
Kidavashari alisema mshtakiwa huyo ni mzoefu kwa vitendo vya kutoroka gerezani kwani kabla ya kufanya tukio hilo, alikuwa ametoroka katika Gereza la Kalila Nkulunkulu wakati akitumikia kifungo cha miaka mitano jela kwa kosa la wizi wa mifugo.
Kidavashari alisema watuhumiwa hao wanashikiliwa na polisi wakisubiri uchunguzi kukamilika ili wafikishwe mahakamani kujibu mashtaka ya kumtorosha mshtakiwa huyo.
Alitoa wito kwa watumishi wa umma na wa sekta binafsi kufanya kazi kwa kufuata misingi ya utumishi huku wakiendelea kuihudumia jamii kwa ukaribu.
Kidavashari alisema cheo ni dhamana katika kutoa huduma kwa jamii na kuonya kuwa polisi haitasita kumchukulia hatua za kisheria atakayebainika kukiuka sheria na kujihusisha na vitendo vya uhalifu.

No comments:

 

ADVERTISE WITH US

AFRICAN FASHION

PLACE YOUR ADS HERE!