VITAMINI A ni mojawapo ya virutubishi muhimu katika kipindi chote cha maisha ya binadamu. Vitamini hii huhitajika mwilini kwa ajili ya kusaidia macho kuona vizuri, ukuaji na maendeleo mazuri ya mtoto na kuimarisha kinga ya mwilini dhidi ya maradhi mbalimbali ya kuambukiza.
Maziwa ya mama ni chanzo bora zaidi cha awali cha vitamin A kwa watoto wachanga na wale ambao hawajafikia umri wa miaka miwili. Vile vile vyakula vyenye vitamin A kwa wingi ni vile vitokanavyo na wanyama, mfano maziwa ya wanyama, mtindi, siagi, jibini, nyama, samaki, ini, na kiini cha yai na vile vitokanavyo na mimea kama vile mboga za majani zenye rangi ya kijani kibichi. Pia matunda yenye rangi ya manjano, mafuta ya mawese, karoti na viazi vitamu vyenye rangi ya manjano.
Vitamin A pia hupatikana kwenye vyakula vilivyoongezewa kirutubishi hiki. Mratibu utoaji matone ya vitamin A na tiba ya minyoo Tanzania, Francis Modaha anaeleza kuwa maziwa ya mama ni chanzo cha vitamin A kwa mtoto kwa miezi sita ya mwanzo. Modaha anasema lakini sio watoto wote nchini wanaonyonyeshwa maziwa ya mama pekee bila kupewa kinywaji au chakula kingine hadi wanapofikia umri wa miezi sita na kisha kuendelea kunyonyeshwa maziwa ya mama hadi kufikia miaka miwili au zaidi.
Mratibu huyo anasema vyakula wanavyopewa watoto wadogo havina vitamin A ya kutosheleza mahitaji yao kwa sababu hula kiasi kidogo cha chakula na familia nyingi hazifahamu vyakula vyenye kuongeza vitamin A kwenye vyakula vinavyotumiwa kwa wingi. Anasema utoaji wa matone ya vitamin A umeonesha kuwa ni njia ya gharama nafuu na yenye ufanisi inayoweza kutumiwa na nchi ili kuzuia na kutibu upungufu wa vitamin A kwenye ini.
Vile vile hifadhi hiyo ya vitamin A mwilini inaweza kutumika kwa kipindi cha miezi minne hadi sita hivyo utoaji wa matone ya vitamin A kwa watoto kila baada ya miezi sita ni mbinu bora ya kuwakinga dhidi ya athari mbaya za upungufu wa vitamin A mwilini. Anasisitiza kuwa ni muhimu mtoto apate matone ya vitamin A kila baada ya miezi sita vinginevyo akiba ya vitamin A iliyopo kwenye ini lake inaweza kupungua au kuisha kabisa.
Anasema matone ya vitamin A huokoa maisha ya watoto kwa kuwalinda dhidi ya maradhi hatari ikiwemo kuharisha, surua na ya mfumo wa hewa pia husaidia kuzuia upofu. Na watoto wasiopata matone ya vitamin A wana uwezekano mkubwa zaidi wa kuugua maradhi, kupofuka na hata kufariki dunia. Anashauri kila mzazi au mlezi wa mtoto mdogo anapaswa kufahamu umuhimu wa vitamin A kwa ukuaji, maendeleo mazuri, afya na uhai wa mtoto.
“Vile vile vyakula tulavyo havikidhi mahitaji ya vitamin A kwa watoto kwani hula kiasi kidogo wakati mahitaji yao ni makubwa na hivyo ni muhimu wapatiwe matone ya vitamin A mara mbili kila mwaka. Pia wanapaswa kufahamu wakati na mahali ambapo zoezi la utoaji wa matone ya vitamin A hufanyika ili waweze kuwapeleka watoto wao kila baada ya miezi sita. Modaha anaeleza kila mtoto mwenye umri wa kati ya miezi sita au miaka mitano anahitaji kupewa matone ya vitamin A mara mbili kwa mwaka.
Hapa nchini matone hayo hutolewa kwa watoto mara mbili kwa mwaka. mwezi wa sita na mwezi wa 12. Kwa maelezo ya mratibu huyo, wakati wa utoaji wa matone hayo watoto wote wenye umri wa mwaka moja hadi miaka mitano hupatiwa pia dawa ya minyoo. Anasema wanatoa matone hayo kwa sababu familia haziwezi kumudu kuwapa watoto wao vyakula vyenye vitamin A kwa wingi.
Vile vile vyakula vya gharama nafuu vyenye vitamin A kwa wingi havipatikani kwa misimu yote katika mwaka. Anasema vitamin A iliyomo kwenye chakula hupotea wakati wa matayarisho. Modaha anaeleza zaidi kuwa maradhi kama vile kuharisha, surua na maradhi ya mfumo wa hewa husababisha upungufu wa vitamin A mwilini. Modaha anaeleza kuwa watoto na wanawake huathirika zaidi na tatizo la upungufu wa vitamin A kutokana na sababu mbalimbali.
Akifafanua hilo anasema watoto wanahitaji vitamin A kwa ajili ya ukuaji na maendeleo mazuri na kuimarisha kinga dhidi ya maradhi mbalimbali ya utotoni. Upungufu wa vitamin A kwa watotot unaweza kusababishwa na ulaji duni ikiwa ni pamoja na kutonyonya vizuri maziwa ya mama, kuwalisha watoto vyakula vya nyongeza visivyokuwa na vitamin A ya kutosha na kuwapa maziwa mbadala wa maziwa ya mama.
Pia kitendo cha kuwaachisha watoto kunyonya maziwa ya mama mapema kabla ya kutimiza umri wa miaka miwili husababisha upungufu wa vitamin A, kiwango kisichokidhi cha vitamin A kwenye maziwa ya mama kutokana na lishe duni na maambukizi ya maradhi. Kwa upande wa wanawake wajawazito wanahitaji vitamin A kwa ajili ya kusaidia ukuaji na maendeleo mazuri ya mimba.
Pia wanawake wanaonyonyesha wanahitaji vitamin A kwa ajili ya kuboresha kiasi cha vitamin A katika miili yao. Kwa upande mwingine anasema vitamin A inahitajika kwa ajili ya ukuaji na maendeleo mazuri ya mtoto ikiwa ni pamoja na mifupa na macho. Upungufu wa vitamin A unahusishwa na ongezeko la vifo vya wanawake vinavyotokana na uzazi na vifo vya watoto.
Kutoona vizuri katika mwanga hafifu, watoto kuzaliwa kabla ya miezi tisa ya ujauzito, kasi ndogo ya ukuaji na maendeleo ya mtoto na kuongezeka kwa uwezekano wa mtoto kupata maradhi kama vile kuharisha na magonjwa ya mfumo wa hewa. Mratibu huyo anasema kuna njia mbalimbali za kuzuia upungufu wa vitamin A kwa watoto ambazo ni kuhamsisha unyonyeshaji maziwa ya mama pekee katika kipindi cha miezi sita ya mwanzo ya mtoto na kuendelea kunyonyesha hadi miaka miwili na zaidi.
Pia kumpa mtoto aliyefikisha umri wa miezi sita vyakula vya nyongeza ikiwa ni pamoja na vyakula vyenye vitamin A kwa wingi. Na kutoa nyongeza ya vitamin A kwa watoto yaani matone ya vitamin A. Kwa upande wake Mratibu wa Chanjo mkoa wa Dar es Salaam, Alex Mkamba anasema suala la minyoo linaathiri na kwa hapa Tanzania tatizo hilo ni kubwa sana.
Mkamba anasema imebainika kuwa karibu asilimia 89 ya mazingira yanayozunguka ni hatarishi kwa sababu ya utupaji duni wa vinyesi pamoja na mazingira kuwa machafu yanayosababishwa na watu kujisaidia ovyo. Pia asilimia 58 ya watu wanatumia vyoo ambavyo havina viwango na asilimia 42 ya watu wanatumia vyoo vinavyokubalika.
No comments:
Post a Comment