Friday, 8 January 2016

SHEHENA YA PETROLI YENYE SUMU YAPIGWA "STOP" DAR





Shirika la Viwango Tanzania (TBS) limezuia upakuaji  wa shehena ya mafuta ya petroli kutoka Umoja wa Falme za Kiarabu (UAE) yenye tani za ujazo 38,521 katika bandari ya Dar es Salaam kutokana na kuwa na madhara kiafya. 

Hatua hiyo ya TBS inatokana na sampuli za maabara kuonyesha mafuta hayo kuwa na kemikali zenye madhara kiafya, mazingira na viwango duni. Sambamba na hatua hiyo, TBS imezuia shehena ya mafuta ya vilainishi vya mitambo na magari ya kampuni ya HASS Petroleum (T) Ltd, yenye  lita za ujazo 16,080 kutoka nchini humo.
Mkurugenzi Mkuu wa TBS, Joseph Masikitiko, alisema jana jijini Dar es Salaam kuwa meli ya MT. Ridgebury John B iliyopakia shehena hiyo, iliwasili nchini ikiwa na mafuta yasiyo na vigezo vinavyotakiwa, hivyo  waagizaji hao kutakiwa kuyarudisha yalikotoka kwa gharama zao. Alisema madhara ambayo yamo katika mafuta hayo ni kuwadhuru kiafya watoa huduma, hususan wauzaji katika vituo vya mafuta, magari kuharibika na uharibifu wa mazingira kutokana na moshi mchafu wa mitambo unaotoka kwenye magari. Alisema mafuta hayo ambayo yana kemikali za ‘oxygenates’, yana uwezo wa kuvuta maji au mvuke kwa wingi, hivyo sehemu kubwa ya petroli huwa ya maji na kusababisha injini, mitambo na magari kuharibika kwa muda mfupi mara baada ya kununuliwa.
Kuhusu vilainishi, Masikitiko alisema vilizuiwa kuingia nchini na kampuni hiyo imetakiwa kuvirudisha katika nchi ilikozinunua.
Alionya kuwa waagizaji wanaoendelea kuagiza na kuuza matairi yaliyokwisha muda wake hata kama hayajatumika, watambue kuwa Tanzania si dampo la matairi mabovu. Alisema matairi hayo  husababisha ajali za barabarani na athari za kiuchumi, hivyo watakokiuka kuchukuliwa hatua za kisheria.
Alibainisha kuwa sheria na kanuni zilizopo bidhaa kabla haijaingia sokoni isipokuwa na viwango, mwagizaji hulazimika kulipia faini ya Sh. milioni 50 hadi Sh. milioni 100 ama kwenda jela kwa miaka mitatu.
CHANZO: NIPASHE

No comments:

 

ADVERTISE WITH US

AFRICAN FASHION

PLACE YOUR ADS HERE!