
Mwendo kasi kimeelezwa kuwa ndiyo chanzo cha basi la kampuni ya Luwinzo kugongana uso kwa uso na lori na kusababisha vifo vya watu wanne eneo la Kinegembasi Tarafa ya Kasanga Wilaya ya Mufindi mkoani Iringa.
Kamanda wa Polisi mkoani Iringa, Peter Kakamba, alisema ajali hiyo ilitokea jana majira ya asubuhi barabara kuu ya Iringa - Makambako kwa kuhusisha basi lenye namba za usajili T 782 AZR.
Kamanda Kakamba aliwataja waliofariki dunia katika ajali hiyo kuwa ni Rashid Kibalala (47), aliyekuwa kondakta wa basi hilo na Salim Changwila (28), aliyekuwa mfanyakazi wa gari hilo.
Aidha, alisema abiria wengine wawili ambao bado hawajafahamika majina yao, walifariki dunia wakiwa wanapatiwa matibabu katika Hospitali Teule ya Wilaya ya Mufindi.
Kamanda Kakamba alisema kuwa chanzo cha ajali hiyo ni mwendo kasi wa basi hilo wakati dereva akijaribu kulikwepa lori lililokuwa limeegeshwa kando kando ya barabara lenye namba za usajili namba za usajili T718 CRV na tela namba T 529 ART aina ya Iveco.
Alifafanua kuwa lori hilo lililokuwa limebeba makaa ya mawe, lilitokea Songea mkoani Ruvuma kuelekea mkoani Tanga.
Kwa mujibu wa Kamanda Kakamba, basi hilo lilikuwa likitokea mkoani Njombe kuelekea jijini Dar es Salaam.
Alisema abiria waliosajiliwa katika kitabu kabla ya kuanza safari walikuwa 35, lakini wengine ambao idadi yao haijafahamika, walipandia njiani.
Akizungumza kwa njia ya simu, Mganga Mfawidhi wa Hospitali ya Wilaya ya Mufindi, Dk. Innocent Mhagama, alisema alipokea miili miwili ya marehemu pamoja na majeruhi 32 ambao wanaendelea na matibabu hospitali hapo.
Dk. Mhagama alisema kuwa kati ya miili hiyo, mmoja umetambuliwa na kuchukuliwa na ndugu zao kwa mazishi.
Aidha, alisema kati ya majeruhi hao, mmoja hali yake ni mbaya na alipelekwa katika Hospitali ya Rufaa Iringa kwa matibabu zaidi.
“Watu wanne wamekufa katika ajali hiyo, wawili walifia eneo la ajali na wawili wengine katika Hospitali Teule ya Wilaya ya Mafinga," alisema Dk. Mhagama.
No comments:
Post a Comment